Habari za leo rafiki?
Karibu kwenye kipengele hiki kipya cha NYEUSI NA NYEUPE ambapo tunachambua jambo kwa namna lilivyo. Hapa tunaweka ushabiki wa aina yoyote pembeni na kuutafuta ukweli wenyewe wa jambo husika. Kwa kuwa siku zote ukweli huwa unauma, kuwa tayari kukutana na vitu ambavyo hutavipenda, lakini ndiyo ukweli wenyewe. Makala hizi zitakuwa zinakujia kila siku ya jumapili kupitia AMKA MTANZANIA.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia kwa undani kuhusu ajira, hasa ugumu wa kuacha ajira ambayo ni ngumu na hailipi. Hili ni jambo ambalo nimekuwa naliona kwa wengi, watu wanang’ang’ana na ajira ambazo ni ngumu kwao na mbaya zaidi hata kulipwa hawalipwi. Lakini watu hao bado hawathubutu kuacha ajira hizo.

Miaka ya nyuma nimewahi kufanya kazi kwenye taasisi fulani, kulikuwa na wafanyakazi ambao wana miaka mingi wanadai taasisi hiyo lakini hawalipwi. Na wakati huo pia bado walikuwa hawapati mishahara yao kwa wakati, kwa kifupi maisha yao yalikuwa ni magumu, lakini bado hakuna ambaye alikuwa na wazo la kuondoka kwenye ajira hiyo. Mbinu walizokuwa wakipanga ni namna gani ya kupambana walipwe mishahara yao kwa wakati na kulipwa madeni yao. Na hapo ulikuwa ukiangalia, taasisi yenyewe ilikuwa haifanyi vizuri kibiashara kusema kwamba inatengeneza faida kubwa. 
 

KUPATA KITABU HIKI BONYENZA MAANDISHI HAYA.


Nimekuwa pia najifunza sana kwa wale ambao wananiomba ushauri na marafiki wengine. Wengi ambao tayari wapo kwenye ajira, wana ndoto ya siku moja kuondoka kwenye ajira hizo, lakini siku hiyo huwa haifiki, kila siku kuna sababu ya kwa nini waendelee kuwa kwenye ajira hizo.

Leo nataka tuangalie NYEUSI NA NYEUPE kwenye swala hili la kuacha ajira na kwenda kwenye ajira nyingine au kujiajiri. Hili ni jambo gumu kidogo, ambalo tunahitaji kuliangalia kwa kina ili tuweze kujua msingi wake na pale tunapotaka kuchukua hatua, tuwe na taarifa sahihi.

Tafiti nyingi ambazo zimekuwa zinafanywa, zinaonesha kwamba watu wengi hawaridhishwi na ajira walizonazo. Pia watu wengi ambao wamekuwa wanapatwa na msongo wa mawazo, ajira imekuwa chanzo kikuu cha kufikia hapo. Kwa sababu kazi inachukua karibu nusu ya muda wa mtu, kazi inapokuwa tatizo, hata maisha ya mtu yanakuwa tatizo kubwa. Tunaona haya kila siku, lakini kwa nini bado watu hawawezi kuondoka wenyewe kwa hiyari?

Kuna wengine ambao wanakuwa wanaona kabisa kazi zao hazina matarajio yoyote ya mbeleni. Kwa namna wanavyochukuliwa kwenye kazi hizo, wanaona kabisa hakuna anayejali kama wapo au hawapo. Lakini watu hao hawawezi kuchagua kuacha kazi hizo wao wenyewe, watasubiri mpaka wafukuzwe au kupunguzwa kazi.
Wapo wengi ambao wanafanya kazi miaka na miaka, lakini mishahara yao haijawahi kukutana. Yaani akipokea mshahara mmoja unaisha kabla mshahara mwingine haujatoka, anakuwa ni mtu wa kukopa na kulipa madeni kila mwanzo na mwisho wa mwezi. Mtu anaweza kwenda hivi kwa miaka kumi mpaka ishirini, lakini hawezi kufika mahali na kusema sasa imetosha, kazi hii siitaki tena.

Kuna watu wengi ambao wamekuwa wakiogopa kuacha kazi zao wenyewe, baadaye inatokea wamefukuzwa kazi hizo, ndiyo wanapata akili ya kufanya makubwa kwenye maisha yao. Baadaye wanakuwa na maisha bora sana na kushukuru sana kufukuzwa kwao kazi. Na hata wale ambao walikuwa nao kwenye kazi moja, ila wakabaki kwenye ajira, wakiwaangalia wanaona kweli maisha yao yamebadilika baada ya kufukuzwa kwenye ajira, na wakati wao wana ajira lakini maisha ni magumu. Lakini bado hawatathubutu kuacha ajira zao na kushika hatamu ya maisha yao.

Hapa kuna jambo kubwa na zito, ambalo huwezi kulichukulia juu juu, kwamba watu waamue kuteseka kama kuna njia nyingine ya wao kuwa na maisha bora. Ndiyo maana tunakwenda kuangalia NYEUSI NA NYEUPE kwenye hali hii ya kushindwa kuondoka kwenye ajira kwa hiyari yako mwenyewe.

Kwa nini ni vigumu sana mtu kuondoka kwenye ajira ambayo haimridhishi?

1.     Uongo wa zama na zama.
Sababu namba moja na kubwa kabisa ya watu kushindwa kuondoka kwenye ajira ni ule uongo ambao tumekuwa tunaimbiwa miaka na miaka. Uongo huu umenasa kabisa kwenye mawazo yetu na kuutoa ni kazi ngumu sana.
Fikiria tangu unazaliwa, unakua, unaenda shule ya msingi, sekondari, chuo na hatimaye kuingia kwenye ajira, wimbo ni mmoja, soma kwa bidii, faulu, utapata kazi nzuri na kuwa na maisha bora. Tumelishika hili maisha yetu yote, tumelifanyia kazi, na mwishowe tunapata kazi, lakini bado maisha yetu hayawi bora. Lakini mbona bado hatustuki na kuchuka hatua? Kwa sababu tunaendelea kudanganywa, tena na tena na tena.
Safari hii uongo unabadilika, kwamba umeshapata kazi, lakini maisha yako ni magumu kwa sababu upo ngazi ya chini, sasa kuwa na adabu, fanya kazi zako vizuri, tii sheria na utapanda cheo, siku moja utakuwa mkurugenzi wa kampuni au shirika hili na maisha yako yatakuwa bora sana. Sasa uongo huu ndiyo unamaliza wengi na ndoto zao. Hapa watu wanajiambia kwamba kama wakiweza kuvumilia, muda siyo mrefu watapanda vyeo na maisha kuwa bora.

Uongo huu una matatizo mawili;
Tatizo la kwanza, kadiri cheo kinavyoongezeka na kipato kuongezeka na matumizi nayo yanabadilika, ugumu wa maisha nao unaongezeka. Kwa kuwa mfanyakazi wa chini unaweza kwenda kazini kwa usafiri wa umma, lakini kadiri cheo kinapanda utaona huwezi tena kwenda na usafiri wa umma, unahitaji usairi wako, na siyo tu usafiri, bali usafiri wa maana, unaoendana na hadhi yako. Gharama zinaanza kwenda juu, kuanzia usafiri, mavazi, nyumba, na hata chakula unachokula ukiwa kazini.

Tatizo la pili; nafasi inayoangaliwa ni moja, wanaoiangalia ni wengi. Bosi ni moja tu kwenye kitengo cha kazi, mkurugenzi ni mmoja tu kwenye kampuni au taasisi, lakini kuna wafanyakazi zaidi ya 20 ambao wanaangalia nafasi hiyo moja. Kwa hesabu za kawaida tu ni kwamba haiwezekani kila mtu akapata nafasi hiyo, lakini bado tutajidanganywa, kwamba sisi ni bora zaidi ya wengine, hivyo tutaipata, na tunashangaa siku zinakwenda lakini hatuipati.

2.     Wazazi, familia, ndugu, jamaa na marafiki.
Hawa watu wanaotuzunguka, ni kikwazo kikubwa sana kwetu kufanya maamuzi ya kuondoka kwenye ajira. Kwa jamii zetu, ni vigumu sana kueleweka pale utakapowaambia watu wako wa karibu kwamba kazi uliyonayo huoni kama itakufikisha kule unataka, hivyo unaiacha. Hebu pata picha wewe ni kijana na unaenda kwa wazazi wako waliokusomesha na kuwaambia hii kazi ya ualimu niliyonayo kwa kweli hainifai, nimeamua kuacha na nifanye vitu vingine…. unaweza ukaachiwa hata laana. Hawawezi kukuelewa kabisa, kwa sababu wanajua wewe kuwa na ajira ya uhakika ndiyo maisha bora kwako na hata kwao pia.
Hivi ndivyo inavyokuwa kwa wenza, na hata marafiki zetu. Kila ukiwapa wazo lako la kuacha ajira, wanakuona labda utakuwa umechanganyikiwa. Inakuwa vigumu mno kuacha ajira wakati kila anayekuzunguka hakubaliani na wewe.

3.     Hofu ya kupoteza zile faida zinazotokana na ajira.
Kuna faida ambazo zinatokana na ajira, kiuhalisia huu pia ni uongo mwingine ambao umetumika kuwavutia watu kubaki kwenye ajira. Faida hizo ni kama bima ya afya, mafao ya uzeeni, fidia pale unapopata matatizo na kadhalika. Lakini hebu angalia kwa undani, bima ya afya si unakatwa mshahara wako? Mafao ya uzeeni je, si sehemu ya mshahara wako kukatwa? Lakini bado tunashawishika kwamba ajira ndiyo zinatupa vitu hivi.
Faida hizi zimekuwa zinatusaidia kwa sababu tumekosa nidhamu, ni vigumu sana mtu kujiwekea fedha ya dharura ambayo ataitumia pale yeye au mtu wake wa karibu atakapougua, hivyo kuwa na bima ya afya kunakuwa ni ahueni.
Pia ni vigumu sana mtu kujiwekea mwenyewe akiba ya uzeeni, hivyo mafao ya uzeeni kuonekana ni dili kubwa ndani ya ajira. Tusichimbe tu ndani zaidi kwenye mafao haya, maana nayo ni uongo mwingine ambao umekuwa unawafanya watu wabaki kwenye ajira. Niguse kidogo tu; angalia sakata linaloendelea kuhusu mafao, kwamba mtu hataweza kuchukua mafao yake mpaka afikishe miaka 60, hata kama ameacha kazi, ndiyo utajua mafao nayo siyo ya uhakika kama ulivyokuwa unafikiri.

4.     Hofu ya kutokuwa na uhakika na kule unakoenda.
Pamoja na ajira kuwa ngumu, lakini mtu anakuwa na kitu kimoja, kwamba ana uhakika wa kazi, na hata kama kipato ni kidogo, ana uhakika wa kukipata. Sasa mtu akifikiria kuacha hivi alivyonavyo sasa, na kwenda kufanya vile ambavyo hana uhakika navyo, hofu inamzuia kuchukua hatua. Na misemo yetu ya kiswahili, kwamba ni heri kidogo ulichonacho, kuliko kikubwa ambacho huna, basi tunashindwa kabisa kuchukua hatua.

5.     Kukosa mpango bora wa kutoka pale ulipo sasa.
Watu wengi ambao wamekwama kwenye ajira wamekuwa na fikra moja, kwamba ili waweze kutoka kwenye ajira na kujiajiri basi wanahitaji kuwa na mtaji mkubwa ili waanze biashara ambayo haitakufa. Hivyo wanajipa kazi ya kukusanya mtaji ili tuweze kuondoka kwenye ajira hizo. Lakini maisha nayo yanaendelea, changamoto hazikosekani. Hivyo ukikusanya na kufika kiasi fulani, mara kuna ndugu anaumwa inabidi utumie. Majukumu nayo yanaongezeka, gharama za maisha zinapanda, tunakuja kugundua kwamba zoezi hili la kukusanya mtaji ni gumu kuliko tulivyodhani.
Lakini uzuri ni kwamba matumaini hayakauki, kwamba kama tumeshindwa sasa, basi tusubiri mpaka tutakapostaafu, tutaweza kufanya yale tunayotaka kufanya. Na sababu tunajipa mbili; kwanza tutapata mafao, hivyo fedha haitakuwa tatizo, pili majukumu yatakuwa yamepungua, watoto wameshakua na kujitegemea hivyo ni sisi tu. Huu ni uongo mwingine ambao umepoteza maisha ya wengi.
Wapo ambao kweli wanafikia nafasi hiyo ya kustaafu na wanapewa mafao yao na kweli majukumu hawana lakini unajua nini kinatokea? Tafiti zinaonesha wengi hufariki ndani ya miaka mitano baada ya kustaafu kwao, tutalichambua hili kwa undani siku nyingine. Lakini ukweli ni kwamba mambo yamekuwa hayaendi kama watu wanavyokuwa wamepanga.

Ni hatua zipi ambazo mtu anapaswa kuchukua ili kuondoka kwenye mtego huu wa kushindwa kuondoka kwenye ajira?
Kwenye NYEUSI NA NYEUPE sikuachi hivi hivi, bali nakupa njia mbadala, hatua za kuchukua ili kutoka pale ulipokwama sasa. Na kama umezisoma sababu hizo za kuwa kwenye mkwamo, utakuwa umeanza kupata picha ni nini cha kufanya.
Zifuatazo ni hatua unazoweza kuanza kuchukua sasa ili kuondoka kwenye mkwamo wa kiajira.

1.     Badili kabisa mfumo wa mawazo na maisha yako.
Tukichukulia akili yako kama kompyuta, basi nitakuambia unatakiwa ku ‘format’ yaani kufuta kabisa zile fikra za kizamani na kuweka fikra mpya. Sahau kuhusu usalama wa ajira, sahau kuhusu faida za kwenye ajira. Anza kufikiria ni kipi unataka kwenye maisha yako na kama ajira uliyonayo sasa inakupatia au itakuwezesha kupata. Na ninaposema unachotaka siyo fedha pekee, bali hata kuridhishwa na kazi unayofanya, na kuipenda pia.
Unahitaji kuondoa fikra za zama zilizopita na kuweka fikra za zama hizi ambapo kuna taarifa nyingi ambazo unaweza kuzitumia kupata kile unachotaka kupata.
Waheshimu wale wanaokuzunguka, sikiliza maoni yako, lakini fanya maamuzi yako mwenyewe. Kumbuka kwamba ni wewe pekee utakayeyaishi maisha yako, hakuna mwingine anayeweza kukusaidia kuyaishi. Japokuwa wanakushauri na kukuonya mambo mengi, lakini bado wewe unahitaji kufanya maamuzi yako. Fanya maamuzi ambayo unajua unaweza kuishi nayo bila ya kujutia na siyo kufanya kwa sababu unataka kuwaridhisha wengine. Hivyo kama unachagua kuendelea na ajira yako, chagua ukijua ni jambo muhimu kwako, kama unachagua kuondoka, basi chagua ukijua utakuwa tayari kupambana na lolote utakalokutana nalo.
Ni kweli utawachukiza watu pale utakapochukua maamuzi ambayo hawakubaliani nayo, lakini baadaye watajifunza na kukuheshimu kwa maamuzi hayo.

2.     Anza kuchukua hatua ukiwa bado upo kwenye ajira yako.
Usiendelee kusubiri tena mpaka kila kitu kiwe sawa, uwe na mtaji wa kutosha ndiyo uondoke kwenye ajira na kwenda kufanya mambo mengine. Usisubiri tena mpaka ustaafu ndiyo uweze kuishi maisha ya ndoto yako. Badala yake anza sasa, anza wakati huu ukiwa bado upo kwenye ajira hiyo inayokusumbua. Na ninachoweza kukuambia ni kwamba unaweza kufanya chochote ukiwa bado upo kwenye ajira yako kwa sasa.
Kuhusu hili nimeandika kitabu kinaitwa BIASHARA NDANI YA AJIRA, ni kitabu ambacho kitakupa hatua kwa hatua namna unavyoweza kufanya biashara ukiwa bado umeajiriwa, pia kina mifano ya biashara ambazo unaweza kuanza kuzifanya ukiwa bado umeajiriwa. Nakushauri sana sana sana ukisome kitabu hiki, kitakupa mwanga mkubwa.
Kukipata kitabu hiki bonyeza maandishi haya na utapata maelekezo ya kukipata kitabu hiki. Nasisitiza tena, kisome, kitakusaidia sana.

3.     Shika hatamu ya maisha yako.
Kitu kimoja ambacho kinawafanya watu wabaki pale walipo, ni kuamini kwamba kuna watu wa kuja kuwatoa hapo walipo. Wanaamini maisha yao ni magumu kwa sababu waajiri wao wanawalipa kidogo, au serikali imewatelekeza. Sasa wewe achana na kundi hili la watu, shika hatamu ya maisha ya maisha yako.
Acha kabisa kitu kinaitwa kulalamika, kama kuna kitu hukipendi kibadili, na kama huwezi kukibadili achana nacho.
Naamini kwa pamoja tumeweza kuona ukweli halisi wa ugumu wa kuondoka kwenye ajira na hatua tunazoweza kuchukua ili kuondoka kwenye mtego huu. Sasa kazi ni moja, kufanyia kazi haya ambayo tumejifunza, ili maisha yetu yaweze kuwa bora sana.
Nakutakia kila la kheri rafiki katika kufanyia kazi haya uliyojifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)