Unaweza kuchagua uvae viatu vya aina gani, kwa sababu unaweza kuwa na aina tofauti za viatu. Unaweza kuchagua ni chakula cha aina gani ule, kwa sababu kuna vyakula vingi unavyoweza kuchagua.

Lakini inapokuja kwenye maisha yetu, huwezi kuchagua maisha mengine zaidi ya hayo uliyonayo sasa. Huwezi kusema unabadili maisha na kuchukua mengine kwa sababu hayo uliyopewa siyo bora kama ulivyotaka.

Unayabadili maisha kwa kubadili namna unavyoyachukulia na kubadili jinsi unavyofanya mambo yako. Na siyo kwa kutaka upewe maisha mengine kwa sababu hayo uliyonayo siyo bora.

Kwa maisha uliyonayo sasa, unaweza kuchagua moja kati ya haya mawili;

Unaweza kuchagua kuwa na maisha ya hofu, kutokuwa na uhakika na kuiona kila siku inayokuja afadhali ya jana. Unakosa matumaini na kukubali hakuna namna ya kuweza kutoka hapo ulipo sasa.

Au unaweza kuchagua kuyapokea maisha kama yalivyo, na kuyafanyia kazi ili kuwa bora zaidi. Kuonesha ule uwezo mkubwa na wa kipekee ulipo ndani yako, kuwa tayari kujaribu zaidi hata pale unaposhindwa, na pia kuwa na matumaini kwamba kesho itakuwa bora kuliko leo.

SOMA; Usidharau Ushindi Mdogo Mdogo Unaoupata Kila Siku, Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako, SEHEMU YA PILI.

Haya ni maamuzi ambayo unapaswa kuyafanya wewe mwenyewe kwenye maisha yako, kwa sababu wewe ndiye utakayeyaishi maisha yako, hakuna mwingine anayeweza kukusaidia kwenye jukumu hilo.

Maisha bora hayatashushwa kwako, wala hakuna unakoweza kwenda kuyabadili maisha yako. Bali maisha bora yanaanza na wewe mwenyewe, kwa namna utakavyochagua kuyachukulia maisha, na hatua unazochukua kila siku. nguvu zote zipo mikononi mwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK