Kitu ambacho najifunza kila siku ni aina tofauti za watu ambao tunahitaji kuchanganyika nao kila siku kwenye shughuli zetu. Katika aina hizi za tofauti, watu wana tabia za tofauti, na mitazamo ya tofauti.
Kuna watu ambao wana mtizamo wa kukataa kila kitu ambacho wao hawawezi au hawajui. Yaani watu hawa wanaamini kwamba kama kitu hawakiwezi wao au hawakijui wao basi hakuna mwingine anayeweza au kujua.
Sasa hapa ndipo ubishani mkubwa unapoanzia baadhi ya watu, unajikuta wewe unajua na una uhakika na unachojua, ila kuna ambaye hajui na ana uhakika unachosema hakipo. Unaweza kutumia nguvu kubwa mno kumwelewesha, ukiamini ataelewa, lakini anabaki na msimamo wako ule ule.
Hapa ndipo watu wamekuwa wanapoteza nguvu nyingi na muda wao ambao wangeweza kuutumia kufanya mambo ya msingi zaidi. na leo rafiki yangu nataka nikusaidie kuokoa muda na nguvu zako, ambazo ni rasilimali muhimu kwa mafanikio yako.
Unapokutana na mtu wa aina hii, ambaye anakataa kabisa jambo unalojua ni sahihi, usipoteze muda wala nguvu zako, acha na yeye mwenyewe atakuja kuona matokeo.
Huhitaji kukesha usiku mzima ukijaribu kumshawishi mtu kwamba kesho jua litachomoza mashariki, badala yake unaweza kupumzika na kulala na asubuhi mtu akaona mwenyewe jua linachomozea wapi.
Ukielewa msingi huu mmoja, utapunguza sana mabishano na watu, mara zote pendelea kuwaacha watu waone wenyewe. Kwa sababu unaweza kupiga kelele mno, lakini wasikuelewe, ila wakiona watachagua wenyewe kukubali au kukataa.
Kumbuka siyo jukumu la kila mtu kukubaliana na wewe, na wala siyo jukumu lako kuhakikisha kila mtu anakubaliana na wewe, fanya kile ambacho ni sahihi na watu sahihi wataona kile ambacho ni sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK