Niliwahi kuandika kwenye makala za nyuma kwamba, haijalishi unajua nini, bali anakujua nani. Unaweza kuwa unajua sana, unaweza kuwa bora sana kwenye kile unachofanya, lakini kama watu sahihi hawajui kama unajua, hutaweza kufanya makubwa.

Lakini wengi wanaposikia hili wanasikitika, kwamba sasa wao wametokea familia masikini, hawana ndugu wenye uwezo wanaowajua na hivyo hawawezi kupata fursa nzuri. Hapa ndipo wengi wanapokosea na kushindwa kuchukua hatua ya kuboresha maisha yao.

Leo nakupa kanuni rahisi sana ya mafanikio ambayo wengi hawaitumii, au huenda hawaijui. Kanuni hii kwa kiingereza inasema;

YOUR NETWORTH = YOUR NETWORK

Yaani;

UTAJIRI WAKO = NA MTANDAO WAKO.

Hii ina maana kwamba ukiwa na mtandao mkubwa ndivyo unavyokuwa tajiri mkubwa. Hivyo kazi sasa ni unakuzaje mtandao wako.

Usifikiri kwamba utakuza mtandao kwa kupendelewa na ndugu au watu wa kabila lako ambao wamepata fursa nzuri, inawezekana hivyo ila siyo njia bora na ya uhakika.

Njia bora na ya uhakika ya kukuza mtandao wako ni wewe mwenyewe kuweka juhudi kubwa. Anza kwa kufanya kile unachokifanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kila unapopata nafasi ya kukutana na mtu, toa thamani kubwa, kupitia maneno na vitendo vyako.

Hakuna wakati rahisi kukuza jina lako na mtandao wako kama wakati huu wa mitandao ya kijamii. Itumie mitandao hii vizuri kukuza jina lako na itumie kuwafikia watu wengi zaidi.

Unapokuza mtandao wako hukuzi kwa kumfikia kila mtu, bali unaukuza kwa kuwafikia watu sahihi kuendana na kile unachofanya na jina unalotaka kujenga.

Dunia ya sasa, mtu akiwa na shida, hatua ya kwanza ni kuingia kwenye mtandao na kutafuta suluhisho la shida yake. Hivyo kama wewe ni mtu unayeweza kutatua shida hiyo na umeweka taarifa zako kwenye mtandao, basi atafikia kwako na mtafanya kazi pamoja.

Vitu muhimu ambavyo unapaswa kuwa navyo ili kukuza jina lako kwenye zama hizi ni blog, kurasa kwenye mitandao ya kijamii na ujuzi unaoweza kuwasaidia wengine kuwa na maisha bora. Tumia vitu hivi kuwafikia wengi zaidi na kujenga jina lako.

MUHIMU; Nitaendesha semina ya bure kwa siku saba kuhusu KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG, bonyeza hapa kushiriki semina hii.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)