Maisha yetu yanaathiriwa na kila kitu ambacho tunachagua kufanya au kutokufanya.
Yaani upo hapo ulipo sasa, kutokana na mambo ambayo ulifanya au ulishindwa kufanya huko nyuma. Na kile unachofanya leo, au unachoshindwa kufanya, ndiyo kinaamua maisha yako ya kesho yaweje.
Kitu ambacho kimekuwa kinawashinda wengi kwenye maisha yao, ni kufanya maamuzi ambayo ni muhimu kwa maisha yao. Kwa sababu kufanya maamuzi ni kugumu, na wale wanaowazunguka wamekuwa wakichangia watu kuogopa kufanya maamuzi fulani, basi wengi wamekuwa wakiahirisha kufanya maamuzi.
Lakini watu kutokufanya maamuzi hakuwafanyi wawe upande salama, badala yake kunawafanya wawe na maisha magumu zaidi. Mtu anaweza kuona anakwepa kufanya maamuzi magumu kwenye maisha yake, lakini anajikuta akiangukia kwenye maamuzi magumu ya wengine.
Iko hivi, kama hutafanya maamuzi ya maisha yako, wengine watakufanyia maamuzi hayo. Na kama unavyojua, sifa ya kwanza ya binadamu ni ubinafsi, hivyo maamuzi watakayokufanyia wengine, yatakuwa na manufaa kwao kuliko yalivyo na manufaa kwako. Huu ndiyo upande mbaya wa kutokufanya maamuzi.
Kama huna nidhamu ya kuweza kukaa chini na kufanya maamuzi magumu ya maisha yako, wengine watakufanyia maamuzi hayo na watakupa nidhamu ya kutekeleza maamuzi hayo, ambayo yana msaada zaidi kwao kuliko kwako.
SOMA; Usifanye Maamuzi Yako Kwa Kigezo Hiki, Utajuta Sana…
Nakuambia hili ili ukumbuke kufanya maamuzi yote muhimu ya maisha yako, kwa sababu wewe ndiye muumbaji wa maisha yako, usimpe mtu mwingine jukumu hilo, atakupoteza kwa sababu anajifikiria yeye zaidi.
Kuepuka kufanya maamuzi hakukuondolei mzigo, badala yake kunakupoteza zaidi, kwa kuwapa wengine ruhusa ya kukufanyia wewe maamuzi na kukutumia kufikia ndoto zao.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)