Nimewahi kutoa mfano huu kwenye makala za nyuma, lakini leo nitaurudia tena ili tuweze kujifunza.

Kijana mmoja alikuwa na babu yake wamekaa nje barazani wakipiga hadithi, sehemu waliyokaa ni pembezoni mwa barabara ambapo watu wanapita. Wakati wanaendelea na hadithi zao, wakapita watu na mizigo, wakasimama na kuwauliza, sisi tumetoka eneo la jirani, tunahama, ungependa kujua watu wa eneo hili wana tabia gani? Babu yule akawauliza, kule mnakotoka watu wana tabia gani? Wakajibu wana tabia mbaya, wana wivu, masengenyo na roho mbaya. Yule mzee akawajibu hata hapa watu wana tabia hizo hizo. Basi watu wale wanaendelea na safari yao.

Wakiwa wanaendelea na hadithi zao, wakapita watu wengine nao wanahama, wakasimama kuuliza, tumetoka eneo la mbali na tunatafuta pa kuhamia, watu wa eneo hili wana tabia gani? Yule mzee akawauliza, kule mnakotoka watu wana tabia gani? Wakajibu wana tabia nzuri, ni wema, wanajali na kusaidiana. Mzee akawajibu hata hapa watu wana tabia hizo hizo. Basi wakasema wanahamia.

Baadaye yule kijana alimuuliza babu yake, mbona sijakuelewa, wale umewaambia hapa kuna watu wabaya, hawa umewaambia kuna watu wazuri. Mzee alimwangalia kijana na kumwambia, watu ni wazuri na watu ni wabaya, unachagua kipi unachotaka kuona na utakiona.

Hii iko wazi kabisa;

Uliza mtu yeyote ambaye amewahi kuondoka kwenye kazi moja kwenda nyingine akiamini kule atakutana na mambo bora zaidi.

Uliza mtu yeyote ambaye amewahi kuachana na mwenza wake na kuamini atapata mwingine ambaye ni bora zaidi.

Uliza watu ambao wamewahi kuhama eneo moja na kwenda eneo jingine kwa kuamini kule ni bora zaidi.

Kwenye kila hali kama hizo, watu wanaishia kupata kitu kile kile ambacho wamekikimbia sehemu waliyotoka. Hii ni kwa sababu tatizo siyo eneo ambalo upo, wala tatizo siyo watu ulionao, bali tatizo ni kipi ambacho kipo ndani yako. Kama haupo vizuri hapo ulipo sasa, basi hakuna sehemu nyingine ambayo unaweza kwenda na ukawa vizuri zaidi ya ulivyo sasa. Uzuri unaanzia ndani yako wewe na siyo nje yako.

Hii ina maana kwamba kama unataka kutoka sehemu moja kwenda nyingine, sababu isiwe kukimbia pale ulipo sasa kwa sababu hakukufai, kwa sababu utakapoenda utakutana na unachokimbia. Bali sababu iwe kuwa bora zaidi baada ya kupawezea vizuri pale ulipo sasa. Iwe ni kwenye kazi, biashara au hata makazi.

SOMA; Jambo Moja La Kukumbuka Kuhusu Mabadiliko.

Hapo ulipo sasa, kama huna furaha, kama huyafurahii maisha yako, hakuna sehemu nyingine yoyote unayoweza kwenda ikakuletea furaha. Anza kufanya mabadiliko ya ndani yako ukiwa hapo ulipo sasa, ili uweze kufurahia popote ambapo itaenda.

Popote unapokwenda, kuna kitu kimoja huwezi kukikimbia, wewe mwenyewe, utaenda na wewe popote utakapokwenda. Hivyo mabadiliko ya kweli siyo kubadili eneo unalokaa, wala kazi unayofanya, badala yake mabadiliko ya kweli ni kuanza kubadilika wewe mwenyewe. Anza kubadilika na mazingira uliyopo yatabadilika.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)