Kila kitu kina gharama, namaanisha kila kitu. Hakuna na wala hakujawahi kutokea kitu cha bure, kila kitu kina gharama, tofauti ni kwamba kuna gharama ziko wazi na kuna gharama ambazo zimefichwa.

Kila kitu kina gharama kwa sababu hakuna kitu kinachotokea chenyewe. Lazima watu waweke juhudi, wakati mwingine waumie ili kuweza kutoa kile ambacho watu wanahitaji. Hiyo yote inaleta gharama kwenye kitu chochote kile.

Sasa unaposikia kitu ni bure, au ni bei rahisi, kabla hujakimbilia jiulize ni gharama ipi ambayo imefichwa, wewe huwezi kuiona lakini ipo? Na kama haipo gharama iliyofichwa, jiulize je ni nani anayelipa gharama hiyo?

Hii ni sehemu nzuri sana ya kuanzia na hili ni zoezi zuri la kufanya kwa sababu litakupa nafasi ya kuona vitu kwa uhalisia wake. Na unapoona vitu kwa uhalisia wake unaweza kufanya maamuzi ambayo ni sahihi kwako.

Kwa vitu ambavyo unaambiwa ni bure, kuna gharama ambazo zimejificha kama;

  1. Ubora wake kutokuwa wa hali ya juu, hii itakupelekea kuhitaji kununua kitu cha gharama zaidi.
  2. Itakuchukua muda mpaka kupata kile unachotaka na hivyo kujikuta unalipa gharama ya muda.
  3. Itakugharimu utu wako, baada ya kupokea ha bure utajikuta unalazimika kurudisha fadhila hata kama ni kitu ambacho hupo tayari kufanya.
  4. Kukosa uhuru wa kuchagua, utajikuta unapokea chochote unachopewa kwa sababu huna nguvu ya kuchagua.
  5. Kushindwa kuthamini kitu na kukitumia vizuri, kitu kinapokuwa cha bure, hata wewe mwenyewe hukipi uzito mkubwa.

Na vitu vya bei rahisi pia vina gharama hiyo iliyojificha, mara nyingi unapata thamani ambayo ni ya chini, na hivyo kujikuta unalipia tena, na pia utapoteza muda wako mwingi mpaka upate hicho ambacho ni cha bei rahisi.

Ufanye nini?

Kabla hujafurahia na kutumia nafasi unayoambiwa ni bure au bei rahisi, jiulize kwanza na gharama gani iliyojificha, kisha jipime kama unaweza kulipa gharama hiyo. Kama huna namna kwa sasa unaweza kuilipa, kama unaona itakugharimu sana ni bora ukazane na ulipe gharama kamili badala ya kukimbilia vya bure au vya bei rahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK