Kama ambavyo nimekuwa nasema na kusisitiza mara kwa mara, ili tufanikiwe, tunahitaji kwenda tofauti na baadhi ya mambo yetu ya asili ambayo yanatufanya tuwe na maisha fulani. Akili zetu, saikolojia yetu na hata miili yetu, ina mazoea fulani ambayo yamekuwa kikwazo kwetu kupiga hatua.
Kwa mfano, vitu ambavyo ni rahisi kufanya, ndiyo vitu ambavyo ni rahisi kutokufanya. Na hili limekuwa linawazuia wengi kwani wamekuwa wakisema ah hiyo rahisi hata mimi naweza kufanya, lakini hawafanyi, wanabaki pale walipo.
Ni rahisi sana kufanya mazoezi madogo kila siku, lakini pia ni rahisi kutokufanya, na hii inapelekea watu kuwa na afya mbovu.
Ni rahisi mno kuweka akiba ya shilingi elfu moja kila siku, ambapo ukijenga tabia hii kwa miaka, utajikuta huna madeni na una akiba na kuweza kuwekeza. Lakini pia ni rahisi kutokuweka akiba ya shilingi elfu moja kila siku, kwa sababu kuna matumizi mengi ya elfu moja hiyo, ambayo hata siyo ya msingi.
Nimekuwa nikisema na nirudie tena, mafanikio makubwa hayaji mara moja, mafanikio siyo ajali, na wala siyo mafuriko. Mafanikio makubwa yanakuja kidogo kidogo, kwa vitu vidogo unavyofanya kila siku, mafanikio ni manyunyu ambayo yanajikusanya na kuwa maji mengi.
SOMA; Kauli Kumi Za Kukuhamasisha Kutoka Kwa Mahatma Gandhi.
Kwa kuwa wengi hawajui au wanajua lakini hawazingatii hili, wamekuwa wanapuuza mambo madogo madogo na hivyo kushindwa kufanikiwa. Zingaita sana mambo hayo madogo.
Jua kile ambacho ni rahisi kufanya, ambacho ni kidogo, ndiyo pia rahisi kutokufanya na hivyo kushindwa kufanikiwa. Jitenge na kundi kubwa la watu ambao wanasema wanaweza kufanya, halafu hawafanyi. Wewe kuwa mfanyaji, zingatia mambo madogo madogo na utatengeneza mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)