Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha, ambapo tunapena maarifa sahihi ya jinsi ya kuishi maisha yetu, kwa ubora na furaha. Unaishi hivyo unavyoishi kutokana na falsafa ya maisha ambayo umeibeba. Tatizo la jamii zetu ni kwamba hatuchagui wenyewe falsafa ya kuendeshea maisha yetu, badala yake tunafanya kile ambacho kimezoeleka kufanya. Hivyo unakuta wengi hawayafurahii maisha yao. Ndiyo maana ni muhimu sana kila mmoja wetu kujijengea falsafa ya maisha yake.

Moja ya jukumu la falsafa kwenye maisha yetu ni kutuwezesha kuviona vitu jinsi ambavyo vipo, na siyo jinsi tunavyotaka kuona au tunavyoaminishwa kuona. Na nisikudanganye, hakuna kitu kigumu kwenye maisha kama hiki. Wengi tumekuwa hatuoni vitu kama vilivyo, bali tumekuwa tunaviona vitu kama ambavyo tunataka kuviona sisi wenyewe, au vile ambavyo wengine wanatuaminisha tuone. Kwa hali hii ukweli imekuwa ni kitu adimu sana kukipata au kukiona.

Leo nataka tuangalie dunia kwenye jicho la ukweli, na tuyaangalie maisha kama yalivyo na siyo kama tunavyotaka kuyaona. Ukweli ni kwamba kwa kuangalia unavyotaka kuona, dunia inaweza kuwa sehemu mbovu sana ya kuishi. Na ukifuatilia habari, utaona kama mwisho wa dunia ni kesho.

Msikilize mwanasiasa yeyote anayekushawishi ukubaliane naye, atakuonesha ni jinsi gani usipokubaliana naye basi maisha yatakuwa magumu mno. Pia msikilize mhubiri wa dini, atakuonesha ni namna gani usipokubaliana naye dunia itakuwa ngumu sana kwako.

Jaribu kuianza siku yako kwa kuangalia taarifa ya habari kwenye televisheni, au kusikiliza matukio kwenye redio, na utaona ni namna gani ambavyo dunia inaelekea mwisho kabisa. Utasikia huko Palestina kuna mtu kajilipua na bomu na kuwaua wengine, utasikia ISIS wameshambulia sehemu na kuua watu, utasikia Marekani mtu mweusi amepigwa risasi na askari. Ukija kwa habari za nyumbani utasikia mtu amemuua mweziye kwa ugomvi wa deni, mwingine amebaka, mwingine kajiua mwenyewe.

Ukishafuatilia habari hizi, ukawasikiliza wanasiasa halafu ukawasikiliza wahubiri wengine, utakosa matumaini kabisa kuhusu maisha ya hapa duniani.

Habari nyingi tunazopata kila siku nyingi ni habari hasi, hata kama kuna habari chanya, hazipewi kipaumbele, ila hasi ndiyo zinapewa kipaumbele.

Sasa leo kupitia makala hii ya falsafa mpya ya maisha, tunakwenda kuweka hizi kelele pembeni na kuujua ukweli wenyewe, hii itatusaidia kufanya maamuzi sahihi na kuendelea na maisha yetu vyema.

Nakumbuka siku bajeti ya mwaka huu imesomwa, kuna rafiki yangu mmoja alinipigia simu akiwa na hofu kubwa, akinieleza ni namna gani bajeti hii itatukomesha wananchi, tuliongea sana lakini mwishowe nikamwambia pamoja na yote, lakini lazia maisha yataenda. Hivyo unaweza kuchagua kuhofia bajeti hii kila siku, au ukaendelea na maisha.

Ukiangalia hali ya nchi kwa sasa, kutokana na mabadiliko yanayoendelea, wengi wamekuwa kwenye hali za hofu. Hivyo inapotokea habari yoyote hasi, inapewa kipaumbele na kuongezwa chumvi hata kuzidi uhalisia wake. Habari kama hizi zimekuwa zinawafanya watu waishi maisha yenye hofu na kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako.

Karibu kwenye msingi wetu mkuu wa falsafa.

Msingi mkuu wa falsafa ambao nimejifunza kwa wanafalsafa wengi walioishi hapa duniani, zaidi ya miaka 2000 iliyopita ni huu; HAKUNA JAMBO ZURI WALA BAYA LINALOTOKEA DUNIANI, BALI TAFSIRI YETU NDIYO INALIFANYA JAMBO KUWA ZURI AU BAYA. Ukiielewa falsafa hii, hutakuja kutetereshwa tena na habari yoyote hasi. Kwa sababu unakuwa umeelewa msingi halisi wa dunia.

Iko hivi, mambo yanatokea duniani kwa sababu yanatokea, ajali, maafa na mengine ya aina hiyo. Hakuna jambo zuri wala baya, ni kwamba mambo lazima yatokee. Tafsiri yetu sisi ndiyo inafanya mambo hayo kuwa mabaya au mazuri, ikiwa mambo yale yametokea kama tunavyotaka basi tunafurahi na kuona ni mazuri. Ikiwa yametokea tofauti na tulivyotaka basi tunachukia na kuona ni mabaya. Lakini dunia haijali kama tunachukia au tunafurahi, yenyewe inakwenda kwa asili yake.

Na hata tabia za watu wanaotuzunguka, siyo nzuri wala mbaya, bali tafsiri yetu kwenye tabia hizo. Kwa mfano mtoto mdogo anayejifunza kuongea akikuambia wewe ni mjinga, utakachofanya ni kumcheka na kuachana naye. Lakini mtu mzima mwenzako akikuambia wewe ni mjinga, utakasirika na kuona amekudharau na kukutukana. Sasa kuna tofauti gani hapo? Neno ni lile lile, lakini tafsiri yako ndiyo imekupa maana unayotaka wewe. Kwa nini utegemee mtu mzima akupe maneno mazuri, kwa nini usichukulie na yeye bado hajakua na kukomaa kisawasawa kiasi cha kuelewa kwamba maneno fulani siyo ya kupaswa kuongea mbele ya wengine? Kwa nini usimcheke na kuondoka zako? Unaanza kuona sasa ni nini namaanisha?

Sasa turudi kwenye hizi kelele zetu za maisha ya kila siku.

Kwanza kabisa, kwa namna yoyote ile, usiangalie habari kupitia tv, au kusikiliza kwenye redio. Kwa sababu hivi ni vyombo vitakavyokuonesha mambo hasi kwa lazima, wataanza na zile bahari za kusisimua ili kushika hisia zako, wakati unasubiri habari inayoweza kuwa nzuri kwako. Ni bora ukapata habari kwenye magazeti au mitandao, ambapo unaweza kuchagua zile habari unazotaka tu, labda za biashara au michezo. Zile habari za ukurasa wa mbele usizisome kabisa, zimewekwa chumvi nyingi kuliko uhalisia ulivyo.

Pili unapopata habari yoyote, iwe hasi au chanya, usikimbilie kuibeba kama ilivyo, na wala usikubali ikupe hofu, badala yake anza kuhoji kuhusu habari hiyo. Sawa kuna mtu kajinyonga huko newala, hiyo inaathiri vipi maisha yako ya kila siku? ndiyo kuna mtu mmoja kamuua mwenzake kwa kumchoma kisu, lakini kuna watu wengi siku hiyo hiyo wamewaokoa watu wasife, hutasikia habari zao. Utapata habari kuna daktari kakosea matibabu na kuua mgonjwa, lakini siku hiyo hiyo kuna madaktari wamekesha wakikazana kuokoa maisha ya watu, hutasikia habari zao.

Ichambue kila habari unayoipokea na iweke sehemu yake, usimeze kila kitu na kwa namna yoyote ile, usiingiwe hofu kutokana na habari uliyoipata.

Tatu; usiwe mtu wa kusambaza habari yoyote unayoipokea ambayo hujaidhibitisha wewe mwenyewe. Maana hakuna kinachochochea moto habari hasi kama watu kusambaza kile walichosikia.

Nimalize kwa kusema kwamba, kadiri siku zinavyokwenda, dunia inazidi kuwa sehemu salama mno ya kuishi, na maisha ya watu yanazidi kuwa bora. Ila kuna watu wenye ajenda zao binafsi, wanatumia matukio hasi machache ambayo yanatokea, na lazima yatokee, kuwapa watu hofu ili kutimiza matakwa yao. Mfano mwanasiasa atakupa hofu ili umchague, chombo cha habari kitakupa hofu ili ununue taarifa yao, au ukodoe macho yako wakuoneshe matangazo na wao walipwe. Kila unapoona watu wanashabikia habari hasi, jua kuna watu wananufaika kwa hali hiyo. Usikubali kuwa mteja wa kizembe wa habari hizi hasi.

Tujikumbushe hili kila siku, mambo yanatokea na mambo yatatokea, siyo mazuri wala mabaya, bali tafsiri zetu ndiyo zinayafanya kuwa mazuri au mabaya.

Kila la Kheri mwanafalsafa mwenzangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK