Habari za leo rafiki yangu?
Karibu tena kwenye mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ambapo tunashirikishana maarifa muhimu ya kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi kila siku. Kila siku ni siku nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi ili kuhakikisha maisha yetu yanakuwa bora. Swali la msingi sana ambalo tunapaswa kujiuliza ni je, juhudi hizi tunaziweka wapi? Kwa sababu kama unaweka juhudi kwenye yale yale ambayo umekuwa unayafanya, utazidi kupata matokeo yale yale. Yaani kama ulikuwa unachimba shimo, unapozidi kuweka juhudi ndiyo unazidi kuingia kwenye shimo refu.

Leo napenda kuongea na waajiriwa wote, na waajiriwa watarajiwa, juu ya changamoto za ajira na jinsi mtu anavyoweza kununua uhuru wake kutoka kwenye ajira. Waajiriwa namaanisha wale wote ambao wanauza muda wao na utaalamu wao kwa watu wengine, yaani unampa mtu muda wako na utaalamu wako na yeye ndiye anayeamua akulipe kiasi gani. Waajiriwa watarajiwa namaanisha wahitimu wa ngazi mbalimbali ambao kwa sasa wanatafuta kazi. Na huu ndiyo msimu wa kuhitimu hivyo maombi ya kazi na ushauri kuhusu kazi yamekuwa mengi.

Tuanze kwa kuusema ukweli kama ulivyo, japo ukweli huwa unaumiza, lakini hata kuukwepa bado hakuubadilishi kuwa ukweli.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Kosa kubwa kabisa ambalo mtu anaweza kufanya kwenye maisha yake dunia nzima, ni kuchagua kuwa mwajiriwa pekee kwa miaka yake yote. Na kosa kubwa kabisa mtu anaweza kulifanya hapa Tanzania ni kuchagua kuwa mwajiriwa wa umma pekee maisha yake yote. Ninaposema pekee namaanisha mtu anategemea ajira tu kuendesha maisha yake, hana chanzo kingine cha kipato zaidi ya ajira aliyonayo.

SOMA; Je Ungependakutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kuanzia hapo ulipo sasa? Bonyeza hapa kujua zaidi.

Kwa nini ni kosa kubwa sana kutegemea ajira pekee kwa ajili ya kipato?

Kwa sababu kunakutengenezea utegemezi wa kipato. Kipato kimoja hakiwezi kutosheleza mahitaji yote ya maisha, na hivyo mtu kuwa tegemezi, badala ya kuwa na uhuru wa kifedha. Kwa kutegemea chanzo kimoja pekee, mtu anaishi kwa hofu kwa sababu iwapo chanzo hiko kimoja kitapotea, basi maisha yake yapo kwenye hatari kubwa.

Na jambo jingine muhimu sana ni kwamba, chanzo kimoja cha kipato, hakiwezi kukufanya kuwa tajiri, na ni nani ambaye hapendi kuwa tajiri? Kuna watu watajisikia vibaya kwa sababu nimetaja neno tajiri hapo, kama vile ni mwiko. Sawa tuachane na hilo la utajiri, muhimu ni kwamba unahitaji kuwa na uhuru wa kifedha, unahitaji kuamka asubuhi ukiwa na hamasa ya kwenda kuweka juhudi kubwa na kutoa huduma bora, na siyo kuamka ukiwaza leo nikamkope nani, au leo nitoe kisingizio gani kwa wanaonidai. Hiki ni kitu ambacho huwezi kukipata kwenye ajira.

Kwa ni kosa kubwa kwenye maisha ya Mtanzania ambaye amechagua kuwa mtumishi wa umma kwa maisha yake yote?

Kwa sababu ambazo zipo wazi, kwanza kabisa, siku za nyuma ilikuwa ni uhakika wa ajira, watu walikimbilia kupata ajira serikalini ambapo walikuwa na uhakika wa kuwa na ajira hizo mpaka pale watakapostaafu. Hata kama kipato ni kidogo, lakini wengi walikimbilia ajira hizi kwa sababu walikuwa wanaona wanakuwa na muda wa kufanya mambo yao. Lakini ulikuwa ukiwachunguza hawa watu wanaokuambia wana muda wa kufanya mambo yao, hakuna makubwa waliyokuwa wanayafanya.

Pili siku za hivi karibuni, ajira za umma umekuwa mwiba mkali, imekuwa ni sehemu ya kufanya kazi kwa nidhamu ya woga, utaalamu umekuwa hautumiki tena badala yake watu wamekuwa wakiangalia lipi ambalo litawafurahisha viongozi na kulifanya hilo. Hii imewafanya waajiriwa wengi kufanya kazi wakiwa na hofu kubwa. Unajaribu kumhoji tu mtu kwa nini anakuhudumia vile anavyokuhudumia anakujibu nalinda kibarua changu, na hapo anakuwa anafanya kitu ambacho hukutegemea afanye hivyo. Hapo hatujaangalia wale ambao ‘wanatumbuliwa’ bila ya kupewa nafasi ya kusikilizwa au kuonywa.
Sasa tumeyajadili haya siyo kukupa wewe nafasi ya kujifariji, au kulalamikia haya yanayoendelea, ila tuangalie namna unavyoweza kuchukua hatua. Unanijua mimi vizuri, sitaki upoteze muda wako kulalamika na kulaumu kama wengi wanavyofanya, ninachotaka ufanye ni kuchukua hatua, kwa sababu maisha yako ni jukumu lako wewe mwenyewe, kama kuna kitu hukipendi ni wajibu wako kukibadili, na kama huwezi kukibadili basi achana nacho.

Ni hatua gani unaweza kuchukua kuondokana na changamoto hizi za utegemezi wa ajira?
Watu wengi wamekuwa wanahubiri kwamba acha kazi nenda kawe mjasiriamali. Kama vile ujasiriamali ni kitu cha kwenda kuanza na kufanikiwa hapo hapo, UJASIRIAMALI NI MTINDO WA MAISHA, nitakuja kuandika kwa kina juu ya hilo. Lakini nataka nikuambie kwamba hutumii ujasiriamali kama mbinu ya kutoka kimaisha, bali unachukua ujasiriamali kama mtindo wa maisha umechagua kuishi. Hivyo unaweza kuanza kuuishi popote ulipo, iwe umeajiriwa au huna ajira.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Nina mapendekezo mawili;

Pendekezo la kwanza, kama wewe ni kijana, ambaye umehitimu masomo yako na unatafuta ajira kwa zaidi ya miaka miwili ila hujapata, achana kabisa na hilo swala la kutafuta ajira. Kama miaka miwili umekuwa unazunguka na bahasha hujapata ajira, ni wakati sasa wa kuangalia upande wa pili. Weka bahasha na vyeti kabatini na anza mapambano yako mwenyewe, jipe miaka mingine miwili ya kwako tu, kufanya kila unachoweza kufanya mpaka kuhakikisha umesimama. Nina uhakika, kwa miaka miwili, kama umechagua kufanya kitu, utafika mbali sana, kuliko kuendelea kusubiri ajira ambazo zinazidi kuwa changamoto kila siku.

Pendekezo la pili, kama wewe ni mwajiriwa, ambaye umekuwa kwenye ajira kwa muda mrefu na maisha yako yote yanategemea ajira, sikuambii uache kazi na kwenda kupambana, ila nakuambia anza mapambano ukiwa hapo hapo kwenye ajira. Ila ninataka nikuambie ukweli zaidi, ambao hutaki kuusikia, chagua kuteseka zaidi ya unavyoteseka sasa, hakuna uhuru unaoletwa kirahisi, uhuru unapiganiwa. Hii ina maana kwa mfano, uanzishe biashara wakati bado upo kwenye ajira yako ya sasa, kwa hiyo uende kazini, ukitoka, badala ya kwenda kupumzika, uingie kwenye biashara yako. Na mwisho wa wiki, ambapo huendi kazini, badala ya kupumzika, uende kwenye biashara yako.
Hii inaweza kupelekea kufanya kazi zaidi ya masaa 12 kwa siku, kupunguza muda wa kupumzika na wa kulala, na kuachana na marafiki ambao umezoeana nao, hiyo ndiyo gharama ya uhuru wa kifedha, lazima uwe tayari kuilipa kama kweli unataka kupata uhuru.

SOMA; KITABU CHA MAY; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Mwisho kabisa nimalizie kwa kusema, tengeneza vyanzo tofauti vya kipato, usitegemee kipato kimoja pekee, iwe ni kwenye kazi au biashara. Kadiri unavyokuwa na vyanzo vingi, ndivyo unavyokuwa huru kifedha, kwa sababu chanzo kimoja kikiwa na changamoto, vyanzo vingine vinaendelea kutiririsha kipato.

Nakutakia kila la kheri katika kununua uhuru wa maisha yako kupitia uhuru wa kipato.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)