Kuna watu ambao ni mashujaa, watu ambao tunawaona wana uthubutu mkubwa na kuweza kufanya yale yaliyowashinda wengine. Kila mmoja anapenda kuwa shujaa, japo ni wachache wanaofikia kiwango hiko.

Kuna watu ambao ni waoga, watu ambao hawathubutu kufanya mambo makubwa. Watu ambao wapo tayari kufanya kwa ukawaida ili tu wasijiingize kwenye matatizo.

Kwa nje tunawaona watu hawa wa aina mbili kama watu tofauti sana, tunaona kama mashujaa kuna kitu cha ziada ambacho wanacho na waoga wamekosa kitu hiko.

Lakini tunapoingia ndani na kuangalia kwa umakini, tunagundua ya kwamba mashujaa na waoga wote wana kitu hiki kimoja, kinachofanana kwao.

Kitu hicho ni hofu, shujaa ana hofu na mwoga naye ana hofu. Kinachowatofautisha watu hawa wa aina mbili ni namna wanavyoichukulia hofu hiyo. Na hapa ndipo tabia zao tofauti zinapoonekana.

Mashujaa wanatumia hofu zao kuwahamasisha kuchukua hatua, hutumia hofu walizonazo kama sababu ya kuchukua hatua, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kuondokana na hofu zao zaidi ya kuchukua hatua.

Kwa upande wa pili, waoga wanatumia hofu zao kuwazuia kuchukua hatua. Hofu zao zinawafanya wakimbie na hivyo kushindwa kabia kuchukua hatua.

SOMA; KUJIAMINI; Umuhimu Wa Tabia Ya Kujiamini.

Swali la kizushi; je mashujaa/waoga wanazaliwa au wanatengenezwa?

Kama umesoma mpaka hapa, jibu tayari unalo, watu hawa wanatengenezwa, kutokana na mazingira waliyokulia na hatua ambazo wamekuwa wakichukua.

Hivyo kama upo upande wa waoga, umekuwa unashindwa kuchukua hatua, anza kuziangalia hofu zako kwa upande wa pili. Usione hofu kama kitu cha kukumaliza, bali ichukulie kama kitu cha kukuhamasisha.

Kama hofu uliyonayo kwenye kuanza au kukuza biashara yako ni kupata hasara na kushindwa, tumia hiyo kama hamasa, kwamba uanzeje biashara ambayo haitashindwa wala kufa na itakuletea faida kubwa. Chukua hatua na mwisho wa siku utakuwa mshindi.

Wewe ni shujaa, pale unapoamua kuchukua hatua, licha ya kuwa n ahofu. Lakini unapokubali hofu zikutawale na kukuzuia kuchukua hatua, wewe ni mwoga.

Mashujaa ndio wanaofanikiwa kwenye maisha yao.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)