Umewahi kwenda kwenye biashara fulani kupata mahitaji yako lakini ukatoka pale ukiwa unajisikia vibaya na hutamani kurudi tena pale? Vipi kwa upande wa pili, ulishawahi kwenda kwenye biashara fulani na ukajisikia vizuri sana, ukatamani kurudi tena na kila unayekutana naye unamweleza kuhusu biashara ile?
Naamini umeshakutana na hali hii mara nyingi mno. Sasa ni wakati wa kuitumia hali hiyo kwenye biashara yako mwenyewe, na hata kazi yako mwenyewe.

Unakumbuka ni kitu gani kilikufanya ujisikie vizuri kwenye biashara moja na kujisikia vibaya kwenye biashara nyingine? Hii ndiyo zawadi unapaswa kuijua na kuweza kuitoa kwa wateja wako ili nao wajisikie vizuri na waendelee kuja kwenye biashara yako.

Zawadi unayoweza kumpa mteja wako na akafurahia sana kufika kwenye biashara yako ni kumfanya kuwa shujaa. Kila mtu anapenda ushujaa, hivyo unapomfanya mteja kuwa shujaa, kupitia bidhaa au huduma unayompatia, atajisikia vizuri na atapenda kuja tena kwenye biashara yako.

SOMA; Njia bora za kutatua hali ya kutoelewana baina yako na mteja wako.

Swali ni je unamfanyaje mteja wako kuwa shujaa?

  1. Mpatie bidhaa au huduma ambayo inatatua changamoto zake na kutimiza mahitaji yake.
  2. Mfanye ajisikie ufahari kupata kile ambacho unamuuzia, kiwe cha kipekee ambacho hawezi kupata mahali pengine popote.
  3. Kuwa tayari kusaidia pale anapokutana na changamoto kutokana na matumizi ya bidhaa au huduma unayomuuzia.
  4. Tengeneza hadithi ambayo itamfanya mteja aone namna gani anafanya maamuzi bora kwa kufanya biashara na wewe.
  5. Timiza unachoahidi, na nenda hatua ya ziada. Mshangaze mteja, mpe vitu ambavyo hajazoea kupata.

Kila mtu kuna siri moja kubwa ameibeba kwenye nafsi yake, siri hiyo ni kupenda kuonekana wa muhimu. Kwa dunia ya sasa ambapo kila kitu ni mwendo kasi, hakuna mwenye muda wa kumfanya mwingine ajione muhimu. Sasa kama wewe utachukua hatua hii, utajijengea nafasi ya kipekee kwenye biashara yako.

Mfanye mteja wako kuwa muhimu sana leo, mfanye kuwa shujaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK