Lengo la kila mmoja wetu ni kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

Kuwa na biashara yenye mafanikio, inayokua na kutuletea faida kubwa mara zote.

Tuwe na kazi zenye mafanikio, ambapo tunafanya makubwa na kupata matokeo makubwa.

Na maisha yetu kwa ujumla yawe ya mafanikio, chochote tunachogusa kinageuka kuwa mafanikio, tuwe na mkono wa maajabu ambapo kila tunachogusa kinageuka dhahabu.

Hii ni ndoto nzuri, na ndicho tunacholenga kwenye maisha yetu.

Lakini kwa bahati mbaya sana uhalisia haupo hivi, utapanga vizuri biashara lakini unapoingia utapata hasara, utakutana na changamoto na mengine ya kukurudisha nyuma.

Utapanga vizuri namna ya kuboresha kazi yako, lakini unapofika kwenye kazi unakutana na vikwazo vingi, kuanzia kwa wafanyakazi wenzako mpaka mwajiri wako. Wengine wanakuona wa ajabu, wengine hawathamini kile unachofanya. Na hapo bado hujakosea na kuharibu mengine ambayo watu walikuwa wamefanya tayari.

Umepanga kuingia kwenye kilimo, una mahesabu yako vizuri ya mwisho wa msimu utavuna kiasi gani kwa mtaji ulioweka, lakini unafikia mavuno na hupati hata ile fedha uliyowekeza.

Huu ndiyo uhalisia wa maisha, na una faida kubwa sana kwetu.

Je ni faida gani? Tuione faida kwa kuangalia kinyume cha hali hiyo.

Kuna hatari kubwa sana ya kufanikiwa kwenye kila kitu, kwenye kupata matokeo mazuri kwenye kila unachogusa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DEEP WORK (Mbinu Za Kufanya Kazi Yenye Maana Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu).

Hatari ya kwanza ni kujiona unaweza sana na hivyo kusahau kujifunza, hapa unaona wewe ndiyo wewe na unasahau kujifunza na hivyo unajiandaa kushindwa zaidi baadaye.

Hatari ya pili ni kufanya kile ambacho umezoea kufanya. Kama hupati changamoto yoyote, ni dalili tosha kwamba hakuna makubwa unayofanya, unafanya yale uliyozoea kufanya kila siku na unapata matokeo yale yale, unaogopa kufanya mapya kwa sababu hujui ni matokeo gani utapata.

Hivyo ni wakati wa kujitathmini sasa, iwapo unafanikiwa kwenye kila kitu, angalia kama kuna makubwa unayofanya na usijisahau na kuja kushindwa zaidi baadaye.

Na iwapo unashindwa kwenye yale unayofanya, hakikisha kuna masomo unajifunza na kuyatumia ili kufanikiwa zaidi.

Mafanikio ni safari, usikubali chochote kikuzuie njiani.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)