Mwandishi na mwanafalsafa Ralph Waldo Emerson aliwahi kusema kila mtu atafikia hatua kwenye elimu yake ambapo atagundua WIVU NI UJINGA na KUIGA NI KUJIUA MWENYEWE. Na sina neno la ziada zaidi ya hayo maana ndiyo ukweli wa maisha.
WIVU NI UJINGA.
Ndiyo, hakuna namna nyingine tunayoweza kuusemea wivu zaidi ya ujinga. Tunawaonea wengine wivu pale wanapokuwa na vitu ambavyo sisi hatuna. Tunaona labda wao wamebahatisha, au wametumia njia zisizofaa kupata vitu hivyo. Lakini wote huu ni ujinga. Kama kuna mtu ambaye ana kitu wewe huna, maana yake amefanya vitu ambavyo wewe hufanyi. Siyo kwamba huwezi kufanya, bali umechagua kutokufanya, au hujui ya kwamba unaweza kufanya.
Hivyo badala ya kuwaonea watu hawa wivu, ingekuwa vyema kama tungeamua kujifunza kwao, tukajua mbinu zao wanazotumia kupata matokeo ambayo wanayapata na maisha yetu yakawa bora sana.
Wivu ni ujinga, usikubali ukuingie, unapoona mtu ana kitu ambacho huna, usianze kujipa sababu kwamba yeye ana bahati, badala yake jifunze kupitia yeye na utaweza kupata kile unachotaka kupata. Na wakati mwingine siyo lazima uwe na kila kitu ambacho wengine wanacho.
Na ujinga mwingine wa wivu ni kushindwa kuelewa kwamba hata kama una nini, kuna watu ambao bado watakuzidi. Huwezi kuwa na kila kitu na kuwazidi wengine wote.
KUIGA NI KUJIUA MWEYEWE.
Hili nimekuwa naliandikia na kusisitiza sana, usiige. Watu wamekuwa wanaiga kila kitu kwenye maisha yao na hivyo kujikuta wakiishi maisha ambayo hawayafurahii. Wamekuwa wakiangalia wengine wanafanya nini, na wao kutaka kufanya kama wao.
Hii ni kujiua wewe mwenyewe kwa sababu kila mtu ni wa pekee, hakuna watu wawili wanaofanana hapa duniani. Wewe ni wewe na upo hivyo ulivyo peke yako hapa duniani. Hakuna mtu ambaye anafanana na wewe kwa kila kitu. Hii ina maana kwamba kuna vitu vya pekee ambavyo unaweza kuvifanya wewe tu na siyo mtu mwingine yeyote. Kuna vitu ambavyo wewe unaweza kuvifanya kwa ubora kuliko watu wengine wote duniani.
Sasa unapoiga maisha ya wengine, maana yake unayaweka maisha yako pembeni. Kitu kibaya kabisa kinachotokea ni hutaweza kuwa bora kama wale unaowaiga, na wakati huo huo hutakuwa na ule ubora ambao upo ndani yako. Hivyo unakuwa umejiua wewe mwenyewe.
SOMA; BIASHARA LEO; Jinsi Ya Kukabiliana Na Anayekuiga Kwenye Biashara.
Epuka wivu na kuiga, hivi ni vitu ambavyo vitakupoteza kabisa kwenye safari yako ya mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK