UCHAMBUZI WA KITABU; BE YOUR OWN BRAND (Pata Kile Unachotaka Kwa Kuwa Vile Ulivyo Wewe)

Moja ya changamoto kubwa kwa zama hizi, ni watu kuiga kile ambacho wengine wanafanya. Yaani akitokea mtu mmoja akawa ameanzisha mtindo fulani mpya, na ukawa na mafanikio, basi kila mtu anaiga mtindo huo. Iwe ni vipindi vya tv au redio, uandishi na hata aina za biashara.
Wengi wa wanaoiga vitu kwa wengine, huwa hawafanikiwi kama wale walioanzisha, na sababu kuu ni moja, hakuna kitu kimoja kinachoweza kumfaa kila mtu, ila kila mtu ana kitu cha kipekee kwake, ambacho akikijua na kukifanya, atafanikiwa sana.
Ni sababu hii ilipelekea waandishi David McNally na Karl Speak kuandika kitabu BE YOUR OWN BRAND, yaani mtu uweze kujijenga wewe kama wewe, kutokana na utofauti ulionao na wengine.

Niseme tu kwa uwazi, hakuna wakati ambao tunahitaji kujitofautisha na wengine kama zama hizi. Hii ni kwa sababu chochote unachofanya sasa, iwe ni kazi au biashara wapo watu wengi wanaofanya kitu hicho. Sasa kama utakuwa unafanya kwa ukawaida, kama wengine, unajichimbia kaburi, kwani hakuna atakayekukumbuka. Ukiweza kujitofautisha, utaweza kujenga mafanikio makubwa kwa chochote ulichochagua kufanya, hata kama ni kuuza maji, au kufagia barabara.
Karibu tujifunze kwa pamoja namna tunavyoweza kutengeneza majina yetu na kuwa wa kitofauti na wa kipekee na hatimaye kufikia mafanikio makubwa sana.

1. Kila mtu ana BRAND (chapa/jina) na kila mtu anaweza kutengeneza jina lake hilo likawa la kipekee sana kwake. Ili kujijengea jina au chapa yako, huhitaji kubadili haiba yako, badala yake unahitaji kujua kile ambacho tayari kipo ndani yako na uweze kukitumia vizuri. Huhitaji kuwa kama mtu fulani uliyemwona amefanikiwa ili ufanikiwe, ila unahitaji kuwa wewe ili ufanikiwe. Tofauti ya wale wenye brand kubwa na wanaoshindwa kuwa brand kubwa ni kujitambua na kutumia uwezo mkubwa ambao mtu anao.

2. Kutengeneza jina lako kunaanza na kile unachokifanya kwa wengine. Hukuzi jina lako kwa kujitangaza, unakuza jina lako kwa jinsi unavyogusa maisha ya wengine, kwa namna unavyowafanya kuwa bora zaidi. Hivyo unapofikiria utakuzaje jina lako, anza kujiuliza ni watu gani ambao unaweza kuwasaidia kubadili na kuboresha maisha yao. Unahitaji kujenga mahusiano bora na watu ili waweze kulikuza jina lako. Mahusiano haya yanaanza na namna unavyowafanya wajisikie kupitia wewe. Kuna usemi kwamba watu watasahau kile ulichowaambia, watasahau kile ulichofanya lakini kamwe hawatasahau jinsi ulivyowafanya wakajisikia/walivyohisi. Ndiyo maana tunawakumbuka sana waliotukasirisha au kutufurahisha kuliko waliokuwa wanaongea tu.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha The Four Purposes of Life (Makusudi manne ya Maisha)

3. Hapo ulipo wewe tayari ni brand, tofauti ni kama brand yako ni kubwa au ndogo. Wewe ni brand kwa sababu kuna picha au taswira ambayo watu wanaipata wakisikia jina lako au wakikutana na wewe. Kwa mfano ni taswira gani inakujia kwenye akili yako unaposikia jina Makirita Amani? Basi hivyo pia kuna namna watu wanapata taswira wanaposikia jina lako, iwe ni kwenye familia, kazi na hata biashara. Hii ina maana kwamba nguvu ya brand zetu, inaanzia kwa wale wanaotuzunguka.

4. Inapokuja kuhusu brand yako, unachofikiri wewe hakina uzito kama kile wanachofikiri wengine kuhusu wewe. Habari mbaya au nzuri kuhusu wewe ndizo ambazo zinawapa watu taswira kuhusu wewe. Hivyo unahitaji kuwa makini kwenye kila unachofanya, ili kisije kuwa kinapingana na unavyotaka watu wakuchukulie.

5. Kutengeneza brand yako, haitoshi tu kwa wewe kuwa tofauti na wengine, bali unahitaji kuleta tofauti kwenye maisha ya wengine. Wewe unaweza kuamua kuwa tofauti, ila kama hakuna tofauti unayoweza kusababisha kwenye maisha ya wengine, hakuna anayeweza kukukumbuka. Mara zote fikiria ni tofauti gani unaweza kuleta kwenye maisha ya wengine.

6. Kwenye zama hizi tunazoishi za mitandao ya kijamii, ni muhimu sana uwe makini na brand yako. Tangu zama za kale kumekuwepo na umbeya duniani, lakini kwa zama za sasa, mitandao ya kijamii inamwaga petroli kwenye moto wa umbeya. Hii ina maana kwamba umbeya unasambaa kwa kasi sana zama hizi kuliko zamani. Hivyo unahitaji kuwa makini sana na kile unachofanya.

7. Brand yako inaweza kuathiriwa na wale watu unaohusishwa nao, watu wanakuhukumu kutokana na tabia za marafiki zako au wale unaokaa nao muda mrefu. Hivyo kama unaonekana na matapeli, moja kwa moja watu wanachukulia na wewe ni tapeli. Ni muhimu ujue ni brand gani unataka kujenga kisha jihusishe na wale watakaopelekea watu kuona brand yako sawasawa.

8. Kuna funguo kuu tatu za kuifanya brand yako kuwa kubwa na imara.
Moja ni UTOFAUTI, ni kitu gani cha tofauti unachofanya au unachosimamia. Huwezi kuwa brand kama unafanya kile ambacho kila mtu anafanya.
Mbili ni UHUSIANO, kile unachofanya, kinahusiana vipi na wale watu unaowalenga. Brand yako inatokana na namna wengine wanavyojisikia kwa kuwa na wewe au kufanya kazi na wewe.
Tatu ni MSIMAMO, ni kwa namba gani maneno na matendo yako yanaendana wakati wote. Kama unabadilika kila mara, huwezi kujenga brand ambayo watu wanaiamini.

SOMA; Huyu Ndiye Mwalimu Wa Kwanza Na Muhimu Sana Kwenye Malezi Ya Mtoto.

9. Brand yako inaanza kuwa imara pale unapochagua kitu unachoamini na kukisimamia. Ni lazima uchague kitu ambacho unakiamini kutoka ndani ya moyo wako, na upo tayari kukisimamia hata kama dunia nzima inakupinga. Unapochagua kitu unachoamini, ndiyo unajitenga na kundi na kutengeneza kitu cha tofauti ambacho watu wataweza kukihusisha na wewe. Namna unavyoweza kutetea na kufanyia kazi kile unachoamini, ndivyo watu wengi wanavyovutiwa na wewe, na wao wanakuamini na kuwa pamoja na wewe.

10. Watu watavutiwa kuwa na wewe kutokana na kile unachosimamia kwa kuamini na maadili uliyojiwekea. Brand ni mahusiano yako na wengine, kadiri watu wanavyokuamini, ndivyo brand yako inavyozidi kukua. Hivyo linda sana imani yako kwa wengine, usifanye kile kitakachowafanya watu waanze kuhoji uaminufu wako.

11. Ili kujenga mahusiano mazuri kati ya unachofanya na wale ambao unataka wakipate, usijifikirie wewe kwanza, bali anza kuwafikiria hao wengine. Kuna usemi wa Zig Zigler kwamba unaweza kupata chochote unachotaka kupata, kama utawawezesha wengine kupata kile wanachotaka. Hivyo kama unataka kuwa tajiri, wawezeshe wengine kuwa matajiri kupitia kile ambacho wanakitaka wao, na wewe unaweza kuwapatia.

12. Katika kujenga imani yako na wale wanaokuzunguka, hakikisha kila unachofanya, kinaendana na ile picha unayotaka kujenga. Kama unataka kujenga picha kwa wengine kwamba wewe ni makini, basi mara zote kuwa makini, kwenye mambo makubwa na madogo. Kama unataka kujenga picha kwamba wewe ni mwaminifu, basi kuwa mwaminifu kwenye mambo yako yote. Maneno yako yanapoanza kupishana na matendo yako, unapoteza kabisa imani ya watu kwako, na unaharibu brand yako.

13. Watu wanaikubali brand na kushirikiana nayo kupitia maeneo haya matatu muhimu, yajue na yatumie kujenga brand yako.
Moja; UMAHIRI, je ni kipi ambacho watu wanakipata kutoka kwenye brand husika. Hapa unachagua maeneo ambayo unayafanyia kazi. Hapa unajikabidhi majukumu ambayo watu wakija kwako wewe utayatatua.
Mbili; VIWANGO, je unafanya kile ulichochagua kwa viwango gani? Hapa unapima ubora wa jinsi unavyofanya mambo yako, na viwango ndiyo vinakutofautisha wewe na wengine?
Tatu; MTINDO, je unafanya kile unachofanya kwa namna gani ya tofauti? Hapa ni namna unavyowasiliana na kushirikiana na wengine.

14. Kabla hujaanza kutengeneza brand yako, ni lazima uhakikishe kwamba unaweza kumwonesha mtu unayetaka kujenga naye mahusiano kwamba unaweza kumtatulia matatizo yake au kutimiza shida zake. Huu ndiyo msingi mkuu, kwa sababu kama huwezi kutatua tatizo au kutimiza kile unachofanyia kazi, hata ungekuwa tofauti na ukawa na mbinu nyingi kiasi gani, hazitasaidia. Kwa kifupi chagua eneo ambalo unataka kujulikana kupitia hilo, inaweza kuwa michezo, uandishi, kazi au biashara.

15. Jijengee miiko na maadili ili uweze kufanya kile unachotakiwa kufanya bila ya kuharibu brand yako, hata kama unapitia hali gani. Ni rahisi sana kujisahau hasa pale mtu anapoanza kupata sifa kwa kufanya kitu kizuri, wengi huanza kuharibu na baadaye sifa zao kuharibika. Ili lisikukute hili, jiwekee maadili na miiko. Maadili ni namna unavyofanya mambo yako. Miiko ni yale mambo ambayo ni lazima uyafanye au kamwe hutoyafanya hata kitokee nini. Ili kujenga brand unahitaji kuwafanya watu wajue wakija kwako lazima wapate kitu fulani, na pia wajue kwa namna yoyote ile wewe huwezi kufanya vitu fulani, ambavyo haviendani na wewe.

SOMA; Siri Kubwa Ya Kukutoa Kwenye Umaskini.

16. Msingi mkuu wa brand yako ni kujua uhalisia wako. Watu wengi wamekuwa wakikazana kuwa kama wengine na kujikuta wanaharibu zaidi. Unahitaji kujua uhalisia wako, jua ni maeneo gani uko vizuri na maeneo gani ambayo una madhaifu. Usihangaike na madhaifu, badala yake tumia yale ambayo uko imara. Uhalisia ndiyo mgongo wa brand. Unapoiga wengine unafika wakati unachoka, lakini unapofanya kile kinachoendana na uhalisia wako, huwezi kuchoka, maana hayo ndiyo maisha yako.

17. Linapokuja swala la mafanikio, unahitaji kutumia maadili na miiko yako kufanikiwa. Watu wengi wamekuwa wakipindisha maadili na miiko yao ili tu kufanikiwa, na jamii zimekuwa zikiaminishwa hivyo. Kuna watu wamekuwa wakisema kabisa kwamba huwezi kuwa tajiri kama siyo mwizi au fisadi. Lakini ukweli ni kwamba brand inayodumu ni ile inayosimamia maadili na miiko yake. Hivyo unaweza kuchagua kupindisha maadili na miiko yako ili ufanikiwe haraka lakini mafanikio hayo yasidumu, au usimamie maadili na miiko yako, uchelewe kufanikiwa lakini ufanikiwe milele.

18. Ili kujua uhalisia wako ambao utakuwezesha kujenga brand yako hatua hizi tatu muhimu unapaswa kuzipiga;
Moja; jua kusudi la wewe kuwa hapa duniani(PURPOSE). Upo hapa duniani kufanya nini? Ulikuja duniani kutoa mchango gani? Kila mtu anapaswa kujua hili, na unalijua wewe mwenyewe, hakuna wa kukufundisha.
Mbili; tengeneza maono yako(VISION). Je ni ndoto zipi ambazo unazo kwenye maisha yako? ni kitu gani cha tofauti unataka kufanya hapa duniani? Maono yako ndiyo yatawavutia watu kuandamana na wewe.
Tatu; Maadili yako (VALUES), ni kipi ambacho unasimamia kama ukweli? Ni mambo gani muhimu zaidi kwako? Ni vitu gani upo radhi kufanya au kutokufanya katika safari yako ya mafanikio? Maadili yako ndiyo yanawafanya watu wakuamini.

19. Bila ya kujali unapitia nini, bila ya kujali uko wapi, simamia kile unachoamini. Kuna wakati ambapo brand yako itajaribiwa, kila mtu anapitia majaribu fulani kwenye maisha yako. unafika wakati ambapo mambo yanakuwa magumu kiasi kwamba uko tayari kusaliti kile ulichokuwa unasimamia mwanzo, ukisaliti unaharibu kabisa brand yako, lakini unapoendelea kusimamia kile unachoamini hata kama unapitia magumu, unajenga brand imara. Nafikiri umekuwa unaona jinsi wanasiasa wanavyopoteza kuaminiwa na kuitwa wasaliti pale wanapotoka chama kimoja na kwenda kingine. Simamia kile unachoamini, wakati wote.

20. Kujenga BRAND (JINA/CHAPA) YAKO ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Ni kazi ambayo unahitaji kuifanya kila siku na kila wakati. Kwenye kila kitu unachosema au kufanya, dunia inakuangalia. Na dunia hii ya mitandao ya kijamii, pamoja na simu zenye uwezo wa kurekodi picha na sauti, linda sana BRAND yako, maana hapo ndipo mafanikio yako yalipo. Kila siku na kila nafasi unayoipata kukutana na mteja au mtu yeyote, ni nafasi nzuri kuitangaza na kuikuza brand yako. hakikisha mtu yeyote anayekutana na wewe, haondoki kama alivyokuja, tafuta namna ya kuongeza thamani kwenye maisha yake, hata kama ni kumfanya atabasamu.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako. tumia haya uliyojifunza kujenga brand yako, na kuweza kuishi maisha ya mafanikio. Katika ulimwengu huu wa sasa, ambapo mtandao una nguvu kubwa, moja ya njia za kutumia kujenga brand yako ni mtandao wa intanet na mitandao ya kijamii. Unahitaji kuitumia vizuri kutangaza jina lako. Kama hujaanza kutumia mitandao hii, na ungependa kuweza kuitumia vizuri kukuza jina lako, biashara yako na hata kutengeneza kipato, wasiliana nami kwa namba 0717396253. Karibu sana.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s