Vinavyotuzuia kufanikiwa ni vingi kuliko vinavyotuhamasisha kufanikiwa, ndiyo ukweli wa maisha ulivyo na ndiyo sababu wachache ndiyo waliofanikiwa, huku wengi wakikazana lakini wasiyaone mafanikio.
Ili kuyafikia mafanikio ni muhimu kujua kila njia ya kukufikisha kwenye mafanikio, na pia kujua zile njia ambazo zitakuzuia kufanikiwa. Ni kazi ngumu kujua haya yote, na kwa mara nyingine tena ndiyo sababu kwa nini wachache ndiyo waliofanikiwa.
Vikwazo vya mafanikio vinaanzia ndani yetu wenyewe na baadaye vinatoka kwa wale wanaotuzunguka na mazingira pia.
Ndani yetu kuna uvivu, uzembe na ujinga ambavyo vimekuwa vinatuzuia kuchukua hatua kubwa za kuboresha maisha yetu.
Wale wanaotuzunguka wanatukatisha tamaa kutokana na uvivu, uzembe na ujinga wao, ambao wanaamini kila mtu anapaswa kuwa nao.
Na mazingira hayajabaki nyumba, kuna changamoto nyingi zinatokana na mazingira ambazo hazijali wewe umepenga nini. Unakwenda kulima ukiwa umejipanga vizuri kabisa, ukitegemea mvua zitanyesha halafu hazinyeshi, au zinanyesha mpaka zinaleta mafuriko yanabeba mazao yako.
Hii ni vita ngumu ambayo huwezi kuishinda kwa urahisi, ni lazima uwe umeamua hasa kutoka ndani ya moyo wako kwamba utapambana mpaka tone la mwisho, ili uweze kupata kile ambacho unataka kupata.
Inawezekana lakini siyo rahisi, njia pekee kwako kufika unakotaka ni kufanya. Jiandae vya kutosha lakini jua majibu yatatokana na kufanya, hivyo kuwa tayari kufanya. Na kuwa tayari kupokea matokeo ambayo huenda huyapendi, na uyatumie kufanya maamuzi bora zaidi kwako.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)