Kwa kumwangalia tu mtu, unaweza kujua ni kitu gani kimemfikisha pale alipo sasa, ni maamuzi gani alifanya au hakufanya yamepelekea kuwa pale alipo sasa.

Kwa mfano unapomwangalia mtu ambaye yupo kwenye ajira miaka mingi na malalamiko yake ni kipato kutokutosheleza, huku akiwa na madeni mengi, iko wazi kwamba mtu huyu alichagua ajira kuwa msingi wa maisha yake. Alishindwa kufanya maamuzi ya kujiongeza na hivyo kubaki pale pale alipo.

Unapomwangalia mtu ambaye ni mlevi, unajua kabisa kwamba alichagua njia rahisi ya kutatua changamoto zake kwenye maisha, au kujipa starehe, akaanza kutegemea njia hiyo na sasa hawezi tena kuondoka kwenye njia hiyo.

Iko wazi kwamba pale tulipo sasa, na kile tunachofanya sasa ni matokeo ya maamuzi ambayo tulifanya au tulishindwa kufanya siku zilizopita. Lakini hili siyo muhimu sana kwa sasa, tukishajua hivi inatusaidia nini?

Muhimu zaidi ni kujua kwamba leo hii, sasa hivi tunaweza kufanya maamuzi au kuacha kufanya maamuzi fulani na yakaathiri sana maisha yetu ya baadaye.

Kama leo utafanya maamuzi ya kubadilika, ya kufanya kazi zako kwa utofauti, ya kuweka juhudi kubwa zaidi, ya kuanzisha biashara yako ya pembeni kama umeajiriwa, na ukakomaa na maamuzi hayo, siku zijazo utaangalia nyuma na kushukuru sana. Pia kama leo utaacha kufanya maamuzi haya, miaka ijayo utaona maisha yapo kama yalivyokuwa, na mbaya zaidi yanazidi kuwa magumu.

MUHIMU; Je ungependa kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kuanzia hapo ulipo? Bonyeza maandishi haya.

Kila siku yako, jiulize ni maamuzi gani nikiyafanya leo, maisha yangu yatakuwa bora sana siku zijazo. Ni maamuzi madogo madogo tunayofanya kila siku ndiyo yanajikusanya na kuwa maisha yetu, hakuna siku moja maisha yanabadilika ghafla, bali maamuzi madogo madogo ya kila siku ndiyo yanajenga maisha yetu.

Usikwepe kufanya maamuzi kwenye maisha yako, kwa sababu usipofanya maamuzi juu ya maisha yako, wengine watakufanyia maamuzi, na siyo maamuzi bora kwako bali kwao.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)