UCHAMBUZI WA KITABU; PROSPERITY ON PURPOSE (Mwongozo wa kuishi maisha ya mafanikio makubwa).

Linapokuja swala la mafanikio, mengi yamesemwa na kuandikwa. Kwa kifupi kila mtu ana la kusema kuhusu mafanikio, kuanzia waliofanikiwa wenyewe mpaka wale ambao wameshindwa.
Pamoja na mengi ambayo tayari yamesemwa na kuandikwa bado kuna mengi tunahitaji kujifunza na kujikumbusha kila siku kuhusu mafanikio. Na hapa ndipo mwandishi Justin Herald anapotupa mwongozo wa kuishi maisha ya mafanikio.

Kwa kuanza mwandishi anatofautisha utajiri na maisha ya mafanikio. Kuna watu ambao lengo lao kwenye maisha ni kuwa matajiri, hivyo chochote wanachofanya, wanaangalia fedha kwanza. Ila pia wapo watu ambao wanataka kuishi maisha ya mafanikio, wanaangalia namna wanavyoweza kuboresha maisha ya wengine na yao pia. Wale wanaowaza utajiri pekee wanaweza kuupata ila maisha yao yanakuwa siyo bora na hawayafurahii. Ila wale wanaotaka maisha ya mafanikio, wanakuwa na maisha bora na utajiri pia.

Mwandishi anatukumbusha kwamba utajiri siyo lengo kuu la maisha, ila utajiri ni matokeo ya kuwa na maisha ya mafanikio. Hivyo kama tunataka kuwa na maisha bora na ya utajiri, tusiangalie utajiri pekee, bali tuangalie mafanikio kwa ujumla, yetu na ya wale wanaotuzunguka. Utajiri utakuwa matokeo ya yale maisha ya mafanikio tunayoishi.
 
SOMA; Kama Unataka Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako, Acha Kuogopa Kufanya Mambo Haya.

Karibu tujifunze yale muhimu kutoka kwenye uchambuzi wa kitabu hiki.
1. Tofauti kuu ya utajiri na mafanikio.
Mwandishi anatukumbusha ya kwamba utajiri ni pale ambapo tunajifikiria sisi wenyewe, tunafikiria kupata kile ambacho tunakitaka. Tunaweza kukazana na kupata, lakini maisha yetu yanaendelea kuwa yalivyo. Lakini maisha ya mafanikio ni pale unapojifikiria wewe na wengine. Pale unapoangalia ni jinsi unavyoweza kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

2. Kanuni kuu nne za maisha ya mafanikio.
Zipo kanuni nyingi za maisha ya mafanikio, ila ukizileta kanuni hizi pamoja, unapata kanuni kuu nne ambazo ni kama ifuatavyo;
Moja; ni lazima uwe na dhamira na kiu ya kweli ya kutoka pale ulipo sasa, lazima uwe tayari kuleta mabadiliko kwenye maisha yako, ujitoe na usikubali kurudishwa nyuma na chochote.

SOMA; Kama Unafanya Mambo Haya 10 Katika Maisha Yako, Ni Lazima Ufanikiwe.

Mbili ni lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu ili kuweza kufika pale unapotaka kufika. Hii ni kwa sababu katikati ya safari utakutana na vikwazo, changamoto na vishawishi vingi. Kama huna nidhamu, huwezi kufika.

Tatu; ni lazima uwe mnyenyekevu. Bila ya unyenyekevu huwezi kuwa na mafanikio makubwa, na ukiyapata hayatadumu. Hii ni kwa sababu mafanikio yako yanatokana na ushirikiano bora na wengine, na usipokuwa mnyenyekevu ukifanikiwa utaharibu mahusiano yako na wengine.

Nne; ni lazima uwe tayari kupokea mrejesho wa wengine. Siyo mara zote utapata kile unachotaka, au kukubaliwa kile unachoomba. Unahitaji kuweza kupokea mrejesho hasi na chanya kutoka kwa wengine na kufanyia kazi.

 3. Usiweke lengo la kuwa tajiri.
Kuna tofauti kubwa ya kuwa tajiri na kuwa na mafanikio ya kifedha (uhuru wa kifedha). Unapoweka lengo la kuwa tajiri, kila unachokiangalia unaangalia fedha pekee, siyo mbaya lakini utajinyima fursa nyingi. Wakati mwingine unaweza kujikuta umeingia kwenye mambo ambayo siyo mazuri kutokana na uchu wako wa utajiri. Lakini lengo lako linapokuwa mafanikio ya kifedha, au uhuru wa kifedha, unakuwa na mtazamo wa tofauti unajua kwamba unawahitaji wengine katika safari yako hiyo. Unawajenga wengine ili wewe kuweza kufikia lengo lako.

SOMA; Dalili Sita(6) Kwamba Una Fikra Hasi Zinazokuzuia Kufikia Mafanikio Na Jinsi Ya Kuondokana Nazo.

4. Kitu kimoja kinachoweza kukuzuia usifanikiwe.
Uchoyo ni tabia moja ambayo imewazuia watu kuishi maisha ya mafanikio. Na mara zote wale watu ambao wanaangalia fedha pekee ndiyo wamekuwa wachoyo sana. Hii ni kwa sababu wanaogopa kupoteza fedha na hivyo kuzishikilia, kwa njia hii wanazidi kujinyima fursa za kuwaongezea kipato. Epuka uchoyo kama lengo lako ni kuwa na maisha ya mafanikio.

5. Ubinafsi ni sumu kubwa ya mafanikio.
Kitu kingine ambacho kimekuwa kinawazuia watu kuishi maisha ya mafanikio ni ubinafsi. Ubinafsi ni tofauti kidogo uchoyo, kwenye uchoyo unashikilia kile ulichonacho na hutaki wengine wakipate, kwenye ubinafsi unajifikiria wewe zaidi hata kama wengine wataumia kwa kufanya hivyo. Unapokuwa mbinafsi huku ukiwa na lengo la kuwa tajiri, utaumiza watu wengi mno. Hii itakuzuia kufanikiwa kwa kiasi kikubwa/

6. Mafanikio siyo lele mama.
Kitu kimoja kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni mtazamo walionao kuhusu mafanikio. Waliofanikiwa wanajua kabisa kwamba mafanikio siyo lele mama, wanahitaji kuweka juhudi na bidii kubwa ili kupata kile wanachotaka. Na hata wakishakipata, wanahitaji kuweka juhudi zaidi ili kulinda na kuongeza zaidi. Lakini wale wanaoshindwa, wana mtizamo tofauti, wanaamini wale waliofanikiwa walipata bahati ambayo wao bado hawajaipata. Na pale wanapojitahidi kuongeza bidii kidogo na kupata mafanikio madogo, wanajisahau kabisa na kuacha kuweka juhudi, mwishowe wanaanguka.

SOMA; Hii Ndiyo Siri Kubwa Ya Kuishi Maisha Marefu Na Yenye Mafanikio Makubwa.

7. Upo hapo ulipo sasa kwa sababu.
Hujafika hapo ulipo sasa kwa ajali au bahati mbaya, bali umejitengenezea mazingira yote yanayokuzunguka sasa. Siyo serikali, siyo wazazi na wala siyo marafiki, bali wewe mwenyewe, kwa kufanya au kutokufanya vitu fulani, umejifikisha hapo ulipo sasa.
Sasa hii ni habari njema sana kwa sababu;
Kwanza; unaweza kuwa na kesho bora kuliko leo, kwa sababu ulichofanya jana unaweza kukibadili leo.
Mbili; unaweza kuchukua hatua leo na kesho ukawa na maisha ya tofauti na uliyo nayo leo.

8. Tofauti ya umasikini na fikra za kimasikini.
Kuna watu ambao ni masikini, ambao hawa siku moja wanaweza kutoka kwenye umasikini na kuwa na maisha ya mafanikio. Ila kuna watu ambao wana fikra za kimasikini, ambao hawa hawawezi kutoka kwenye umasikini wao kwamwe, mpaka pale watakapobadili fikra zao za kimasikini. Mpe chochote mtu mwenye fikra za kimasikini na atakupa sababu ya kuendelea kuwa masikini.

SOMA; Kama Unataka Kuwa Tajiri Katika Maisha Yako, Hakikisha Unaishi Maisha      Haya.

9. Kichocheo cha fikra za kimasikini.
Kitu kimoja ambacho kinachochea sana fikra za kimasikini ni kufikiria vile vitu ambavyo huna badala ya kufikiria vile ambavyo unavyo kwa sasa. Watu wenye fikra za kimasikini muda wote wanalalamikia vile vitu ambavyo wamekosa, wana kila sababu kwa nini hawapigi hatua kwenye maisha yao. Lakini hawawezi kuangalia kile walichonacho sasa na jinsi wanavyoweza kukitumia kufika mbali zaidi.

Ondokana kabisa na fikra za aina hii, usitumie muda mwingi kufikiria unachokosa, badala yake angalia vile ulivyonavyo na unavyoweza kuvitumia kuondoka hapo ulipo sasa.

10. Mfano wa nusu glasi kwenye fikra za kimasikini.
Katika kupima mtazamo wa watu, mfano wa nusu glasi umekuwa ukitumika. Mfano huu ni inachukuliwa glasi ya maji na kuwekwa maji nusu, kisha mtu anaulizwa anaona nini. Kuna ambao wataona glasi imejaa nusu, hawa wana mtazamo chanya kwamba angalau kuna kitu. Ila kuna ambao wataona glasi ipo tupu nusu, hawa wana mtazamo hasi wa kuona walichokosa.
Wenye fikra za kimasikini wao muda wote wanaona glasi ipo nusu tupu na kutafuta nani wa kuijaza au nani kaifanya iwe tupu. Hili linawazuia kutumia fursa ya nusu iliyopo kuboresha maisha yao zaidi.

11. Tabia ambazo tumekuzwa nazo ni kikwazo cha mafanikio.
Kila binadamu anazaliwa akiwa mpya kama kitabu kipya. Anavyokua anajifunza kutokana na mazingira yanayomzunguka. Jamii zetu nyingi hakuna miongozo ya maisha ya mafanikio, hivyo watu wamekuwa wakiishi maisha ya kusogeza siku, watoto nao wanaiga maisha hayo. Ndiyo maana utakuta maisha kwenye jamii yanafanana kwa kiasi kikubwa.
Uzuri ni kwamba unaweza kuvunja tabia hizi ulizofundishwa kwenye jamii na kujijengea tabia za mafanikio.

12. Unahitaji kufanya kitu cha tofauti na unavyofanya sasa.
Kama maisha yako yapo vile vile miaka nenda miaka rudi, hakuna mchawi hapo, bali maelezo ni rahisi, umekuwa unafanya kitu kile kile miaka yote hiyo. Kwa mfano, kama wewe ni mwajiriwa ambaye unategemea mshahara wako pekee kuendesha maisha, hakuna kitakachobadilika kwenye maisha yako.
 Kama unataka maisha yako yabadilike, ni lazima uanze kubadilika wewe kwanza, uanze kubadili vile unavyofanya, uanze kufanya kwa tofauti na hapo utaona matokeo ya tofauti.

13. Akili pekee haitoshi, wazo bora au ajira bora pekee haitoshi.
Unahitaji kuwa na mapenzi makubwa sana kwenye kile unachofanya kama kweli unataka kuwa na maisha ya mafanikio. Na hapa ndipo maisha ya mafanikio yanapotofautiana na utajiri. Kwa mfano mtu anaweza kufanya kazi ambayo inamwingizia kipato kikubwa, akawa tajiri lakini bado akawa na tatizo kubwa, ile kazi haipendi na hivyo kuona maisha yake kama utumwa. Hivyo ili kuwa na maisha ya mafanikio ni lazima upende sana kile unachofanya. Unapokuwa na mapenzi makubwa kwenye kile unachofanya, hata kama kipato siyo kikubwa, utakuwa na maisha bora.

SOMA; Kama Una Maisha Haya Hufiki Popote, Kimafanikio.

14. Vikwazo na changamoto hazikwepeki.
Panga malengo makubwa utakavyo, weka mipango bora uwezavyo. Lakini usisahau kitu hiki kimoja, vikwazo na changamoto havikwepeki, hata ungejiandaa kiasi gani. Na hapa ndipo tofauti nyingine kati ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa inapoonekana. Wanaofanikiwa wanategemea kukutana na vikwazo na wanavitatua, wanaoshindwa hawategemei vikwazo, hivyo wakikutana navyo wanaacha kabisa kufanya kile wanachofanya.
Kumbuka hili kila siku unapoamka kitandani, hakuna njia ya mteremko ya kukufikisha kwenye mafanikio. HAKUNA.

15. Chochote unachojaribu kufanya siyo kipya.
Wewe siyo mtu wa kwanza kufanya kile ambacho unajaribu kufanya, wapo wengine walishafanya kabla yako, wengine wakafanikiwa huku wengine wakishindwa. Hivyo chochote unachofanya, jifunze kwa wengine waliofanya pia. Wengi hawana muda wa kujifunza, wanaishia kufanya kwa mazoea, na hivyo kuendelea kuwa kawaida. Na mbaya zaidi, wanarudia makosa yale yale ambayo waliowatangulia waliyo yafanya na wakashindwa. Jifunze sana juu ya kile unachofanya kwenye maisha yako.

16. Viungo vinne vya maisha ya mafanikio.
Tumegusia sana tofauti ya utajiri na maisha ya mafanikio. Utajiri unapima eneo moja la maisha ambalo ni fedha. Maisha ya mafanikio yana maeneo mengine muhimu ambayo ni lazima tuyazingatie kama tunataka kuwa na maisha ya mafanikio.
Moja; afya, kama huna afya ya mwili huwezi kupambana ili kufanikiwa.
Mbili; hisia, kama huwezi kudhibiti na kusimamia vizuri hisia zako, mafanikio kidogo yatakupoteza kabisa.
Tatu; mahusiano, yafaa nini kuwa na utajiri mkubwa ikiwa huna maelewano na ndugu zako au familia yako?
Nne; fedha, hapa ndipo wengi wanapoishia kuhesabu, wanazishika lakini wanashangaa maisha bado ni magumu kwao.

17. Mafanikio ni kutoa na kupokea.
Wanaoshindwa wanajua kitu kimoja, mafanikio ni kupokea, kupata tu wakati wote na hakuna kutoa. Wanaofanikiwa wanajua mlinganyo sahihi, mafanikio ni kupokea na kutoa. Huwezi kupokea kama hutoi, na hivyo wamekuwa wanatoa kwa wengine. Ni asili ya dunia kwama kila pengo lazima lizibwe, na pengo dogo linaweza kuzibwa na kifusi kikubwa. Hivyo wanaofanikiwa wanatumia vizuri kanuni hii ya asili, wanatoa na baadaye wanapokea mara dufu.

SOMA; Je, Unataka Kuishi Maisha Ya Mafanikio Siku Zote? Hakikisha Unaishi Maisha Haya Kila Siku. 

18. Unapotoa kuwa na mtazamo sahihi.
Kama tulivyoona ili ufanikiwe lazima pia uwe mtoaji na siyo mpokeaji peke. Ila kuwa makini unavyotoa, hutoi ili upokee, kama vile kurudishiwa, badala yake unatoa kwa sababu unataka kutoa. Na siyo kwamba ukitoa leo basi kesho unapokea, inaweza kuchukua hata miaka, lakini lazima utapokea. Na muhimu zaidi usitumie kutoa kwako kama nafasi ya kuwanyanyasa wengine. Usianze kuwaambia watu mimi nilikupa hiki hivyo na wewe nipe hiki, kanuni ya asili haiendi hivyo. Toa kwa moyo mmoja, usitegemee kupata chochote kutokana na kutoa kwako. Huenda hata unayempa hatakushukuru, usijali wewe umetaka kutoa.

19. Utumie uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Ni tafiti za kisayansi zinaonesha kabisa kwamba uwezo ulio ndani yetu ni mkubwa mno kuliko ambavyo tunautumia. Yaani uwezo tunaoutumia kwenye maisha yetu ya kawaida, ni mdogo sana ukilinganisha na uweo mkubwa tulionao. Ukitaka kupima hili angalia pale unapojikuta kwenye hali ya hatari au changamoto, utajikuta unafikiri kuliko ilivyo kawaida yako. Kuishi maisha ya mafanikio ni lazima utumie uwezo huu mkubwa uliopo ndani yako. Japo huwezi kuutumia wote, hakikisha kila siku unapiga hatua kubwa zaidi ya ulizopiga nyuma.

20. Tabia ni kiungo muhimu mno katika kuishi maisha ya mafanikio.
Kuna watu hata wapewe nini, bado maisha yao yanakuwa magumu, hii inatokana na tabia ambazo wamejijengea. Tabia zinaweza kukupeleka kwenye mafanikio au zinaweza kukuzuia kufikia mafanikio yako.
Mwandisi ametushirikisha tabia nne muhimu tunazohitaji kuwa nazo ili kufanikiwa;
Moja; maadili, lazima uwe na miiko ya vitu gani lazima ufanye na vipi huwezi kufanya kamwe.
Mbili; kujitoa kwa ajili ya kufanikiwa. Kuna wale ambao wanasema watafanya, na kuna wale ambao wanafanya, hawarudishwi nyuma na chochote.
Tatu; ujasiri, kama huwezi kupambana hutafika mbali.
Nne; unyenyekevu, tumeshajifunza huko juu.
Kama umechagua kuishi maisha ya mafanikio, basi lazima ujue mwongozo sahihi na kuufuata. Mafanikio siyo bahati waliyotengewa wachache. Bali ni matokeo wanayopata wale wanaoyafanyia kazi.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya mafanikio, tujifunze kwa pamoja kila siku. Karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA tuwe karibu zaidi. Kujiunga tuma ujumbe wenye neno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya whatAssp kwenda namba 0755 953 887. Karibu sana, mafanikio ni haki yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: