Habari za leo rafiki yangu?
Hamasa kidogo siku ya leo itakusukuma kuweka juhudi kwenye miezi hii michache iliyobaki kumaliza mwaka huu 2016. Mwaka ulianza taratibu na sasa unamalizika. Na swali ambalo nitakuuliza ni hili, je mwaka huu umeongeza maana yoyote kwenye maisha yako au unaishia kuuhesabu tu kama mwaka mwingine unaopita?

Kwa maana namaanisha miaka kumi ijayo, kuna kitu utaangalia na kusema mwaka 2016 nilifanya maamuzi sahihi ambayo yamekuwa bora sana kwangu? Kama hujafanya kitu cha aina hiyo kwenye mwaka huu, basi unaelekea kuupoteza rafiki yangu. Na nitakusihi sana leo hii, yaani sasa hivi utakapomaliza kusoma hapa, angalia ni kipi kimoja unachoweza kubadili kwenye maisha yako. Nakusihi tena rafiki, usikubali mwaka huu upite bila ya kufanya kitu cha tofauti na namba ambavyo umekuwa unafanya miaka mingine. 

WAHI TIKETI YAKO SASA, BONYEZA PICHA KUPATA TIKETI.

Vipo vitu vingi sana unavyoweza kuanza kufanya leo na ukabadili kabisa mwelekeo wa maisha yako kabla mwaka huu 2016 haujaisha. Angalia ni kipi hasa unachotaka kwenye maisha yako, na anza kukifanyia kazi. Acha kusubiri mpaka kila kitu kiwe sawa, na badala yake anza sasa. Kama utahitaji msaada wangu kwenye hatua gani uchukue au uanzie wapi, tuwasiliane.

Karibu rafiki kwenye kile ambacho napenda kukushirikisha kupitia makala hii ya leo. Leo nakuambia jiwashe moto na watu watakuja kukuangalia ukiungua. Sijajua kama umeielewa vizuri hiyo sentensi, lakini nitakuelezea ili uweze kuelewa vizuri.

Sehemu yoyote ambapo kuna giza, mwanga unaleta tofauti. Mwanga unafanya watu watoke kwenye giza na kusogea kwenye mwanga. Wote tunajua kwamba hakuna mwanga kama hakuna nguvu inayotumika kutengeneza mwanga huo. Nguvu hiyo inaweza kutokana na viumbe, ikatokana na madini au ikatokana na umeme.
Kwenye kazi au biashara ambayo unafanya, kuna watu wengi mno ambao wapo kwenye giza. Kuna vitu vingi ambavyo watu hawajui kama vipo au vinatokea. Wapo ambao maisha yao ni magumu kwa sababu tu hawana taarifa na maarifa sahihi ya kile wanachotaka kwenye maisha yako. Ndani ya giza hili, hakuna aliye tayari kutoa mwanga kwa sababu kutoa mwanga kunahitaji nguvu, na nguvu inatoka ndani ya yule ambaye anataka kutoa mwanga.

Ndiyo maana nakuambia wewe rafiki yangu, jiwashe moto na watu watakuja kukuangalia ukiungua, na siyo kukuangalia pekee, bali watafaidika na mwanga wako, na wewe pia utafaidika kupitia wao. Unapojiwasha moto, unatoa fursa na nafasi nzuri kwa wengine kupata maarifa na taarifa sahihi zinazowawezesha kuchukua hatua kuboresha maisha yao.

Kujiwasha moto maana yake ni kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho unafanya. Ni kujitoa kwa hali na mali, kufanya siyo kwa sababu wengine wanafanya, ila kufanya kwa sababu umechagua kufanya, na kwa sababu unataka kutoa mchango kwenye maisha ya wengine. Kwa sababu unajua mafanikio yako ni matokeo ya mafanikio ya wale wanaokuzunguka na wanaonufaika na kile unachofanya.

Unapojiwasha moto, unaacha kujionea huruma, unaacha uvivu, unaacha kufanya kwa mazoea na unajitoa hasa, unaweka kila tone la jasho, machozi na damu yako kwenye kile ulichochagua kufanya. Unakubali kuteseka kwa ajili ya wengine, siyo kwa sababu unataka uonekane unateseka, bali kwa sababu unafurahia kutoa mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine.

Utakapoamua kujiwasha moto, wapo wengi watakaokuja na maoni ya ushauri wao, kwamba unafanya sana, kwamba umepitiliza, na maneno mengine ya kukata tamaa. Lakini mimi nataka nikuambie jambo moja, endelea kuchochea moto, wale wakatishaji tamaa siyo watu wazuri kwako. Achana nao na songa mbele, wewe angalia kile ambacho unatoa kwa wengine.

Huu ndiyo ujumbe wa hamasa ambao nataka uondoke nao siku ya leo rafiki yangu. Unapochagua kufanya kitu, kifanye kweli mpaka akila mtu akiangalia aseme kweli hapa kuna mtu amejitoa kufanya. Amua kufanya kweli, usiguse juu juu, bali fanya, na fanya kweli kweli.

Nasisitiza sana rafiki yangu, fanya kwa sababu ndiyo kitu unapenda kufanya, fanya kwa sababu unataka kutoa mchango wako kwenye maisha ya wengine na fanya kwa sababu unataka kuacha alama hapa duniani. Usifanye kwa sababu kila mtu anafanya, au kwa sababu umezoea kufanya au kwa kuwa wengine watakuona ukifanya. Ukiwa na sababu hizo za mwisho hutaweza kujiwasha moto, utajionea huruma na utafanya yale ambayo ni ya kawaida. Na sote tunajua, wale wote ambao wanafanya kwa kawaida, huishia kupata matokeo ya kawaida.

Mwaka unaisha rafiki yangu, fanya kitu leo, fanya kitu sasa.

Nikukumbushe haya muhimu;
1.     Karibu kwenye kundi la TELEGRAM la AMKA MTANZANIA, bonyeza maandishi haya kujiunga moja kwa moja kwenye kundi hili.
2.     Jiunge na mfumo wetu wa email, ambapo kila jumanne, alhamisi na jumapili nakutumia email nzuri za mafunzo na hamasa. Bonyeza hapa kujiunga na mfumo wa email.
3.     Tarehe 30/10/2016 tutakuwa na semina ya milioni ya ziada, itafanyika ubungo plaza, dar. Hii siyo semina ya kukosa rafiki, pata tiketi ya kuhudhuria semina hii, bonyeza hapa kupata tiketi ya kushiriki semina hii ya kipekee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK