Je umewahi kutokuridhishwa na jinsi watu wanavyokuchukulia?

Labda unataka watu wakuone wewe ni mtu makini lakini hawakuoni hivyo? Au unataka watu waheshimu muda wako lakini hawauheshimu? Au unataka watu wakuheshimu na kukusikiliza lakini wanakudharau na kutokukusikiliza?

Unapokuwa kwenye hali kama hii ni rahisi kuona kwamba watu wanakuchukulia tofauti na unavyotaka wakuchukulie, labda wanakudharau. Lakini ukweli ni huu, watu wanafanya kile ambacho wewe mwenyewe umewaruhusu wafanye kwako.

Hii ina maana kwamba kama unaona watu wanakudharau, maana yake wewe mwenyewe umewaruhusu wakudharau. Kama watu hawaheshimu muda wako, ni wewe umewaruhusu kutokuheshimu muda wako. Watu hawawezi tu kuja kwenye maisha yako na kufanya kile wanachojisikia kufanya, bali wanakusoma vizuri na kufanya vile ambavyo unakubali wafanye.

Watu wanakuangalia kwa kila kitu unachofanya na jinsi unavyochukulia kile wanachokufanyia. Kama hujiheshimu na wao hawakuheshimu. Kama unachukulia muda wako hovyo hovyo nao wanauchukulia hivyo hivyo. Watu wanapojaribu kufanya jambo kwako, na wewe usiwakataze au kuwakanya, wanachukulia ni kitu cha kawaida kwako, na hivyo wanarudia tena.

Kama kuna namna ambavyo unapenda kuonekana kwa wengine, au unataka wengine wakuchukulie, basi anza kuishi vile unavyotaka uchukuliwe. Fanya kile ambacho unataka wengine wajifunze kuhusu wewe, na pale mtu anapofanya kinyume na unavyotaka kufanyiwa, mweleze ukweli kwamba hupendi alivyofanya.

Kwa namna hii watu watajifunza na kukuheshimu, watakapokuwa na wewe watafanya vile wewe unavyopenda wafanye.

SOMA; HEKIMA; Maana Yake, Faida Zake Na Mambo 11 Ya Kufanya Ili Uwe Na Hekima.

Mfano mzuri ni kwenye muda, ambapo watu wengi wamekuwa wakiumia sana. Kama umekuwa unaruhusu mtu kuja kwako muda wowote anaojisikia na kuanza kukuambia chochote anachojisikia, hivi ndivyo watu watakavyofanya. Lakini kama kuna muda maalumu ambao utawaambia watu muda huu nafanya kazi, na hata akija anajua una kazi muda huo, watajifunza kuheshimu muda wako, na watakuwa wanakuja kwa muda unaokuwa umewaambia.

Kila kitu kinaanza na wewe, watu wanakufanyia kile ambacho unajifanyia wewe mwenyewe. Anza kubadili maisha yako na wale wanaokuzunguka nao watabadilika.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)