Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye mafanikio makubwa, watu wengi sana wamekuwa wanajidanganya. Nasema watu wanajidanganya kwa sababu huwa wanayaangalia mafanikio makubwa kama ndoto, ambayo wanaiona vizuri, ila hawajui wanafikaje pale.
Mtu anaweza kukueleza vizuri maono yake makubwa na hata ndoto zake kubwa. Anaweza kukuambia vizuri anataka kuwa wapi baada ya muda gani, lakini ukiangalia anachosema na hatua anazochukua ni vitu ambavyo haviendani kabisa.
Ili kuweza kufika kule ambapo unataka kufika, kwenye mafanikio makubwa zaidi, hautajikuta pale kama muujiza, bali utahitaji kuanzia hapo ulipo sasa. Na hapo ulipo, panaweza kuwa mbali sana ukilinganisha na kule unakotaka kufika. Na hapo ndipo tatizo kubwa kabisa lilipo kuhusu mafanikio.
Tatizo moja kubwa unalohitaji kutatua ili kuweza kupata mafanikio makubwa, ni kuziba pengo lililopo kati ya hapo ulipo sasa na kule unakotaka kufika. Bila ya kuziba pengo hilo, chochote unachofikiria ni ndoto ambazo hazitakufikisha popote.
Hakuna anayeweza kukuzia kuwa na ndoto kubwa utakavyo, lakini kitakachokuzuia kuzifikia ni pengo lililopo kati ya ulipo sasa na unakotaka kufika. Kadiri pengo hilo lilivyo kubwa, ndivyo kazi unayopaswa kufanya inazidi kuwa kubwa, ndivyo muda unaohitaji unakuwa mrefu zaidi.
Kwa mfano tuseme lengo lako ni kuwa bilionea, na hapo ulipo sasa huna hata akiba au uwekezaji unaokuzalishia, unaishi kwa kipato cha mkono kwenda kinywani, na wakati huo huo una madeni. Safari yako itakuwa ngumu zaidi kwa sababu pengo lililopo hapo ulipo na unapotaka kufika ni kubwa.
Watu wengi wamekuwa wanaweka malengo yao makubwa bila ya kuangalia pengo walilonalo, na ukiwaangalia unaona wanavyochukulia kirahisi mafanikio makubwa.
Huwa wanaona ni kitu ambacho kitakuja kwao tu kwa sababu wanasema wanataka au wameshapanga.
Kupanga ni asilimia 0.001, kuchukua hatua ni asilimia 99.999 ya mafanikio yako.
Kupanga ni rahisi, lakini kuchukua hatua kunakuhitaji kuweka kazi kubwa.
SOMA; Jiwashe Moto, Watu Watakuja Kukuangalia Ukiungua.
Kuchukua hatua kunahitaji machozi, jasho na hata damu.
Utatokwa na machozi kwa maumivu utakayopata kwenye safari yako ya mafanikio. Utahitaji kufanya zaidi ya wengine, utaangushwa, utatapeliwa, utadanganywa na hata wale uliokuwa unawategemea, watakuangusha.
Utatokwa na jasho kwenye hatua utakazohitaji kuchukua. Wakati wengine wanafanya kazi masaa 8 kwa siku, wewe utahitaji kufanya kazi masaa 18 kwa siku. Wakati wengine wanafurahia mwisho wa wiki na kupumzika, wewe hutakuwa na mwisho wa wiki, kila siku itakuwa ni kazi kwako. Jasho litakutoka vya kutosha, na kadiri pengo linavyokuwa kubwa, ndivyo jasho litakutoka zaidi.
Utatokwa na damu pale utakapohitaji kujitoa kafara kwenye baadhi ya mambo. Yapo mambo muhimu sana kwako kufanya, lakini itabidi uache kuyafanya kwa sababu unafanyia kazi kufikia mafanikio makubwa. Kuna vitu vizuri kwako na unavyopenda sana kufanya lakini itabidi uachane navyo ili kufanyia kazi ndoto yako. Utaumia sana kupoteza vitu ambavyo ulikuwa unavipenda na kuvijali, lakini haviendani na mafanikio unayofanyia kazi.
Hivyo rafiki yangu, pengo lililopo kati ya ulipo sasa na kwenye mafanikio makubwa unayotaka, lazima lizibwe kwa machozi, jasho na damu. Lazima ulijue pengo hilo na hatua unazochukua ziendane na ukubwa wa pengo hilo.
Kuchukua hatua ndogo au zisizoendana na pengo unalofanyia kazi, ni kujidanganya na utaishia kuimba kwamba unataka mafanikio makubwa lakini hutayapata.
Hakuna wa kukuzuia kufika popote unapotaka kufika ila wewe mwenyewe. Chukua hatua kubwa sasa, hatua zinazoendana na pengo lililopo mbele yako na utaweza kufanikiwa sana.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha