Maisha yetu hapa duniani, ni kama tumetegwa hivi, tumewekewa vitu vizuri ambavyo tunapenda kuvifanya, lakini vitu hivyo havifanyi maisha yetu kuwa bora. Na wakati huo huo kuna vitu vipo, ambavyo hatupendi kuvifanya lakini hivi ndivyo vinafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Hapa ndipo changamoto kubwa inapoanzia, kwa sababu mwili unataka kingine na akili inataka kingine.

Kwenye afya, kuna vitu vizuri sana vya kula na vyenye ladha, lakini hivi havifanyi afya zetu kuwa bora. Pia kuna vitu vizuri sana vya kunywa, lakini hivi havifanyi maisha na afya zetu kua bora. Njia ya kuwa na afya bora ni kula usichopenda na kunywa usichotaka, hasa pale unapokuwa na uwezo wa kula na kunywa chochote.

Kwenye maisha yetu ya kawaida, kulala ni kuzuri na tunakupenda, kupumzika ni raha na kila mmoja wetu anapenda kupumzika. Lakini kulala na kupumzika hakuwezi kutuletea mafanikio, tunahitaji kuamka na kuweka juhudi kwenye kile tunachofanya. Tunahitaji muda wa kulala, na muda wa kupumzika, lakini siyo muda mwingi kama ambavyo tunataka, ni muda kidogo ili tuweze kupata muda wa kutosha kufanya shughuli zetu. Hivyo tunahitaji kuacha kile tunachopenda, na kufanya kile tusichopenda.

SOMA; Salamu Za Mwaka Mpya Kutoka Kwa Rais Wa Tanzania Mwaka 2040.

Kwenye safari yetu ya mafanikio, kila mtu anapenda njia ya mkato, kila mtu anataka kufika haraka, kila mtu anataka kuweka juhudi kidogo na kupata matokeo makubwa. Lakini njia hii inawapoteza wengi, wengi wameshindwa kufikia malengo yao kwa kupoteza muda kwenye njia hizi za mkato.

Leo wacha nikupe njia moja rahisi kabisa ya kujua kama kitu ukifanye au la, hasa pale unapokuwa njia panda. Jiulize je ni kitu ambacho mwili wako utafurahia kufanya? Na pia angalia ni kitu ambacho kila mtu anakimbilia kufanya? Kama majibu ni ndiyo basi fanya kinyume na kitu hicho. Maana kitu chochote ambacho mwili wako unapenda kufanya na kila mtu anakimbilia kukifanya, siyo kitu bora. Hii ni kwenye afya, kazi, biashara na mafanikio kwa ujumla.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)