Vielelezo 10 Muhimu Vinavyomtambulisha Kijana Na Kutambua Thamani Yake Hapa Duniani.

Habari Mpendwa Rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini hujambo kabisa na karibu tena ndugu msomaji katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza. Kila mtu ana faida yake hapa duniani aidha kwa kujua au kwa kutokujua. Tupo tofauti ndio maana kila mtu ana kitu cha kipekee au ana hazina ya kipekee ambayo bado haijagunduliwa. Wewe ni zawadi kwa wewe mwenyewe lakini pia wewe ni zawadi kwa dunia. Huu ndio wakati sahihi kwako kutoa thamani iliyoko ndani yako. Kila mtu ana deni katika hii dunia, ambalo anapaswa kulipa kabla hajaondoka duniani. Kama una tabasamu ujue kuna mtu anahitaji tabasamu lako, kuna mtu anahitaji upendo wako ambao kama ukiutoa atafarijika katika maisha hivyo utakua umeongeza thamani katika maisha yake.

Hivyo ndugu msomaji, napenda kukukaribisha katika somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza vielelezo muhimu vinavyomtambulisha kijana na kutambua thamani yake hapa duniani. Karibu mpenzi msomaji tuanze kwa pamoja mpaka mwisho wa somo letu. Vifuatavyo ni vielelezo muhimu vinavyomtambulisha kijana na kutambua thamani yake katika hii dunia.

1. Usemi; wewe kama kijana unasema nini juu ya maisha yako na watu wengine? Unasema nini na kuchukua hatua gani pale mambo yako na jamii yako kwa ujumla yanapokwenda vibaya? Unapomwona mwenzako anaangamia na madawa ya kulevya unasema nini? Unapomwona mwenzako amekata tamaa ya maisha wewe kama kijana unasema nini? Unachukua hatua gani? Unampatia ushauri sahihi au na wewe unaendelea kumsukumiza shimoni ili aendelee kutokomea kabisa? Wewe kama kijana unatakiwa kusema na siyo kukaa kimya na kuacha watu wakiangamia kama kuna sehemu inahitajika kusema ukweli sema na siyo kukaa kimya.

2. Mwenendo; unatakiwa kuwa na mwenendo mzuri katika maisha yako na maisha ya watu wengine. Ebu jiulize mwenendo wa maisha yako uliyokuwa nayo sasa ni mwenendo sahihi katika maisha yako? Mwenendo wako ni mzuri au mbaya? Jina lako likitajwa katika jamii watu wanasikia nini kutoka kwako au wanajifunza mwenendo gani kutoka kwako? Mtu akigugo jina lako katika mtandao atajifunza mwenendo au tabia gani hasi au chanya? Kijana unatakiwa kuwa na mwenendo mzuri kwenye maisha yako na jamii kwa ujumla.

3. Upendo; unaishi katika falsafa ya upendo katika maisha yako? Je unajipenda wewe mwenyewe? Kama jibu ni ndio unawapenda na wengine je unapenda kile unachofanya? Wewe kama kijana unatumiaje falsafa ya ujana wako ambayo ni kipindi cha sasa ukoje katika kugusa maisha ya wengine? Hivyo upendo ni kielelezo kinachomtambulisha kijana na kugundua nini thamani yake hapa duniani.

 

4. Imani; maisha ni imani. Lazima uwe na imani na yale unayoyafanya. Lazima kama kijana uwe na imani na maisha yako. Uwe na imani thabiti ya maisha ya kiroho. Unatakiwa ukue katika Nyanja tatu katika maisha yako nazo ni kiroho, kimwili na kiakili. Vitu hivi vitatu vinategemeana kama mizani au mafiga kama vile tunavyojua mafiga yanafanya kazi vema na kwa ustadi kama yakiwa matatu hivyo ukiwa na figa moja huwezi kupika chakula kikaiva. Hivyo ni muhimu kuwa na imani katika maisha yako.

5. Usafi; kijana anapaswa kuwa kielelezo cha usafi na siyo uchafu. Kuna baadhi ya vijana ukikutana nao huwezi kukaa nao karibu kwa sababu wananuka jasho, nguo chafu, yaani wamechoka wamechakaa, wengine wananuka sigara, wengine wananuka pombe. Hivyo basi, tabia kama hizi huwa zinaathiri watu wengine. Kama wewe ni kijana unatakiwa kuwa msafi na nadhifu wa mwili wako. Unatakiwa kujitunza na kujithamini mwili wako ni ndio nyumba yako yaani mahali wewe unaishi usiruhusu kila mtu kuuchezea mwili wako jitunze na jithamini. Kula vizuri, fanya mazoezi, kiufupi kula mlo kamili na usiruhusu mwili wako kuwa kama siti ya daladala au taulo la nyumba ya wageni kila mtu anayekwenda analitumia. Kuwa msafi wa ndani na wa nje wa mwili wako. Mtu akikuangalia uonekane kweli kijana na siyo mzee. Kuwa nadhifu na maridadi kama kielelezo cha usafi.

6. Bidii; hakuna kitu kinachoweza kutokea katika maisha yako kama wewe mwenyewe huna bidii katika kitu hicho. Kama wewe ni mwanafunzi unasoma hakikisha unaweka bidii katika masomo yako. Kama wewe unafanya kazi weka bidii katika kazi yako unayofanya. Juhudi ni muhimu sana katika maisha yako, kwenye chochote unachofanya. Hakuna kitu kirahisi na ingekuwa rahisi kila mtu angefanya. Kuna usemi mmoja unasema hivi ‘’ heri uzee kuliko uzembe’’ kama huna bidii katika maisha yako wewe ni mzembe na wazembe hawahitajiki katika karne hii. 

Hivyo basi, bidii ni kielelezo tosha cha kijana mahali popote pale ambapo kijana yupo. Ukiwa eneo la kazi na wewe ni kijana jaribu kufanya kazi tofauti ongeza thamani na uoneshe tofauti kuwa kweli wewe ni kijana na siyo mzee. Uwe sehemu ya mabadiliko chanya mahali ulipo.

SOMA; Kama Wewe Ni Kijana Unayataka Mafanikio,..Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kuujua Ili Kufanikiwa.

7. Kusoma; kijana unatakiwa usome katika maisha yako siyo kukaa tu na kujishughulisha na mambo ambayo hayaongezi thamani katika maisha yako. Mwanafalsafa Jim Rohn aliwahi kusema kosa chakula lakini usikose kusoma kitabu. Je wewe kama kijana mara yako ya mwisho kusoma kitabu ni lini? Huenda hata ulivyokua shuleni, au chuoni hukujisumbua kusoma vitabu badala yake ulikuwa unatumia tu’ notes’ za mwalimu mpaka unamaliza. Kama wewe unaitwa kijana kuanzia leo anza kujifunza, anza kutafuta maarifa katika maisha yako kwani hujui ya kuwa maarifa ni chakula cha ubongo wako? Mbona wewe unakula kila siku halafu huilishi akili yako? Hujui ya kwamba unatakiwa kukua katika sehemu tatu yaani kiakili, kiroho na kimwili? Anza kusoma acha kutafuta sababu zisizokua na maana.

8. Onya; moja kielelezo cha kijana ni kuonya. Kama unaona watu wanafanya mambo na kwenda kinyume na maadili katika jamii unaonya? Huwezi kumuonya mtu juu ya jambo Fulani wakati na wewe ni mshirika wa mambo hayo. Chochote unachotaka kuonya hakikisha kwanza wewe uko vizuri. Unapomuonesha mwenzako kidole kimoja angalia vidole vingapi vinakurudia wewe? Tumia ujana wako kama kielelezo cha kuonya. Kama uko katika familia yako unaona kuna mtu anaenda kinyume mpe onyo lake kwa kumwambia ukweli yaani wewe onya wala usifunge macho. Kuwa mwaminifu katika maisha yako kwani uaminifu utakulipa.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Kijana Wa Kitanzania(kama una miaka kati 20 mpaka 30 soma hapa)

9. Kufundisha; hapa naongelea kwa kijana yoyote mwenye kipaji au karama Fulani katika maisha yake. Je wewe una kipaji? Kama una kipaji ulichopewa bure je na wewe unakitumiaje ili uweze kuwasaidia wengine? Kama una kipaji chako hakikisha unawafundisha wengine hicho kipaji chako. Hujui ya kwamba wewe ni zawadi kwa wewe mwenyewe na wewe ni zawadi kwa dunia nzima? Fundisha wenzako kile unachojua katika akili yako ambacho kitakua msaada kwa wengine. Kama una maarifa uliyoyapata darasani ni wakati wako sasa wa kufundisha dunia kile unachojua. Usiwe mchoyo au mbinafsi katika maisha yako kama una kitu cha msaada wafundishe wenzako kabla hujaondoka na zawadi uliyonayo. Una kipaji na karama ambayo bado hujaigundua na kuitoa duniani ninachokuomba usife na hazina uliyonayo itoe ili na wengine wajifunze.

10. Uadilifu, nidhamu na uaminifu; katika zama hizi za taarifa uadilifu, uaminifu na nidhamu umekua adimu sana. Uaminifu ni kutekeleza kile unachoahidi au kuwaambiwa watu. Kama unawaambia watu kuwa utawafanyia kitu Fulani hakikisha unatekeleza ahadi yako. Watu wamekosa uaminifu siku hizi hivyo unatakiwa umchunguze mtu kabla ya kufanya naye kitu fulani. 

Ukiwa na uaminifu utakulipa sehemu yoyote ile hata kama hujuani na mtu mtaweza kufanya kazi na mambo yakaenda vizuri. Pia unatakiwa kuwa mwadilifu yaani usimamie misingi uliyojiwekea katika maisha yako. Kama umeamua kuishi katika kusimamia ukweli basi simamia ukweli mpaka pumzi yako ya mwisho hapa duniani. Vile vile unatakiwa kua na nidhamu kwani nidhamu ni daraja la mafanikio katika maisha yako hivyo kuwa na nidhamu thabiti katika maisha yako.

SOMA; Ushauri Muhimu Kwa VIJANA, Okoa Miaka Hii Kumi Ambayo Utaipoteza.

Kwa kutamanisha, unatakiwa kudumu katika yote uliyojifunza leo. Kudumu maana yake ni kusimamia katika yote uliyoamua kufanya. Kama umeamua kusimamia ukweli basi dumu katika falsafa hiyo ya kusimamia ukweli. Kama wewe ni kijana usisubiri upewe ruhusa katika maisha kwani maisha ni muda na ni mafupi lakini ni marefu kama tu ukitumia muda wako vizuri hapa duniani. Unaweza kufanya na kwenda mbali zaidi kuliko mtu yeyote katika familia yako una uwezo mkubwa sana jaribu kuutumia leo.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: