USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Changamoto Ya Kukaribisha Matatizo Pale Unapokuwa Na Fedha.

Hivi umewahi kugundua ya kwamba kila unapokuwa na fedha ndipo matatizo yanayokuhitaji utumie fedha hizo yanakuwa mengi? Kwamba unapokuwa huna fedha hupati matatizo makubwa, ila ukishakuwa tu na fedha, mara mtoto ataumwa, au mazazi atapata shida, au wewe mwenyewe utajikuta kwenye changamoto ambayo inahitaji fedha? Unatumia fedha uliyoipata kutatua tatizo ulilokutana nalo na kushindwa kutekeleza mipango yako mingine! Basi hili ndiyo tunakwenda kujadili leo kupitia makala hii ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufanikiwa.

Habari rafiki yangu, karibu tena kwenye kipengele chetu hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Tunajua ya kwamba changamoto ni sehemu ya maisha, hatuwezi kuzikwepa wala kuzikimbia, njia pekee ya kukabiliana na changamoto ni kuzitatua, na hapa ndipo tunapopeana mbinu muhimu za kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo kwenye safari yetu ya mafanikio.

Leo kama nilivyokudokezea hapo mwanzo, tunaangalia changamoto ya kukaribisha matatizo pale unapokuwa na fedha. Hiki ni kitu ambacho kimekuwa kinatokea kwa watu wengi, wakati huna fedha huoni kabisa matatizo, lakini unapozishika fedha ndiyo matatizo yanajipanga kwa foleni, unajikuta fedha yote uliyopata imeishia kwenye matatizo, ambayo hata hukuwa nayo awali. Nimewahi kumsikia mtu akisema, watoto wake huwa wanaumwa kila mwisho wa mwezi, pale anapopokea mshahara wake. Ni tatizo kubwa ambalo limewazuia wengi kuweza kufanyia kazi malengo ya maisha yao.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html
KUPATA KITABU HIKI BONYEZA PICHA AU MAANDISHI HAYA.

Sasa leo tunakwenda kumalizana na tatizo hili ili tuweze kupunguza vikwazo kwenye safari yetu ya mafanikio. Kabla hatujaanza kujadili ni hatua zipi za kuchukua ili kuondokana na tatizo hili, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Sema kweli mimi nikipata pesa ili nianzishe biashara yangu ndipo matatizo yanajitokeza na kujikuta natumia fedha yote kwenye matatizo hao, nifanyeje! Chacha N. W.

Changamoto anayopitia msomaji mwenzetu ni changamoto ambayo imewasumbua wengi na kuwazuia kufikia mafanikio kwenye maisha yao. Je tunawezaje kutatua changamoto hii ili tuweze kuishi maisha ya ndoto zetu?

SOMA; Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

Hapa nakushirikisha mambo matatu muhimu kufanya ili kuondokana na changamoto ya kuwa na matatizo pale unapopata fedha.

Jambo la kwanza; acha kuyakaribisha matatizo.

Unaweza kushangaa, lakini ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya matatizo unayoyapata wakati unapokuwa na fedha unakuwa umeyakaribisha mwenyewe. Kwa sababu hakuna namna nyingine kwa ni i ukiwa huna fedha huoni matatizo, ila ukizishika tu matatizo lukuki yanajitokeza.

Na hii yote inaanzia kwenye akili yako, unapokuwa huna fedha, unapokutana na matatizo yanayohitaji fedha huhangaiki nayo kwa sababu huna fedha. Mengi unayapotezea na mengine kuyavumilia, kwa sababu huna njia ya kuyatatua. Ila pale unapokuwa na fedha, matatizo yale yale ambayo uliyapotezea na kuyavumilia ulipokuwa huna fedha yanapotokea tena, huyavumilii, badala yake unayatekeleza mara moja. Kwa njia hii unakuwa umeiweka akili yako kwenye hali ya kuangalia matatizo ya kutatua pale unapokuwa na fedha.

Sasa si unakumbuka kwamba tunapata kile ambacho tunakitafuta? Hivyo akili yako inakutii na kukuletea kile ambacho unatafuta, unapokuwa na fedha. Ukiwa huna fedha mtu akikueleza matatizo yake unayachuja sana ikiwa anahitaji msaada wako kweli au la. Mara nyingi unakuta hana uhitaji mkubwa sana. Ila unapokuwa na fedha mtu akikueleza tu tatizo lake unakimbilia kulitatua, hata bila ya kufikiri kwa kina ili kuona kama tatizo hilo linahitaji msaada wako kwa haraka kiasi hicho.

Hatua ya kuchukua ili kuondokana na hali ya kukaribisha matatizo ni kuepuka kuwa na viwango tofauti kwa tatizo moja pale unapokuwa una fedha na usipokuwa na fedha. Chunguza kila tatizo kama kweli linahitaji kutatuliwa kwa uharaka au linaweza kusubiri.

SOMA; Mambo 6 Yakukusaidia Kujua Shughuli Iliyokuleta Duniani.

Jambo la pili; fedha zisikubadilishe tabia.

Kuna watu ambao wakiwa hawana fedha na wakiwa nazo utawajua. Wakiwa hawana fedha utawakuta wamenyong’onyea, wanawahi kurudi nyumbani, hawaonekani kwenye maeneo yao ya kawaida. Kwa kifupi wanakuwa kama wana msiba. Lakini subiri pale wanapozikamata fedha, kila mtu atajua kabisa kwamba sasa wana fedha, atakuwa mchangamfu, ataonekana sehemu za matumizi na wengine kusema hadharani kwamba fedha wanazo.

Hali kama hii huwakaribisha watu ambao huenda hawana matatizo makubwa sana, lakini kwa kuwa wanaona una fedha, basi wanaleta matatizo yao. Kwa njia hii unajikuta unatoa fedha ili kuwasaidia. Muda wote hawakukuletea matatizo yao kwa sababu walijua huna fedha, hivyo hawatapata msaada. Sasa unaona, waliweza kuyavumilia matatizo hayo, ila kwa kuwa wamekuona unajionesha kuwa na fedha, basi na wao wanakuja na matatizo na amhitaji yao.
Hii inatokea kwa wale watu ambao ni wa karibu sana kwako, hivyo huwezi kuwakatalia.

Namna ya kuondokana na hili ni kuacha kuendeshwa na kubadilishwa tabia na fedha. Unahitaji kuwa mtu yule yule nyakati zote, iwe una fedha au huna. Kwanza kabisa usiruhusu mtu aweze kujua kama una fedha au huna kwa kuangalia tabia zako. Jijengee nidhamu ya fedha kwa kudhibiti matumizi yako na wale wanaokuzunguka watakuletea zile shida ambazo ni kubwa kweli, na siyo shida ndogo ndogo ambazo hata wao wenyewe wangeweza kuzitatua.

SOMA; TATIZO SIO FEDHA, TATIZO NI WEWE…..

Jambo la tatu; kuwa na fedha za dharura.

Kwa hayo mawili tuliyojadili hapo juu, hayaondoi yale matatizo ambayo ni makubwa na yanatuhitaji kuyachukulia hatua. Pale ambapo mtu kweli anaumwa na anahitaji kutibiwa, au kuna dharura imetokea na inatakiwa kutatuliwa. Hapa ndipo unahitaji kuwa na fedha za dharura. Fedha hizi utazitumia kwenye nyakati za dharura kweli, pale ambapo umepata tatizo au changamoto kubwa na inahitaji kutatuliwa haraka.

Hakikisha unakuwa na utaratibu wa kutenga fedha ya dharura kwenye kila kipato unachopokea, usitumie fedha mpaka iishe yote, tenga fungu la dharura. Unaweza kutenga angalau asilimia kumi ya kipato chako kila mwezi au kila unapopata kama sehemu ya dharura. Kwa njia hii matatizo yanayotokea hayataingilia ratiba zako.
Hayo ndiyo mambo matatu muhimu kuzingatia ili kuepuka matatizo kukunyemelea pale unapopata fedha. Yafanyie kazi ili kuzuia matatizo kuwa kikwazo cha wewe kutimiza ndoto zao kwenye maisha.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s