Ukiangalia watu na makampuni yaliyoleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yetu na kuwa na mafanikio makubwa, walifanya kile ambacho wengi hawawezi kufanya. Badala ya kuwapa watu kile ambacho walikuwa wanataka, waliwapa watu kile ambacho ni bora zaidi.
Kwa mfano, kabla ya kuja kwa magari usafiri mrefu ulifanyika kwa njia ya treni na usafiri mfupi kwa njia ya magari ya kuvutwa kwa punda na farasi. Kama watu wangeulizwa wanachotaka ni kipi kwenye usafiri, moja kwa moja wangesema tunataka funda na farasi ambao wana mwendo wa kasi zaidi. Au wangesema wanataka usafiri wa treni ambao ni bora zaidi.
Lakini wenye maono hawakutaka kuwapa watu kile wanataka, badala yake walifikiria tofauti na wakaona kuna njia tofauti ya kuweza kufanya usafiri kuwa bora zaidi. Ndipo yakagunduliwa magari. Na bado ugunduzi haukuishia hapo, zilikuja ndege na aina nyingine bora za usafiri.
Hayo ni ya zamani, ngoja tupeane mifano ya hivi karibuni, ambao wote tunaweza kuelewa vizuri, pata picha ya mwaka 2005, hebu niambie ungeulizwa unataka nini kwenye mawasiliano ungesema unataka wasap? Vipi kuhusu facebook na mitandao mingine ambayo wengi tunaitumia kila siku? ni dhahiri kwamba tusingekuwa na mawazo ya vitu kama hivyo. Sisi tungekuwa tunafikiria kupata njia rahisi ya kuwasiliana, labda kwa bei rahisi zaidi. Wenye maono wakaona kuna njia bora zaidi ya mawasiliano, wakatuletea, mwanzoni wengi hawakuelewa lakini baadaye kila mtu anafurahia.
Sasa hiki ndiyo nataka kila mwana mafanikio afanye, usiwape watu kile wanachotaka, bali wape kile ambacho wewe unajua ni bora kwao na kwa viwango ambavyo upo tayari kusimama na kusema ni mimi niliyefanya hivyo. Usisukumwe na hitaji la watu la muda mfupi na kushindwa kutoa kile ambacho wewe unajua ni bora na kinaendana na viwango unavyotaka wewe.
Siyo rahisi, wengi hawatakuelewa, wengi watakupinga lakini utapata wale ambao wanaelewa kile unachofanya na baadaye wengi zaidi wataelewa.
Ndiyo kuna wengi ambao wapo tayari kuwapa watu kile wanachotaka, na kutengeneza faida kwa njia hiyo, lakini watu hawa hawadumu kwa muda mrefu. Unaweza kuchagua kuwa wao na kudumu kwa muda mfupi, au unaweza kuchagua kuwa mwenye maono, kuwa mtaalamu ambaye unawapa watu kile ambacho ni bora, na ukajiweka kwenye nafasi ya kunufaika mara zote.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DEEP WORK (Mbinu Za Kufanya Kazi Yenye Maana Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu).
Kuwapa watu kile wanachotaka ni hatari sana kwa mafanikio yako. mara zote angalia ni namna gani unaweza kuwapa watu kile ambacho ni bora zaidi. Na kwa kuwa wewe mwenyewe ndiye uliyechagua kile unafanya, unahitaji kujua zaidi ya wengine kile unachofanya na namna ya kuboresha zaidi. Usiwe mtu wa kuwapa watu kile wanachotaka, bali kuwa mtu wa kuwapa watu kile ambacho ni bora kabisa kwao.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)