Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu tena kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA, ambapo tunakwenda kushirikishana misingi muhimu ya kuendeshe maisha yetu, ili tuweze kupata kile tunachotaka na kuwa na maisha bora na yenye furaha.
Kabla hatujaingia kwenye makala ya leo ya falsafa, naomba nikukumbushe mambo mawili muhimu sana ya kuchukua hatua mara moja;
- Nitaendesha semina ya bure kwa wiki moja kuhusu KUTENGENEZA FEDHA KWA KUTUMIA BLOG, semina itaanza tarehe 19/09/2016, nafasi ni chache za kushiriki hivyo chukua hatua sasa. Bonyeza hapa kujiunga na semina hii.
- Tutakuwa na semina ya TENGENEZA MILIONI YA ZIADA, semina hii ni ya kuhudhuria siyo kwa njia ya mtandao. Semina hii ina mengi sana ya kujifunza na hatua za kuchukua ili uweze kutengeneza milioni ya ziada kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Kupata nafasi ya kushiriki semina hii bonyeza maandishi haya.
Baada ya hayo mawili muhimu sana, na ninakusihi usikose hata moja, karibu kwenye falsafa yetu ya leo.
Leo tunakwenda kujadili kwa kina kuhusu SARAFU ya maisha yetu, na namna tunavyoweza kuitumia kuyafanya maisha yetu kuwa bora ziadi.
Kabla hatujaingia kwa kina kujadili sarafu ya maisha, kwanza tuangalie sarafu ni nini?
Ukiwa Tanzania sarafu ni SHILINGI YA KITANZANIA,
Ukiwa Marekani sarafu ni DOLA,
Ukiwa Japan sarafu ni YEN,
Ukiwa Uingereza sarafu ni PAUNDI.
Swali ni je sarafu ya maisha yetu kwa pamoja ni nini?
Sarafu ni kipimo cha thamani, tunatumia sarafu kujua kitu kina thamani gani na hivyo unapohitaji kukipata kitu hicho, ni lazima ulipe gharama yake kulingana na sarafu.
Sarafu ya maisha yetu ni nini? Je tunapimaje thamani ya maisha yetu? Hapa ndipo tunapohitaji kujua vizuri ili kuweza kuongeza thamani ya maisha yetu.
Tuchukue mfano wa mtu aliyefariki, kila mmoja wetu amewahi kuhudhuria mazishi ya mtu ambaye alikuwa wa karibu kwetu kwa namna fulani. Je katika yale mazishi ni kwa jinsi gani watu wanapima maisha ya marehemu?
Tukianza na yale maneno ya watu, utasikia yakitajwa mambo aliyofanya, alikuwa mwema, alikuwa mcheshi, alikuwa anawasaidia wengine. Kila mtu atazungumzia namna anavyokumbuka maisha ya marehemu yalivyomwathiri yeye kwa njia chanya au hasi.
Ukija kwenye historia ya marehemu, ambayo imeandaliwa vizuri na inasomwa, utasikia namna ambavyo aliendesha maisha yake, kazi alizofanya, hutasikia watu wakisema vitu alivyomiliki. Hutasikia kwenye historia ya marehemu wakisema marehemu alikuwa na magari matano, nyumba tatu na mashamba mawili, hayo hayawasukumi watu bali namna alivyoishi maisha yake.
Hivyo basi kwa mfano huo halisi tunaanza kuona ni ipi sarafu ya maisha yetu, ni kwa namna gani thamani ya maisha yetu inapimwa.
Sarafu ya maisha yetu ni MUDA. Muda pekee ndiyo kitu ambacho thamani ya maisha yetu inapimwa. Ni kwa jinsi gani umekuwa unatumia muda wako hapa duniani, ndiyo kipimo cha thamani ya maisha yetu.
Kila kitu kwenye maisha yetu kinahusisha muda, kazi, biashara, mahusiano, yote yanahitaji muda ili kuweza kuwa bora.
Muda ndiyo kitu pekee chenye thamani kubwa kuliko hata fedha, poteza fedha unaweza kuzipata, lakini poteza muda huwezi kuupata tena.
Kuyapima maisha kwa muda.
Ukiyaangalia maisha yako leo, ni kiashiria tosha namna gani umekuwa unatumia muda wako. Kama umekuwa mwajiriwa kwenye maisha yako yote, ipo wazi kwamba matumizi ya muda wako ulichagua kumuuzia mtu mwingine, na yeye aamue anakulipa kiasi gani kwa muda huo.
Kama umeweza kuendesha biashara yako mwenyewe, maana yake umeamua kutumia muda wako kufanya kitu kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine, na hivyo kupata faida kupitia muda wako.
Kama mtu atashindwa kutumia muda wake vizuri, na kujihusisha na mambo ambayo hayana manufaa kwake, kila siku ataendelea kuwa na maisha mabovu. Wote wanaofanikiwa ni wale wanaotumia muda wao vizuri, na kwenda hatua ya ziada.
Changamoto kubwa ya muda.
Changamoto kubwa ya muda ni kwamba muda ni ule ule, hauongezeki. Tuna masaa yale yale 24 kwenye siku zetu, hayajawahi kuongezeka na hakuna dalili kwamba yatakuja kuongezeka. Changamoto kubwa zaidi ni kwamba kila siku mambo ya kufanya yanazidi kuongezeka. Kwa muda huu huu tulionao, tunakuwa na vitu vingi ambavyo vinatutaka tufanye. Na hapa ndipo wengi wanapopotea na kushindwa kujitengenezea maisha bora.
Hatua za kuchukua ili kuongeza thamani ya maisha yako kupitia muda.
- Weka vipaumbele vya maisha yako, usikipe kila kitu uzito sawa kwenye maisha yako. Chagua ni mambo yapi muhimu kwako, ambayo kwa kuyatekeleza utaongeza thamani kubwa kwenye maisha yako kisha weka muda wa kutosha kwenye kufanya mambo hayo.
- Linda sana muda wako, usiuache upotee hovyo, unapopoteza muda maana yake umechagua kupoteza maisha. Linda sana muda wako, kuna watu wengi wanaokuzunguka ambao watajaribu kuiba muda wako, kuwa mkali na fuatilia vipaumbele vyako.
- Ipangilie siku yako kabla hujaianza. Hakuna kosa kubwa unaloweza kufanya kwenye maisha yako kama kuianza siku yako bila kuipangilia. Utajikuta unafanya mambo ambayo siyo muhimu kwako, siku imeisha, umechoka lakini huoni matokeo mazuri uliyopata. Kuwa na ratiba yako ya siku nzima na ifuate.
- Wekeza muda kwenye kujenga mahusiano bora na wengine. Marafiki, ndugu na familia ni watu muhimu sana kwako, watu hawa unaweza kujenga nao mahusiano mazuri kupitia muda pekee, na siyo fedha kama wengi wanavyodhani. Tumekuwa tunafikiri njia rahisi ya kutatua matatizo yetu na wengine ni kutumia fedha, lakini kama unataka kujenga mahusiano bora, wekeza muda. Tenga muda na familia yako, tenga muda na marafiki zako na watu wengine wa karibu kwako.
- Wafundishe wengine thamani ya muda wako. Ni rahisi wewe kupangilia muda wako lakini wengine wakaja na kuharibu mipango yako. Ulipanga ufanye kitu fulani anakuja mtu na mahitaji yake unajikuta ukipoteza muda mwingi kumsikiliza au kumsaidia kile anachotaka. Usipo wafundisha na kuwaelewesha watu kuhusu umuhimu na thamani ya muda wako, wao watachukulia kawaida tu. Hivyo ni jukumu lako kuwaeleza watu wazi kwamba ni muda gani hawawezi kukupata kwa urahisi, iwe ni kwa maongezi ya ana kwa ana au kwa njia ya simu. Mwanzoni hawatakuelewa, lakini kadiri siku zinakwenda watakuelewa na kuheshimu maamuzi yako.
Muda ndiyo kipimo pekee cha maisha yetu, tupo hapa tulipo sasa kutokana na matumizi ya muda wetu, na tutafika kule tunakokwenda kulingana na tunavyotumia muda wetu. Tuheshimu na kulinda muda wetu, tuweke vipaumbele na kuvifanyia kazi.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Asante kocha Kwa sarafu hii ya maisha.
LikeLike
Karibu
LikeLike