Hakuna kitu chenye nguvu kwenye maisha yetu kama maneno, maneno yanaumba.
Hata mtu ajaribu kiasi gani kubadilika, kama hatabadili maneno yake, basi ataendelea kubaki pale alipo. Kwa sababu maneno yake yanampa nguvu ya kuendelea kuwa pale ambapo yupo.
Kumekuwa na maneno ya kujifariji ambayo masikini wamekuwa wakijiambia, na maneno haya yanawafanya wazidi kuwa masikini. Maneno haya yanatokana na jamii ambazo watu wamekulia, na mapokeo mabaya ya imani za kidini.
Kwa mfano kuna sentensi moja maarufu sana ambayo masikini wamekuwa wakijiambia;
“Kila tajiri ni mwovu, matajiri wote wamepata fedha zao kwa njia za uovu, rushwa au kudhulumu wengine. Mimi siyo mwovu ndiyo maana sijatajirika.” Nafikiri umeshasikia sentensi hiyo au maneno mengine yanayofanana na hayo.
Bado kuna yale maneno kwamba ni vigumu tajiri kuingia kwenye ufalme wa mbinguni.
Rafiki yangu, kama unataka kuwa tajiri, kama unataka kupata uhuru wa kifedha, kwanza kabisa acha kuwasema vibaya matajiri. Acha kuwaona ni watu waovu na acha kufikiri utajiri ni kitu kibaya. Badala yake wapende matajiri, upende utajiri, washukuru matajiri kwa sababu wanatoa ajira na kutoa huduma na bidhaa kupitia biashara wanazofanya.
Ukishawapenda na kupenda kujua zaidi kuhusu wao, ndipo utakapojifunza siri ambazo zimewafikisha pale. Kwa sababu kuna kitu wanafanya tofauti na wewe na ndiyo maana wametofautiana na wewe. Jifunze na fanyia kazi ili na wewe utajirike.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Naked Millionaire (Muongozo Wa Uhakika Wa Kuelekea Kwenye Utajiri, Uhuru Na Utimilivu).
Ukiwachukia matajiri, ukiuchukia utajiri na kuona wewe upo sahihi sana kuwa masikini, utaendelea kuwa masikini kwa maisha yako yote. Kwa sababu maneno yako yanaumba.
“Hakuna ubaya wowote kuwa tajiri, wala hakuna uzuri wowote kuwa masikini. Weka juhudi kuboresha maisha yako, fanya hivyo kwa kuwasaidia wengine kuboresha maisha yako, na utapata utajiri wa kukutosha.” Makirita Amani.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)