Kila hatua kwenye safari ya mafanikio ni ngumu, na ndiyo maana wengi safari hii inawashinda, hata kuanza tu ni changamoto kwa wengi.

Lakini kuna hatua ambayo ni ngumu zaidi ukilinganisha na hatua nyingine. Leo tunakwenda kuangalia hatua hii iliyo ngumu, na jinsi tunavyoweza kufanya kuwa rahisi kwetu. Kabla hatujaiangalia hatua hii ngumu, hebu tuangalie mifano hii michache;

Nafikiri umewahi kuweka malengo fulani, ukawa na mipango kabisa na ukaanza kutekeleza, lakini hukufika mbali, ukaacha. Na ulipoangalia kwa nini uliacha, siyo kwa sababu ulikuwa huwezi, wala siyo kwa sababu mambo ni magumu, ila tu kwa sababu unashindwa kuendelea kufanya.

Mfano umepanga malengo ya kiafya, kwamba utakula vyakula bora kiafya, lakini baada ya muda unajikuta umerudi kula vyakula ambavyo siyo bora kiafya. Au umepanga kuacha kilevi au mazoea fulani, lakini baada ya muda unajikuta unarudi kwenye ulevi au mazoea hayo hayo.

Wakati mwingine huhitaji hata fedha ya ziada, wala huhitaji kutumia nguvu kubwa, lakini unajikuta unashindwa kufanya kile ulichopanga kufanya. Hii inatokana na hatua hii ngumu katika safari ya mafanikio.

Hatua hiyo ni NIDHAMU.

Unaweza kupanga mambo makubwa na mazuri, unaweza kuwa na hamasa wakati wa kuanza. Lakini kama huna nidhamu, hutafika mbali, utarudi pale pale ulipoanzia na kuendelea kufanya kile ulichozoea kufanya. Nidhamu ni hitaji la msingi kabisa kwenye mafanikio, na ndiyo hatua ngumu.

Angalia, mara nyingi huhitaji kufanya mambo makubwa ndiyo ufanikiwe, bali unahitaji kufanya mambo madogo madogo kwa kurudia rudia ndiyo uweze kufanikiwa. Sasa kama huna nidhamu, utaona mambo hayo ya kurudia rudia ni kama hayakufai wewe, na hivyo utaacha.

Wengi wa wanaoshindwa kufanikiwa siyo kwamba wanashindwa kufanya makubwa, ila mara nyingi wanashindwa kufanya yale madogo madogo. Huona kama hayafai au huona kama ni ya kawaida sana, hivyo kutoyapa uzito na hivyo kushindwa kufanikiwa.

Kwa mfano, ni watu wengi sana ambao wanaishi bila ya kuwa na akiba yoyote ile kwenye maisha yao, kwa miaka mingi mno. Lakini unafikiri watu hawa wangekuwa kwenye madeni maisha yao yote kama wangeamua kuweka akiba ya shilingi elfu moja tu kila siku? au hata shilingi mia tano? Siyo kwamba haiwezekani, ila kinachokosekana ni nidhamu.

Nidhamu ya kuacha matumizi madogo madogo yasiyo ya msingi, ili kuokoa elfu moja au mia tano kwa siku ni changamoto.

Nidhamu ya kuiacha akiba bila ya kuitumia hasa pale mtu anapokutana na changamoto ndogo ndogo ni tatizo.

SOMA; Uhusiano Wa Nidhamu Binafsi Na Mafanikio Makubwa.

Je unajijengeaje nidhamu?

Hapa kuna mambo matano muhimu ya kuzingatia ili kujijengea nidhamu.

  1. Jua madhaifu yako, kila mmoja ana madhaifu yake, ni vyema ujue madhaifu yako ili uweze kuchukua hatua sahihi. Kama hujui udhaifu wako uko wapi, utaendelea kurudia makosa yale yale.
  2. Kuwa na mpango wa kila unachofanya na wa kila siku yako. usifanye jambo lolote bila ya kupangilia, kwa sababu itakuwa rahisi kwako kuchukuliwa na mambo mengine.
  3. Ondoa vishawishi vinavyokurudisha nyuma. Katoka yale maeneo unayotaka kujijenga nidhamu, angalia ni vishawishi gani vinakurudisha nyuma, kisha ondokana navyo au viepuke.
  4. Jifunze kuvumilia hisia usizozipenda. Kila mtu anapenda furaha, lakini siyo kila wakati utakuwa na furaha. Kuna wakati utakuwa na huzuni, hasira, upweke, hizi ndizo nyakati wengi wanakosa nidhamu binafsi. jifunze kuvumilia hisia hizi bila kutafuta njia mbadala ya kuzikimbia.
  5. Pata taswira ya manufaa ya baadaye. Mara nyingi watu wamekuwa wakiangalia kidogo wanachopata sasa na kusahau kikubwa wanachoweza kupata baadaye. Kuwa na taswira ya namna maisha yako yatakavyokuwa bora pale utakapokamilisha kile unachofanya. Hii itakufanya uendelee kukifanya.

Jijengee nidhamu, ni msingi muhimu wa mafanikio na ndiyo hatua inayowashinda wengi.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)