Ili ufanikiwe, unahitaji kuwa mahali sahihi na kwa wakati sahihi, hii ni kauli ambayo tumekuwa tunaisikia kila siku. ni kauli yenye maana kubwa, lakini watu hawaichukulii kwa uzito wake. Watu huichukulia juu juu kwamba wanatakiwa kuwa sehemu sahihi na kwa wakati sahihi. Hivyo kama sasa hawafanikiwi, moja kwa moja wanachukulia kwamba hawapo mahali sahihi na huu siyo wakati wao sahihi.

Hapo ndipo changamoto zote zinapoanzia, hapo ndipo watu wanahama kazi baada ya kazi, wanajaribu kila aina ya biashara lakini mwisho wa siku wanajikuta wanarudi pale pale walipoanzia. Hii inazidi kuwachanganya na kujiona bado hawajaipata sehemu sahihi kwao.

Leo nataka utulie kwanza, kabla hujaanza kukimbilia hizo sehemu unazofikiri ni sahihi zaidi. Nataka ukae na kutafakari hili, kwamba hapo ulipo sasa, ndiyo sehemu sahihi kwako hasa kwa kuanzia. Na wakati ulionao sasa, ni wakati sahihi sana kwako kuanzia. Ukishaelewa hili rafiki yangu, na kulikubali kisha kuanza kulifanyia kazi, hakuna kitakachokukwamisha na hakuna atakayekurudisha nyuma.

Kwanza kabisa amua kwamba hapo ulipo ndiyo sehemu sahihi ya wewe kuanzia, hata kama ni chini kiasi gani, huwezi kuanzia sehemu nyingine zaidi ya hapo ulipo. Hata kama kuna sehemu nyingine unayotaka kufika, lazima uanzie hapo ulipo sasa. Hivyo angalia mazingira yanayokuzunguka hapo ulipo na namna unavyoweza kuyatumia kufika kule unakotaka kufika. Fungua macho yako sawasawa na utaona namna mambo mengi yanavyoweza kukusaidia kufika kule unakotaka kufika.

SOMA; ONGEA NA KOCHA; Tabia Moja Inayokuingiza Kwenye Matatizo Na Kukunyima Fursa Nyingi.

Na pili, huu ndiyo muda sahihi kwako, japo utapata sababu kwa nini uendelee kusubiri, lakini nakuambua sababu hizo siyo za kweli. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kwa nini usianze sasa. Chochote unachotaka kufanya, wakati wa kuanza ni sasa, hakuna siku utakayokuwa tayari zaidi ya ulivyo sasa. Chagua kuanzia hapo ulipo na chagua kuanza sasa.

Hata kama utapiga hatua moja kila siku, baada ya mwaka utakuwa mbali kuliko usingepiga hatua kabisa. Hivyo chukua hatua leo rafiki.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)