Habari rafiki?
Karibu kwenye kipengele chetu cha leo cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa.
Je wewe ni mwalimu? Je umekuwa unatafuta kazi bila ya mafanikio yoyote? Leo nataka nikushirikishe mambo matano unayoweza kuanza kuyafanya mara moja na ukaondoka kwenye hali ya kutokuwa na ajira uliyopo sasa.

Nimekushirikisha ushauri huu ambao niliutoa kwenye kundi letu la telegram la AMKA MTANZANIA, ambapo mwenzetu aliomba ushauri wa ajira. Nimeona ushauri huu unaweza kuwasaidia wengi zaidi hivyo usome na fanyia kazi yale unayojifunza. Kama utapenda kujiunga kwenye kundi hili hakikisha una TELEGRAM kwenye simu yako (inapatikana playstore kama wasap) kisha bonyeza maandishi haya na moja kwa moja utaingia kwenye kundi la AMKAMTANZANIA TELEGRAM.
Karibu tujifunze kupitia ushauri wa leo;

Natafuta kazi, Habari wapendwa,
Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 30, naishi Dar es salaam, Nina elimu ya postgraduates diploma in education, nafundisha history na kiswahili, nina uzoefu wa kufundisha kwa mwaka 1, degree yangu ya kwanza nilisomea mambo ya human resources, nina uzoefu wa kazi ya human resources kwa miezi 6. Nilifanikiwa kuanzisha biashara lakini haikuenda vizuri kutokana na kutokuwa na usimamizi wa kutosha, hivyo naomba yoyote anisaidie kupata kazi yoyote au inayoendana na nilivyosomea ili niweze kusimama tena, na kutafuta mtaji.

NDUGU,

Kwanza nikupe pole sana kwa changamoto unayopitia. Naelewa jinsi ambavyo huenda umetafuta kazi kwa muda bila ya matumaini. Pia muda uliowekeza kwenye elimu ni mwingi na hivyo unahitaji kutumia elimu hiyo vizuri.

Sasa mimi sitaki nikuchoshe na mengi hapa, nataka uniambie kama kweli una njaa na hasira ya kutoka hapo ulipo sasa, kwa kufanya lolote ambalo utahitajika kufanya.
Na kama ni ndiyo basi hapa nakushauri mambo matano (5) ya kuanza kufanya kesho….

1. Andika barua ya kuomba nafasi ya kufundisha kwa kujitolea bila ya kulipwa chochote, na chagua shule kumi zilizopo kwenye eneo linalokuzunguka, shule za sekondari au za primary kwa english medium. Katika shule kumi, hutakosa hata mbili ambazo watakuita kuongea na wewe, waombe wakupe nafasi ya kujitolea kufundisha, wakikupa nafasi hiyo, fanya kazi iliyo bora mno, wafundishe watoto vizuri mno, kiasi kwamba thamani yako iongezeke, fursa zaidi zitakuja.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wahitimu Wa Elimu Ya Juu Mwaka 2016, Ukweli Ambao Umekuwa Unafichwa Kwa Miaka 20 Iliyopita.

2. Kwenye eneo unalokaa, ongea na wazazi wote ambao watoto wao wanasoma sekondari au hata primary, kisha waombe uwafundishe kwa muda wa ziada, jioni au mwisho wa wiki. Tafuta eneo unaloweza kufanyia zoezi hilo, waombe uanze kufundisha hata bure kwanza, halafu wakiona mabadiliko kwa watoto wao, ndiyo uanze kuwachaji kidogo.

3. Kwenye eneo unalokaa, kama kuja watu wenye uwezo kiasi ambao wana watoto wanaosoma, unaweza kuongea nao na ukawa unawafundisha watoto wao majumbani kwao. Popote unapopata nafasi fanya kazi bora sana.

4. Anzisha blog, ambayo inawafundisha wageni kiswahili fasaha, wewe ni mwalimu wa kiswahili, hivyo tengeneza mfumo ambao unaweza kumsaidia mtu asiyejua kiswahili akajifunza vizuri, mwanzo hutakuwa na wasomaji wengi, ila wewe target wale ambao ni wageni, na wapo wengi mno, kuna wachina wana njaa ya kukijua kiswahili.
Nyongeza, hapo kwenye blog toa huduma ya translation, labda kingereza kuja kiswahili, au kama unaweza kiswahili kwenda kiingereza. Kuna wengi wanahitaji huduma hiyo.

SOMA; Shiriki Semina Ya Bure Ya Jinsi Ya Kutengeneza Fedha Kwa Kutumia Blog.

5. Kaa chini na wazo lolote la biashara ambalo unalo kwa sasa, ambalo upo tayari kutoa kila tone la jasho lako kufanyia kazi, yaani iwe passion yako kweli. Liandike wazo hilo vizuri, angalia ni sehemu ipi ya chini kabisa unayoweza kuanzia, kiasi kidogo kabisa unachoweza kuanza nacho. Kisha waangalie watu wote wanaokuzunguka, ambao una mahusiano nao ya kindugu au kirafiki. Wachague wale ambao unajua watakuelewa, kisha zungumza nao kwa namna wanavyoweza kukusaidia kwa wazo hilo ulilonalo.

Anza na hayo, unaweza kuchagua mawili au matatu au yote na uone lipi litawezekana kwako, ila blog anza nayo hata kesho, miaka mingi ijayo utajishukuru sana.
Kama kwa namna yoyote ile wakati unasoma huo mtiririko napo ulikuwa unajiambia mimi siwezi hili au siwezi hili, niseme tu hutaweza kutoka hapo ulipo.
Nimalize kwa kukuambia kwamba kama umechagua kitu cha kufanya hapo, na ukishajipanga kufanya, nitafute, nitakucoach bure kabisa, ukishakuwa na mpango tayari.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.