Kama duniani kungekuwa kama darasani, basi kila mtu angekuwa na yale maisha anayotaka kuwa nayo. Ila kuna tofauti kubwa sana kati ya darasani na duniani, wengi hawaelewi tofauti hii na ndiyo maana wamekuwa wanafanya mambo ya ajabu.
Kama hujaelewa, darasani namaanisha mfumo wote wa elimu, kuanzia chekecheka mpaka chuo kikuu, na duniani namaanisha maisha ya kawaida baada ya elimu.
Kuna tofauti nyingi kati ya darasani na duniani, lakini leo nataka nikupe moja kubwa, ambayo inameza tofauti nyingine zote.
Tofauti kubwa kati ya darasani na duniani ni UHAKIKA. Darasani tunafundishwa uhakika, wakati duniani hakuna uhakika.
Darasani tunafundishwa kwamba ni UHAKIKA kila siku ya juma utakwenda shule, ni UHAKIKA ukifika shuleni utafundishwa, ni UHAKIKA baada ya kufundishwa utapewa mtihani, ni UHAKIKA ukisoma kwa bidii utafaulu mtihani huo.
Lakini unapokuja duniani, mambo ni kinyume na tofauti kabisa. Hakuna chochote ambacho ukikifanya una UHAKIKA matokeo yatakuja unavyotarajia. Unaweza kufungua biashara na usipate matokeo uliyotegemea, unaweza kufanya kila unachoweza kufanya na bado matokeo yakawa tofauti na ulivyotegemea. Unaweza kufanya jambo jema na watu wakakuelewa vibaya.
SOMA; Kama Una Kitu Hiki Kimoja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.
Hakuna kitu chochote ambacho tuna UHAKIKA nacho, unaweza kuipangilia siku yako vizuri lakini ikaenda tofauti na ulivyopanga. Wengi wamekuwa hawaelewi hili ndiyo maana wanaishia kukata tamaa pale mambo yanapokwenda tofauti na wanavyotarajia.
Ni wakati sasa wa kujifunza KUTOKUWA NA UHAKIKA, tuachane na ile dhana ya UHAKIKA ambayo tumekuwa tunahubiriwa miaka na miaka. Tuanze kukubaliana na hali ya kutokuwa na uhakika, tupange na kufanya mambo yetu, lakini tusikate tamaa pale matokeo yanapokuwa tofauti na mipango yetu. Hakuna mwenye uhakika kwenye dunia ya kawaida.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)