Matatizo ni sehemu ya maisha yetu, changamoto na vikwazo havikosekani kwenye safari yetu ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Hili tunalijua, lakini siyo rahisi pale ambapo matatizo yako upande wako.
Unapokuwa kwenye matatizo, kila unachojua kinahama na unabaki kufikiria kuhusu matatizo uliyonayo. Na hapa ndipo tunapofanya makosa makubwa sana kwenye maisha yetu, yanayopelekea sisi kukata tamaa.
Mara nyingi tunapokuwa kwenye matatizo, tunaona kama tatizo tulilonalo ni la kudumu, kama vile tatizo hilo litadumu na sisi maisha yetu yote, na hivyo kuwa na maisha ya hovyo. Hii inatokana na jinsi tunavyoyachukulia maisha yetu wakati wa matatizo haya.
Ukweli ni kwamba hakuna tatizo linalodumu milele, hakuna tatizo linaloweza kuathiri maisha yako yote, na kila tatizo unalopitia sasa litapita kama utaweka juhudi katika kulitatua.
Wote tunajua hakuna kitu kinadumu milele, na hata matatizo yako pia, hayawezi kudumu milele, baada ya muda kila tatizo linakwisha, lakini usisubiri tatizo liishe lenyewe, bali fanyia kazi ili kulitatua.
Hakuna tatizo linaloweza kuathiri maisha yako yote, yaani kila eneo la maisha yako limeathiriwa na tatizo moja. Hivyo unapokuwa na matatizo, usiangalie ule upande ambao una tatizo pekee, bali angalia maisha yako yote, na utaona upande mwingine ambao uko vizuri na utapata hamasa ya kuendelea kuweka juhudi. Ukiangalia matatizo pekee utakata tamaa.
SOMA; ONGEA NA KOCHA; Tabia Moja Inayokuingiza Kwenye Matatizo Na Kukunyima Fursa Nyingi.
Hili pia litapita, ni kauli ambayo inaweza kuwa na matumizi kwenye maeneo mengi ya maisha yetu, na hata kwenye matatizo pia. Wewe fanyia kazi kutatua matatizo yako, na hayatabaki kama yalivyo sasa, utafika wakati na yatapita.
Hakuna tatizo la kudumu, kila kitu kinapita, na usiruhusu maisha yako yote kuvurugika kwa sababu ya matatizo unayopitia. Maisha yako yapo juu ya matatizo yako, usikubali kuyavuruga.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)