Habari rafiki yangu?
Karibu kwenye safu yetu ya makala za NYEUSI NA NYEUPE zinazokujia kupitia mtandao huu wa AMKA MTANZANIA. Kupitia makala hizi tunalichambua jambo kwa kina ili kujua ukweli na uongo wake uko wapi. Kisha mwishoni tunashauriana namna bora ya kuliendea jambo hilo au maamuzi bora ya kufanya.

Leo tunakwenda kuangalia kwa kina kuhusu michango ya sherehe ambao ni utaratibu uliojenga mizizi kwenye jamii zetu. Ni jambo ambalo limekuwa na unafiki mwingi sana, kila utakayekutana naye analalamikia michango hii kuwa mingi, lakini bado watu wanaendelea kutoa michango hii. Je ni nini kimejificha hapa, ni ukweli upi na uongo upi ambao hatujaujua bado? Karibu tujifunze kwa pamoja leo

Kuhusu michango ya sherehe.
Ni utaratibu wa kawaida kwenye jamii zetu ambapo pale mtu anapofanya sherehe, anawaomba watu wamsaidie kuchangia gharama za sherehe hiyo. Na kwa kuwa ni jambo zuri, basi watu wamekuwa wakitoa michango yao na baadaye kuhudhuria sherehe hiyo.

Sina hakika sana kama michango hii imekuwa asili yetu tangu zamani au tumeiga. Kwa sababu kwa kabila na kijiji nilichotokea mimi, zamani sikuwahi kuona watu wakichangishwa fedha kwa ajili ya sherehe. Sherehe nyingi zilikuwa zinafanyika majumbani na mwaliko ulikuwa kwa wote. Kitu ambacho nilikuwa naona ni watu kusaidia kile wanachoweza. Kwa mfano kama mtu ana viti basi anaazimwa, mwenye sufuria kubwa za kupikia na sahani za kulia anaazimwa, mwenye ujuzi wa kupika basi alijitolea kupika kwenye sherehe hizi. Na hata mwenye ndizi na aina nyingine za vyakula alijitolea ili sherehe iweze kwenda vizuri.

Lakini tangu sherehe zimeanza kufanyika kwenye kumbi kubwa za kisherehe, na vyakula kuanza kupikwa na wapishi wa kitaalamu, na vinywaji kuwa vya kisasa na siyo vya kienyeji, gharama za sherehe zimekuwa zinapanda kila mwaka. Kila mwaka kiwango cha kuchangia kwenye shere kimekuwa kinaongezeka. Na hata aina ya uchangishaji nayo pia imebadilika. Zamani mtu alikuwa anaweza kutoa kiwango chochote, kadiri ya uwezo wake na akahudhuria sherehe hiyo. Kitu ambacho ni chema sana, unakwenda kuwashuhudia watu wako wa karibu kwenye sherehe yao muhimu, na kuwaunga mkono pia. Lakini miaka ya hivi karibuni kumekuwa na utaratibu wa kupangiwa kiwango cha kutoa, kwamba ukitoa chini ya kiwango fulani hupewi kadi ya kuhudhuria sherehe hiyo, bali utapewa asante tu. Yaani unaombwa mchango, halafu unalazimishwa ni kiwango kipi lazima uchangie.

SOMA;Hizi Ndio Aina Tano Za Dharura Za Kifedha(Angalizo; Michango Ya Sherehe Sio Mojawapo)

Aina za sherehe ambazo zinachangiwa pia imekuwa inabadilika karibu siku zinakwenda. Zamani tulizoea harusi pekee ndiyo zinachangiwa, kwa sababu ilionekana ni tukio kubwa. Lakini sasa hivi mpaka kipaimara watu wanachangishwa, mahafali watu wanachangishwa, na imeenda mbali mpaka kusherekea tarehe ya kuzaliwa pia watu wanachangishwa.
Sipati picha siku zijazo michango hii itafika mpaka wapi.

Kwa nini michango ya sherehe.
Zamani lengo la michango hii ilikuwa kuwaunga mkono ndugu jamaa na marafiki zetu pale ambapo wanafanya sherehe ya jambo muhimu kwa maisha yao. Hivyo tunaungana nao kwa kuwapa kile ambacho kipo ndani ya uwezo wetu, ili kuwawezesha kutimiza lengo lao. Ilikuwa ni hali ambayo watu wanajitoa kweli kweli, na wala hawalalamiki kuhusu mzigo wa michango hiyo. Au kuhoji kama wamepata huduma sawa na michango yao.
Lakini sasa hivi hatujui tena hata michango hii ya sherehe lengo lake hasa ni nini. Kwa sababu michango inakuwa mikubwa na hata utoaji wake umekuwa wa kulazimishwa zaidi kuliko hiari ya mtu mwenyewe.

Wapo ambao wanataka kufanya sherehe kubwa ili waonekane nao wamefanya sherehe kubwa, waweze kupata vipindi kwenye tv na iwe gumzo. Wapo ambao wanataka wapete kianzio cha maisha kupitia michango hiyo ya sherehe, ambapo linatengwa fungu la zawadi, hasa kwenye sherehe za harusi. Yapo malengo mengine mengi.

Kuna lengo moja ambalo hutasikia likisemwa popote, lakini watu wamelibeba kwenye mioyo yao. Watu wanachangisha watu kwenye sherehe kwa sababu na wao waliwachangia. Hili ni zito na hakuna atakayesema wazi, lakini wengi wanasukumwa na hili, mtu anachangisha watu kwa sababu ameshachangia sana wengine. Rafiki yangu mmoja amewahi kuwaambia wazazi wake kwamba hatafanya sherehe kubwa hivyo hahitaji kukusanya michango ya wengine, wazazi wake hawakukubaliana na yeye, kwa sababu wao wameshawachangia sana wengine, ni zamu yao na wao wachangishe wengine. Linaweza kuwa wazo zuri, nilichanga kwa wengine na sasa ni wakati wangu kuchangiwa, lakini wanasahau kwamba wanamweka kijana wao kwenye mzigo wa maisha yake yote, kwa sababu ukishachangiwa, huna namna utachangia wengine maisha yako yote.

Sababu nyingine inayoweza kuwa ya ukweli au uongo ambayo watu wanatumia ni kwamba ni heshima kutoa mchango wa sherehe. Eti kwamba kama utaandaa sherehe yako kwa gharama zako mwenyewe, halafu ukawaalika watu, wataona kama ni dharau, watu wanapenda kuchangia, inawapa heshima. Sitasema mengi hapo, inaweza kuwa ukweli au inaweza kuwa uongo, kulingana na mazingira uliyopo. Lakini kwa ujumla ni uongo.

Kwa nini unafiki kwenye michango hii ya sherehe?
Kutokana na uzito huu ambao michango ya sherehe imekuwa inapewa kila siku, watu wamekuwa wanailalamikia mno. Unakuta mtu ana kadi zaidi ya kumi kwa mwaka, ambapo akipiga mahesabu kwenye kadi hizo ni fedha kubwa mno kwake. Analalamikia hilo lakini analazimika kuchangia kwa sababu hana namna ya kukwepa. Hapa ndipo unafiki mkubwa unapoanzia.

SOMA; KAMA UNASHANGAA ‘BIG RESULT NOW’ HUJAYAANGALIA MAISHA YAKO VIZURI.

Sasa tuangalie NYEUSI na NYEUPE za kwa nini watu wanalazimika kuchangia japo haitoki ndani ya mioyo yao.

1.     Kuwa sehemu ya jamii.
Watu wengi wamekuwa wanalazimika kuchangia michango hii ili na wao kuwa sehemu ya jamii. Wanaogopa wasipochangia basi wataonekana wa tofauti kwenye jamii hivyo wanakazana kuchanga ili nao wawe sehemu ya jamii. Jamii ni kifungo cha watu kwenye mambo mengi, watu wanalazimika kufanya vitu siyo kwa sababu wanapenda, ila kwa kuwa kila mtu anafanya.

2.     Mategemeo ya kuchangiwa mbeleni.
Hili pia limekuwa linawafanya watu wachangie, kwa sababu wanatarajia mbeleni na wao wataomba kuchangiwa. Niliwahi kuongea na mtu fulani ambaye alikuwa analalamika michango mingi, nikamwambia kwani ni lazima uchangie? Akaniambia nina watoto wengi ambao sasa wameshakuwa vijana, wakianza kuoa na kuolewa nani atanichangia? Hivyo watu wanajiingiza kwenye kifungo ili na wao wachangishe watu baadaye.

3.     Kwa sababu tayari wao wameshachangiwa.
Yaani ukiangalia haya yote yanakwenda pamoja, na yote yanamfunga mtu kwenye mzunguko huu wa michango. Kama tayari ulichangiwa kwenye sherehe yako, utamkataliaje mtu anayekuletea kadi yake ya mchango, na unajua kabisa alikupa mchango wakati wa sherehe yako? Hiki ni kifungo ambacho wengi wamenasa huko.
Hizi ni sababu kuu ambazo zinawafanya watu kuwa wanafiki kwenye michango ya sherehe, wanachangia lakini wanakuwa na malalamiko na manung’uniko makubwa kuhusu michango wanayotoa.

Kama ilivyo kwenye kipengele hiki cha NYEUSI NA NYEUPE, sikuachi bila ya hatua za kuchukua. Sasa tuangalie hatua za kuchukua ili kuondokana na unafiki huu wa michango ya harusi.

1.     Chagua ni watu gani ambao utawachangia, weka vigezo.
Achana na sababu ya kijamii ambayo inawaweka watu wengi kwenye kifungo, wewe chagua ni watu gani ambao utakuwa tayari kuwachangia kadiri ya uwezo wako bila a kuwa na manung’uniko kwenye nafsi yako. Weka vigezo vyako vya kuchagua aina hiyo ya watu utakaowachangia, labda familia na ndugu wa karibu, marafiki wa karibu na watu wengine ambao wanapokuambia kuhusu sherehe zao, moja kwa moja unasukumwa kuwachangia na siyo mpaka ulazimishwe. Ukishakuwa na aina hii ya watu, wengine hata usifikirie mara mbili, usichangie.
Yaani kwa kifupi ni hivi, kama unapata malalamiko kwenye nafsi yako pale mtu anapokupa kadi yake ya mchango, basi usichangie.

2.     Kama tayari ulishawachangisha wengine.
Hapa tayari umeshajiweka kwenye kifungo, kama uliwachangisha wengine, na wao wanategemea wewe uwachangie. Na bora ingekuwa wanategemea uwachangie kwenye sherehe zao tu, mbaya ni kwamba watategemea uchangie hata kwenye sherehe za watu wao wa karibu. Hivyo hapo kunakuwa hakuna mpaka.
Unachoweza kufanya hapa ni kuweka mpaka, unawajua walikuchangia, basi wachangie wao wanapokuwa na shughuli inayowahusu wao moja kwa moja, nje ya hapo usichangie. Ukiweka kigezo hiki taratibu utajiondoa kwenye kifungo ambacho tayari umeshaingia.

SOMA; USHAURI; Kuendelea Na Masomo, Kuoa Au Kujenga, Kipi Bora Kufanya Kwanza?

3.     Kamwe, kamwe, kamwe, usiwachangishe watu kwenye sherehe yako.
Kama bado hujawachangisha watu, usiwachangishe, haya ni maamuzi bora kabisa unaweza kufanya kwenye maisha yako. Usijali wazazi, ndugu, jamaa na hata marafiki wanasema nini, usichangishe kabisa. Badala yake andaa sherehe inayoendana na uwezo wako na igharamie wewe mwenyewe, au na familia yako. 
Lakini siyo kuanza kuhangaika na kila mtu akuchangie.
Na kingine muhimu sana, usije kwa namna yoyote ile kuchukua mkopo kwa ajili ya kufanya sherehe, yaani hata ushawishike kiasi gani, usije kufanya jambo hilo hata kidogo. Ni afadhali usifanye sherehe kabisa kuliko kuifanya kwa fedha za kukopa.

Hili ni shimo ambalo nimekuwa naona watu wanajipeleka wenyewe, wanapopanga sherehe, wanatengeneza bajeti kubwa na kutegemea watu watachangia. Sherehe inapokaribia, watu wanakuwa hawajatoa michango ya kutosha bajeti ile, hivyo wanachofanya ni kuchukua mkopo kuhakikisha sherehe inafanyika kama ilivyopangwa. Hapo mtu anakuwa amejiingiza kwenye mashimo mawili, shimo la kwanza michango, shimo la pili mkopo.

Unafiki huu wa michango ya sherehe umekuwa ni wa pande zote mbili, kwa wanaochanga na wanaochangisha. Umefika wakati sasa kujiondoa kwenye vifungo hivi na kuishi maisha ya uhuru. Kwa sababu wengi wanaendelea na hili siyo kwa sababu wanapenda, bali kwa sababu hawajui jinsi gani ya kutoka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK