Kuna vitu viwili muhimu mno kwa mafanikio kwenye zama hizi tunazoishi.

Cha kwanza ni ubunifu, bila ya ubunifu huwezi kupiga hatua. Hii ni kwa sababu kila mtu anafanya kile ambacho unafanya. Na hata ukianza kitu kipya kabisa, bado watu watakuiga kama kitaonesha mafanikio. Hivyo silaha pekee unayoweza kutumia ni kuwa mbunifu, kila siku na kila mara.

Kitu cha pili ni ushirikiano, huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, unahitaji ushirikiano wa wengi ili uweze kufikia malengo yako. Hakuna mtu anayeweza kufanikiwa yeye mwenyewe. Ushirikiano na wengine ni msingi muhimu wa mafanikio yako.

Sasa kipo kitu, ipo tabia yetu ambayo inaua kabisa misingi hii miwili muhimu ya mafanikio. Tabia hii inaua ubunifu wako na inawazuia watu kushirikiana na wewe.

Tabia hii ni tabia ya kujihami na kujitetea. Ni kawaida yetu sisi binadamu ujihami na kujitetea, pale ambapo ambo yanakwenda tofauti na tulivyotarajia. Kama unakutana na hali ya hatari, ni lazima ujihami ili kuokoa maisha yako. Kama unasingiziwa kitu ni lazima ujitetee ili kuepusha matatizo yasiyokuhusu.

Lakini tunapoleta tabia hii kwenye kazi au biashara zetu, tunaua kabisa ubunifu na ushirikiano. Kwa mfano kama umefanya kosa kwenye kazi yako, kutafuta njia ya kujitetea ili kosa lisionekane lako ni sumu kubwa sana. Unaweza kufanikiwa kuwashawishi watu wakakubaliana ana wewe, lakini hawatakuchukulia kawaida kwenye shughuli zako na wao. Watapunguza ushirikiano na wewe kwa sababu wanajua ukifanya makosa hukubali.

Mfano mwingine ni pale unapoona wenzako wanafanya makubwa, au wanafanikiwa, hawa ni wenzako ambao labda mmesoma pamoja au mmekua pamoja. Ila kwa sasa wao wamepiga hatua na wewe bado. Sasa ili usionekane wewe ni mzembe, unaanza kujihami na kujitetea, kwamba wao walipata bahati, au wametokea familia zenye uwezo, au sababu nyingine yoyote. Hii yote ni kujitetea na haina faida yoyote zaidi ya kumrudisha mtu nyuma zaidi.

Hivyo rafiki yangu, acha tabia ya kujihami na kujitetea, kama umefanya kosa kubali na rekebisha. Kama umefanya uzembe kubali na chukua hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK