Anthony Robbins ni mwandishi na mhamasishaji ambaye ameyatoa maisha yake katika kuwasaidia wengine kufikia maisha ya ndoto zao. Yeye mwenyewe ameanzia kwenye mazingira magumu ambayo yalimpa hamasa ya kuweka juhudi ili kuwa na maisha bora. Aliweza kutoka kwenye mazingira magumu na kujitoa kuwafundisha na kuwahamasisha wengine ili nao waweze kuwa na maisha bora. Tony amenadika vitabu kadhaa kwenye eneo la maendeleo binafsi ya mtu, na pia amekuwa akiendesha semina ambazo zimeleta mabadiliko kwa wengi.
Katika kitabu chake tunachokwenda kuchambua leo, NOTES FROM A FRIEND, Tony anatushirikisha yale muhimu ambayo amekuwa akiyaandika na kuyahubiri kwenye semina zake. Ni mambo mazuri ambayo mtu yeyote akiyazingatia anaweza kubadili maisha yake.

Tony Robbins amekuwa akisimamia falsafa moja kwenye maisha yake, falsafa hiyo anaiita CANI, kifupi cha CONSTANT AND NEVER ENDING IMPROVEMENT, ikiwa na maana kwamba maboresho yasiyokuwa na kikomo. Hii ina maana kwamba kama unataka kuwa na maisha mazuri na ya ndoto yako, basi unahitaji kuwa bora kila siku ya maisha yako. Hii ndiyo kazi kubwa ambayo tumekuwa tunaifanya kupitia kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA, kuhakikisha kila siku kwetu inakuwa bora sana.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wahitimu Wa Elimu Ya Juu Mwaka 2016, Ukweli Ambao Umekuwa Unafichwa Kwa Miaka 20 Iliyopita.

Karibu kwenye uchambuzi wetu wa kitabu hiki ili tuweze kujifunza yale ambayo yatakwenda kubadili maisha yetu.

1. Njia pekee ya kujihakikishia furaha kwenye maisha yako ni kuwasaidia wengine kuwa na furaha kwenye maisha yao. Elewa vizuri hapo, siyo kuwafurahisha, bali kuwawezesha kuwa na furaha. Hakuna anayeweza kumpa mtu mwingine furaha, furaha zinaanza na sisi wenyewe. Hivyo chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kinayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, watakuwa na furaha na wewe utakuwa na furaha.

2. Ili kuwa na maisha bora, ili kujihakikishia kipato kwenye jambo lolote unalofanya, kila siku jiulize swali hili; ni kwa njia hani naweza kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine? Iwe ni kwenye biashara au kazi, ukijiuliza na kujibu swali hilo, na kisha kufanyia kazi majibu yako, utafanya kilicho bora na utafurahia maisha yako, na kipato chako kitakuwa kizuri mara zote. Mafanikio yetu yapo kwenye mafanikio ya wengine, ukiona hufanikiwi jua kwamba hujawawezesha wengine kufanikiwa au kuwa na maisha bora, anza na swali hilo kila siku.

3. Kufikiri chanya ni hatua moja muhimu kwenye kuwa na maisha ya mafanikio, lakini kufikiri chanya pekee hakutoshi kukufanya wewe uwe na maisha bora, unahitaji kuchukua hatua, na siyo hatua ndogo, bali hatua kubwa. Unahitaji kufikiri chanya, na wakati huo ukiwa na mipango na mikakati ya kufikia malengo yako kwenye maisha. Maisha yako hayatabadilika kwa kufikiri pekee, bali kwa kuchukua hatua za kuyabadili. Ni hatua gani unachukua kwa sasa ili kuboresha maisha yako?

4. Mabadiliko makubwa unayotaka kufanya kwenye maisha yako, yamegawanyika kwenye maeneo haya mawili muhimu;
Moja; unataka kubadili hisia zako juu ya vitu au maisha yako. kuna namna ambavyo unahisi au kufikiri maisha yako ambayo huipendelei, hivyo unataka kubadili hisia hizo.
Mbili; unataka kubadili matendo yako, unataka kufanya kitu cha tofauti na unachofanya sasa, unataka kubadili tabia ambayo unayo sasa.
Changamoto kubwa ni kwamba japokuwa kila mtu anataka kufanya mabadiliko kwenye maisha yake, ni wachache sana wanaoyafanya kweli, na katika hao wachache, ni wachache zaidi wanaodumu na mabadiliko hayo.

5. Jana yako siyo sawa na kesho yako. Watu wengi wamekuwa wakijikatisha tamaa ya kuchukua hatua kubwa ya kubadili maisha yao kwa sababu ya historia zao za nyuma. Kwa sababu huko nyuma walijaribu kufanya vitu wakashindwa, au kwa sababu wametokea mazingira mabovu, huwa wanaona hawawezi. Unachotakiwa kukumbuka ni kwamba haijalishi jana yako ilikuwaje, kesho ni siku nyingine tofauti, ambayo una uhuru wa kufanya chochote utakacho.

6. Ung’ang’anizi unalipa, na hii ndiyo sifa pekee inayowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Utawasikia walioshindwa wakikuambia nimejaribu sana lakini sijaweza, lakini ukihesabu mara walizoshindwa huenda ni mara tano au kama ni sana basi mara kumi. Kuna watu walijaribu zaidi ya mara elfu moja ndiyo wakapata walichotaka, na hawa ni wengi mno katika wale waliofanikiwa. Hivyo kama hujajaribu zaidi ya mara elfu moja, usituambie kwamba umejaribu mara nyingi ukashindwa, endelea kung’ang’ana na utapata unachotaka.

SOMA; USHAURI; Biashara Nzuri, Inayolipa Na Unayoweza Kuifanya.

7. Pamoja na kwamba unahitaji kuwa king’ang’anizi ili kufanikiwa, haimaanishi kwamba uendelee kufanya kitu kile kile ambacho umekuwa unafanya kila siku. Badala yake unahitaji kuboresha kadiri unavyokwenda, kila unapofanya na kushindwa, jifunze ni kipi unakosea na fanya marekebisho. Wanasema ujinga ni kufanya kitu kile kile kwa njia ile ile na kutegemea matokeo tofauti, usiwe mjinga, kuwa king’ang’anizi kwa kujifunza na kuboresha zaidi.

8. Tony anatupa ujumbe mmoja muhimu sana, ambao anashauri sana tutoke nao kwenye kitabu hiki na tuufanyie kazi, ujumbe huu ni kuchukua hatua KUBWA na kwa mwendelezo. Iko hivi, watu wengi wamekuwa hawachukui hatua, na wale ambao wanachukua hatua wanachukua hatua ndogo sana kiasi kwamba hata wakipata matokeo hayawi bora kwao. Ila pia wale ambao wanachukua hatua hawana mwendelezo, wanaanza baadaye wanashindwa kuendelea au wanakata tamaa. Sasa sikia rafiki, unapoamua kuchukua hatua, CHUKUA HATUA KUBWA NA KWA MWENDELEZO, usiwe mtu wa kugusa na kuacha, kuwa mtu wa kuendeleza kile ulichoanza.

9. Ili uweze kuchukua hatua za kubadili maisha yako na kuwa bora zaidi, unahitaji kufanya MAAMUZI, sasa hili neno maamuzi limekuwa linatumia kirahisi sana mpaka watu wanaona kuchukua maamuzi ni kitu ambacho hakina uzito. Na wengine hawajawahi kuchukua maamuzi kwa muda mrefu mpaka wamesahau maana halisi ya kuchukua maamuzi. Tony anatuambia kwamba unapofanya maamuzi, maana yake unaamua hiyo ndiyo njia unayochukua, na hakuna cha kukurudisha nyuma, haijalishi unakutana na nini. Unapofanya maamuzi maana yake unaweka kila sababu pembeni na kuweka kila ulichonacho kwenye kile ulichoamua.

10. Maamuzi yanayofanyiwa kazi ni yale ambayo yanaaminiwa. Hivyo unahitaji kuwa na imani kwenye kile ambacho unakifanya, kama huna imani, hakuna chochote utakachofanya kikakusaidia. Kwa sababu unapokosa imani unaifunga akili yako, hata kitu ambacho kipo wazi kabisa, wewe hutakiona. Hivyo kuwa na imani kwamba unaweza na pia kile unachotaka kinawezekana, kwa njia hii utafungua akili yako na utaziona fursa nyingi.

11. Kwenye safari ya mafanikio hakuna kitu kinaitwa KUSHINDWA, Badala yake kuna kitu kinaitwa KUJIFUNZA. Kama umefanya kitu na ukapata matokeo tofauti na uliyotegemea, hujashindwa, badala yake umejifunza njia ambayo haifai, hivyo unaporudia tena, usitumie njia uliyotumia awali. Ukiwa na mtazamo huu, kamwe huwezi kukata tamaa. Lakini pale unapofikiria kukosa unachotaka ni kushindwa, utakosa nguvu ya kuendelea na mapambano.

12. Mafanikio ni matokeo ya kufanya maamuzi bora, kufanya maamuzi bora ni matokeo ya uzoefu tulionao, na uzoefu tulionao unatokana na maamuzi mabovu tuliyofanya. Hivyo usijilaumu kama unafanya maamuzi mabovu kwa sasa, unayahitaji ili uwe na uzoefu wa kuweza kufanya maamuzi mazuri. Jifunze kwenye kila kitu unachofanya, jifunze kwenye kila hali unayopitia na tumia uzoefu huo kufanya maamuzi bora zaidi.

SOMA; KITABU CHA MAY; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

13. Ili kubadili maisha yako yaweze kuwa bora kabisa kuanzia leo, unahitaji kufanya maamuzi haya mawili, leo hii na siyo kesho. Yaani fanya maamuzi haya sasa hivi;
Moja; fanya maamuzi madogo ambayo ni rahisi kwako kufuata kila siku. isiwe kitu kigumu au kikubwa ambacho kinakuhitaji ufanye mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. maamuzi haya madogo, yatabadili maisha yako kadiri unavyofanya kila siku.
Mbili; fanya maamuzi makubwa, ambayo yanakuhamasisha kuchukua hatua kubwa. Maamuzi haya yanakuwa ya kile kitu kikubwa unachotaka kwenye maisha yako.
Ni muhimu kuwa na maamuzi haya mawili, kwa sababu yale madogo yatakupa ushindi wa kila siku, na yale makubwa yatakupa matumaini ya siku zijazo. Kila siku chukua hatua kufikia maamuzi uliyojiwekea.

14. Kule unakopeleka mawazo yako ndiyo chanzo cha furaha au huzuni kwenye maisha yako. watu wenye huzuni na wanaokata tamaa ni wale ambao wanafikiria mambo mabaya wakati wote. Wao kwenye maisha yao wanaona mambo mabaya pekee, wanatumia muda mwingi kufikiria mambo hayo mabaya na hii inawakatisha tamaa. Wale ambao wanakuwa na furaha na hamasa ya kufanya zaidi wanaona mazuri kwenye maisha yao, wanatumia muda mwingi kufikiria hayo mazuri. Hivyo unapojikuta kwenye hali ya huzuni na kukata tamaa, jiulize ni maeneo gani ya maisha yako umekuwa unayafikiria kwa muda mrefu, kama unafikiria mabaya, lazima utakuwa na huzuni na kukata tamaa.

15. Kubadili hisia zako na mawazo yako, anza kwa kubadili mwili wako. Kama umekaa kizembe, utakuwa na hisia mbaya na kuwa na mawazo ya huzuni na kukata tamaa, lakini kama umekaa kikakamavu, unakuwa na hisia nzuri na kuwa na hamasa. Tony anatuambia, kulingana na tafiti zilizofanywa, tunaweza kubadili hisia zetu na mawazo yetu kwa kubadili miili yetu. Hivyo kama umekaa mahali na unaanza kuona unakuwa na mawazo na hisia hasi, nyenyuka na anza kufanya mambo yanayoashiria ushujaa. Unaweza kutembea au kuruka au kufanya chochote kinachochangamsha mwili wako. Kuna namna ya kutembea, kuongea na hata muonekano wa nje ambao unaendana na maisha ya mafanikio. Jua namna hizo na zijenge kwenye maisha yako.

16. Maneno tunayojiambia na kuwaambia wengine kila siku yana nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu, hivyo ni muhimu uyachague maneno yako kwa uangalifu. Unahitaji kutumia maneno ambayo yanaashiria mafanikio na maneno hayo yatakufanya ufikiri kwa mafanikio muda wote. Kwa mfano mtu akikuuliza unajisikiaje, usimwambie tu unajisikia vizuri au unajisikia kawaida, mwambie unajisikia vizuri sana, au hujawahi kujisikia bora kama wakati huo. Kwa njia hii hata kama hujisikii bora, utalazimika kujisikia bora. Mara zote tumia maneno yanayoashiria mafanikio, na utalazimisha akili yako kuona mafanikio.

17. Jinsi unavyoiona dunia, jinsi unavyoyaona maisha , ndivyo unavyotengeneza maisha yako. Kuna ambao wanaona maisha ni vita, hivyo kila mtu anapambana na mwingine, mtu huyu atalazimika kupambana na wengine ili kupona. Kuna ambao wanaona masiha ni mchezo, hivyo wanacheza sehemu yao ili kupata wanachotaka. Dunia moja lakini tuna mitazamo tofauti, hakikisha wewe una mtizamo utakaoendana na maisha unayotaka.

18. Hatua ya kwanza kabisa ya kufanikiwa kwenye maisha yako, ni kuweka malengo. Tumekuwa tunawaona watu ambao wamefanya makubwa, ambayo wengi hawajaweza kufanya, na mara nyingi tumekuwa tunashawishika kwamba watu hawa wana bahati, au walikuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi. Lakini ukweli ni kwamba watu hawa walikaa chini na kuweka malengo jua ni i wanataka kwenye maisha yao, na wakafanyia malengo hayo kazi na hatimaye kuyafikia. Je wewe una malengo gani? Je umeyaandika malengo hayo? Unayafanyia kazi kila siku?

SOMA; Mambo Kumi (10) Kuhusu Maisha Na Mafanikio Niliyojifunza Kutoka Kwa Edward Ngoyai Lowassa.

19. Usijiwekee kikomo kwenye uwezo wako na kile unachofanya. Mara nyingi sisi wenyewe tumekuwa tunajizuia kufanikiwa, kwa kujiambia kwamba hatuwezi kufanya makubwa, au kwamba tutashindwa. Leo jiulize swali hili; kama ungehakikishiwa kwamba huwezi kushindwa kwenye kile ambacho umechagua kufanya, je ungefanya nini? Hofu ya kushindwa imekuwa inatuzuia kuziendea ndoto zetu. Hebu weka hofu hii pembeni, hebu weka vikwazo hivyo pembeni na ona maisha yako kwa picha tofauti kisha chukua hatua.

20. Zoezi la siku kumi; kwa siku kumi, kuanzia kesho, dhibiti mawazo yako na hisia zako. Usikubali kabisa kufikiria jambo lolote hasi, wala usitoe maneno yoyote hasi, usilalamike wala kulaumu mtu yeyote. Zifanye siku kumi zijazo kuwa siku za wewe kuwa chanya na kuchukua hatua, na siyo kujishusha na kujikatisha tamaa. Ikiwa siku yoyote katika siku hizo kumi utajikuta umefikiri au kusema kitu hasi, basi kesho yake anza upya, fanya hivi mpaka utakapoweza kwenda siku kumi bila ya kuwa hasi. Fanya zoezi hili na utaona jinsi ambavyo amisha yako yanaweza kubadilika kwa nafasi kubwa.
Haya ndiyo mambo muhimu tunayapata kwenye kitabu cha rafiki yetu Anthony Robbins, yafanyie kazi ili kuboresha maisha yako zaidi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita