Kila mtu kuna kitu ambacho anataka au kupenda sana kufanya, lakini hajaanza kufanya mpaka sasa. Kikubwa ambacho kinawazuia watu kuchukua hatua ni kusubiri kwa kufikiri kwamba wakati wa kufanya bado. Wengi wamekuwa wakifikiri kwamba bado hawajawa tayari, au bado mazingira hayajawa mazuri kwa wao kuanza.
Lakini rafiki yangu, mwana mafanikio mwenzangu, leo nataka nikuambie ukweli kama ulivyo, kila muda unaosubiri ni muda ambao umechagua kuupoteza. Kwa nini nasema hivi;
Kwanza hakuna siku ambayo utajiona upo tayari, hakuna siku utaona umeshakamilisha kila kitu ndiyo uanze, hivyo kusubiri uaminifu ni kujidanganya.
Pili hakuna siku ambapo changamoto zitaisha kabisa, kila kitu unachopanga kufanya kuna changamoto ambazo utakutana nazo, kabla ya kuanza na hata baada ya kuanza. Hivyo kufikiri kuna wakati changamoto zitaisha kabisa, ni kujidanganya, changamoto zipo na zitaendelea kuwepo.
Tatu hakuna siku mazingira yatakuwa kamili kama unavyofikiria wewe. Usifikiri dunia itakupa kila unachotaka ili kuanza kufanyia kazi wazo lako, unatakiwa kuisumbua dunia, haikupi kirahisi ni mpaka uisumbue.
Kwa nini wengi tumekuwa tunasubiri?
Sababu kwamba bado hatujawa tayari ni sababu ya juu juu, sababu halisi inayotuzuia kuanza ni hofu ya kutokujua matokeo yatakuwaje. Huwa tuna hofu pale tunapotaka kufanya jambo ambalo hatujawahi kulifanya hapo awali. Kwa kuwa hatupendi kukubali hofu ndiyo kikwazo, basi tunatafuta njia ya kuificha hofu hiyo, hivyo tunajiambia hatujawa tayari, wakati tunajua kabisa hakuna wakati ambao tutakuwa tayari kwa kila kitu.
SOMA; Kuna Makundi Matatu Ya Watu; Je Wewe Upo Kwenye Kundi Lipi Kati Ya Haya? Fungua Kujua.
Ni hatua ipi tuchukue ili kuacha kusubiri?
Hatua pekee ni kuanza, kama ambavyo tumekuwa tunasema, JUST DO IT. Anzia pale ulipo, anza na kile ulichonacho na anza kidogo. Kadiri unavyoendelea kukua utaendelea kujifunza na kuzivuka changamoto. Mambo yote ambayo huyajui utayajua pale utakapoanza kufanya.
Najua wasi wasi wako ni je itakuwaje kama ukishindwa? Na mimi nakuambia utashindwa, lakini hutakufa, hivyo utajifunza zaidi.
Ni kitu gani ambacho umekuwa unasema utafanya lakini hujaanza kufanya? Anza kukifanya leo, anza kukifanya kwa hatua ndogo.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)