Habari mpendwa Rafiki na Msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vizuri licha ya kukumbana na changamoto za hapa na pale kwenye shughuli zako za kila siku. Usikatishwe tamaa na changamoto ishi maisha ya furaha na hamasa kubwa ya kufanya kazi kila siku. Kwani mpendwa rafiki, hujui ya kuwa changamoto ni sehemu ya maisha? Na maisha ni furaha anza kuwa na furaha hapo hapo ulipo kwani kuwa na furaha haihitaji wewe uwe na mtaji na kitu cha ajabu na cha kushangaza duniani hakuna duka linalouza furaha hapa duniani. Hivyo basi, mkurugenzi mtendaji wa furaha katika maisha yako ni WEWE mwenyewe.

Mpendwa Rafiki, karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza kwa pamoja faida ya kutumia falsafa ya imani ya dini kwenye malezi ya watoto. Karibu mpendwa msomaji, tuanze pamoja na tumalize pamoja. Natumaini kila mmoja wetu ana imani yake ya dini ambayo anaiamini hivyo basi, hakuna imani ya dini inayofundisha maadili mabaya kwa watoto yaani kufundisha mambo hasi yanayomharibu mtoto na kumpotezea dira ya maisha. Kwanza kabisa watoto wote ili waweze kuwa na msingi mzuri wa kiimani ni lazima wafundishwe kumjua Mungu aliyeumba vitu vyote hapa duniani vinavyoonekana na visivyoonekana.

Wazazi kama walimu wa kwanza kwenye malezi ya watoto wao ndio wakurugenzi watendaji wa kuhakikisha watoto wanakua katika malezi mazuri ya kuishi na kujua misingi na falsafa ya dini yao. Wazazi wengi sasa hivi wanaona ni fahari kubwa kumlea mtoto kidunia kuliko kuwafundisha watoto kumjua Mungu na kuwalea katika maadili ya falsafa ya imani ya dini. Kumlea mtoto kidunia kuna hasara kubwa kwani msingi mzuri wa jamii yetu ya leo unaanzia katika familia. Ili 
tuweze kuwa na jamii bora hatuna budi kuwalea watoto katika maadili mazuri hususani ya falsafa ya imani ya dini.Mpendwa rafiki, watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kusamehe na siyo kulipa visasi. Wazazi ndio maadui namba moja wa kuwafundisha watoto kulipa visasi badala ya msamaha. Kwa mfano, mtoto anaweza kugombana na mwenzake katika kucheza sasa mmoja wao akalia na miongoni mwa watoto wa wazazi hao anaenda kumwambia mwanangu tema mate hapa puuh! Tukamrushie kwa nini akupige. Kwa hiyo, mzazi badala ya kuchunguza kiini cha kosa na kuwapatanisha upya kwa kuwaambia wasameheane bali mzazi anamfundisha mtoto kurudisha kisasi. Ukimfundisha mtoto kulipa kisasi utazaa mauti. Mfundishe mtoto kuomba msamaha angali yuko mdogo kwani msamaha unarudisha uhusiano uliovunjika na kuleta uhusiano ulio kuwepo hapo awali. Haya yanakuwa ndio malezi mazuri ambayo falsafa ya dini hairuhusu kulipa visasi.

Watoto wanatakiwa kufundishwa upendo, upendo ndio falsafa kubwa kuliko falsafa zote, kwani upendo unagusa kila sehemu ya maisha yetu. Kama ukimpenda mwenzako huwezi kumfanyia ubaya ambao wewe hupendi kufanyiwa. Upendo huvumilia yote, upendo unaleta maisha ya amani na furaha. Unaleta maendeleo lakini chuki huzaa mauti tu. Kwa hiyo, ukimfundisha mtoto upendo unaohubiriwa katika falsafa ya imani ya dini basi tutakua tunafanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi kwa kila mmoja wetu. Mfundishe mtoto kuwapenda wenzake na watu wote wanaomzunguka.

Ndugu msomaji, mfundishe mtoto asiwe mbinafsi au mchoyo, maisha ya ubinafsi na uchoyo yametawala katika familia zetu. Hili tunaliona sana katika familia zetu unakuta baba mbinafsi, mama mbinafsi mtoto naye anaambukizwa ubinafsi ambao unakuja kuathiri jamii kwa ujumla. Ukimpa mtoto kitu mfundishe ampatie ndugu au rafiki yake n.k. kwa mfano, watoto wengine unaweza kuwapatia zawadi au kitu unawaambia wagawie na wengine au wenzako anaanza kulia na kutikisa mabega na kujitupa chini. Ukimuona mtoto anaanza tabia hiyo ikomeshe mara moja kabisa usipomkomesha unakua unaandaa bomu ambalo litakuja kukulipukia mwenyewe kama mzazi. Hatuwezi kuwa na kizazi kizuri kama tutawalea watoto katika ubinafsi na uchoyo. Wazazi mnatakiwa kuacha kuishi maisha ya ubinafsi na uchoyo na muanze na kuonesha mfano kwanza nyie na mtumie falsafa ya dini katika kupata malezi bora.

Kama wazazi mnatakiwa kurudi katika falsafa ya dini na kuwalea watoto kwenye misingi hiyo. Acha kukumbatia mambo ya kidunia na kupiga teke misingi ya dini kwenye malezi ya mtoto. Acha ile dhana ya kwenda na wakati na dunia katika malezi ya watoto na watoto wengi wanakuwa hawana hofu ya Mungu ndio maana baadaye wanakua wakatili, wanakosa uadilifu, nidhamu, uaminifu. Ukimlea mtoto katika misingi ya kumjua Mungu Naye Mungu atakubariki pia. Mlee mtoto katika imani thabiti aelewe vizuri imani siyo kuichukulia juu juu, hata wewe mzazi soma maandiko mbalimbali kuhusiana na imani yako mfundishe mtoto imani, siyo kupandikiza chuki tu.

SOMA; Hii Ndiyo Faida Ya Kupanda Mbegu Bora Kwa Wasaidizi Wako Wa K

Mzazi unapaswa kuonesha mfano, kwa watoto wako kama ni kusali basi mfundishe kusali, salini pamoja na nendeni pamoja kwenye nyumba za ibada. Usiwe mzazi wa kutoa amri tu bali kuwa mzazi wa kuonyesha mfano siyo amri tu. Kila unachosema kiendane na matendo yako. Usimfundishe mtoto tabia mbaya kama wewe ni mlevi basi usinywe pombe mbele ya watoto. Kama wewe ni mvutaji sigara usimuoneshe mtoto mfano mbaya mbele yake. Kazi ya mtoto iko katika malezi ndio maana wa swahili wanasema, kuzaa siyo kazi, kazi kumlea mwana. Mtoto ni malezi ndugu yangu ukimpatia mtoto malezi bora utampa mwanga katika maisha yake.
Mpe mtoto malezi bora ambayo hataweza kuyapata sehemu nyingine yoyote. Kama katika familia yenu hakuna aliyewahi kupewa malezi bora basi kuwa wa kwanza kumpatia mtoto malezi bora. Yaani toa thamani yako yote ya malezi bora ambayo hakuna mtu aliyewahi kupatiwa katika familia yenu.

SOMA; Adhabu Saba (7) Zisizostahili Katika Malezi Ya Watoto.

Hivyo , dini inafundisha upendo, unyenyekevu, uadilifu, uaminifu, nidhamu nzuri, kufanya kazi n.k. Dini haifundishi wizi kwa watoto, uchoyo, uchochezi, matusi, ubakaji, ulevi wa kupindukia nk. Bali dini inafundisha mtu ukweli, kuna falsafa ya ukweli inasema hivi ukiujua ukweli nao ukweli utakuweka huru. Ni kweli kabisa kama ukijua ukweli utakuweka huru katika maisha yako. Tunalelewa katika malezi ya nidhamu ya woga haya kwa sasa hayana nafasi tena. Mwambie mtoto ukweli ili uweze kumweka huru.

Mwambie ule usemi wa soma kwa bidii, pata alama nzuri utapata kazi sasa umepitwa na wakati. Mwambie dunia imebadilika ajira zimekuwa siyo za uhakika kama ilivyokua zama za mapinduzi ya viwanda na mwambie kwa sasa tupo zama za taarifa ili ufanikiwe unahitaji taarifa sahihi kwa wakati sahihi. Dunia ya sasa unatakiwa kufikiria nje ya ajira, mfundishe ukweli wote unaoujua bila kumficha naye atakushukuru.

Kwa kuhitimisha, mfundishe mtoto akue kiimani, akue kiroho, usimlee mtoto kidunia kwani hasara zaidi ni kwako binafsi na kwa jamii kiujumla. Mfundishe mtoto kuvua samaki na siyo kumpa samaki yaani mjengee msingi imara wa kujitegemea angali akiwa mtoto, mfundishe kufanya kazi na yale mambo chanya yote yanayopatikana kupitia falsafa ya imani ya dini.

SOMA; Njia Muhimu Za Kumfanya Mtoto Wako Ajione Wa Pekee.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com