Nimekuwa nikipokea maswali na maoni mbalimbali kuhusiana na Makala mbalimbali zilizopo kwenye Amka mtanzania. Lakini nimepokea maswali mengi zaidi yanayohusu ardhi tofauti na ujenzi. Hali hii inatokana na majengo kuwa sehemu ya ardhi kwa mujibu wa taaluma, sera na sheria za ardhi. Kwa kuwa lengo letu ni kuhakikisha watanzania tunabadilika na kila mmoja wetu anafanikiwa kupitia fursa zilizopo hivyo basi Katika kutimiza azma yetu, tumekuwa tukiwapa ushauri ili muweze kuvuka vikwazo mbalimbali vinavyowakabili. Hali hii inaonyesha na kudhihirisha kuwa kuna tatizo kubwa kuhusiana na umiliki na matumizi ya ardhi ndani ya nchi yetu, hali hii inawaumiza watu kimyakimya, hivyo basi kwa umoja wetu na kwa nafasi ya kila mtanzania tuhakikishe tunakuwa sehemu ya ufumbuzi wa migogoro ya ardhi ili turuhusu maendeleo yaweze kufanyika kwa haraka na wakati muafaka, maana ardhi ni rasilimali na kichocheo kikuu cha mafanikio ya kila mmoja wetu. Kupitia Makala hii nitatoa ufafanuzi juu ya mambo machache ambayo yamekuwa na uelewa tofauti katika jamii wakati mwingine kuwa chanzo cha migogoro. 

 
 
1.USIMAMIZI WA ARDHI
Kwa mujibu wa sheria za ardhi Tanzania, Ardhi ni mali ya Watanzania wote bila kujali jinsia wala tabaka. Ardhi ya Watanzania inasimamiwa na Rais kwa niaba ya Watanzania wote kama msimamizi na mdhamini mkuu wa ardhi. Kwa maana hiyo, mamlaka ya juu ya usimamizi wa ardhi ya Tanzania ni Rais wa Tanzania.
Hata hivyo, ili kuhakikisha usimamizi thabiti wa ardhi, serikali kupitia mfumo na muundo wa kiutawala inao wataalamu wanaotoa ushauri kwa serikali na wananchi katika masuala yote yanayohusiana na utawala, usimamizi, umiliki na utumiaji wa ardhi katika masuala endelevu. Wataalam wa Ardhi wa ngazi zote hufanya kazi kwa niaba ya Rais wa nchi. Miongoni mwa majukumu ya wataalamu ambao ni maafisa ardhi ni pamoja na kutoa hati za umiliki wa ardhi katika ardhi ya maeneo yaliyopimwa.
Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama vile halmashauri za wilaya au manispaa zina uwezo wa kutoa maelezo yoyote yanayohusu ardhi kupitia kamati zake au maafisa wake kuhusiana na utawala wa ardhi chini ya Sheria ya Ardhi, kwa ardhi iliyo ndani ya mipaka ya eneo lake.
Halmashauri ya Kijiji imepewa wajibu wa kusimamia ardhi yote ya kijiji. Katika kutekeleza wajibu wake, Halmashauri ya Kijiji itabidi kuzingatia ushauri, mamlaka, uwezo, madaraka, haki na wajibu wa taasisi na mamlaka nyingine zilizotambuliwa na sheria kuhusiana na ardhi. Hata hivyo katika kuendesha utawala katika ardhi ya kijiji, Halmashauri ya Kijiji inafanya kazi kama mdhamini kwa niaba ya wanufaika ambao ni wanakijiji. Kwa maana hiyo chombo chenye madaraka ya mwisho katika usimamizi wa ardhi ya kijiji ni Mkutano Mkuu wa kijiji na ugawaji wote wa ardhi ya kijiji lazima uthibitishwe na Mkutano Mkuu wa Kijiji. Kutokana na uzoefu, kumekuwa kukijitokeza migogoro mingi ya ardhi katika maeneo ya kijiji hasa pale ardhi ya kijiji inapogawiwa kwa wawekezaji. Wanakijiji wanapaswa kufahamu kuwa viongozi pekee hawana mamlaka ya kugawa ardhi ya kijiji bila ya kuwashirikisha wanakijiji wote kupitia mkutano mkuu.

SOMA;  Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa

2. UMILIKI WA ARDHI
Upatikanaji wa ardhi Tanzania huwezeshwa kwa kupitia njia kadhaa ambazo ni halali na zinazokubalika kisheria katika jamii. Kwa ujumla mtu au taasisi anaweza kumiliki ardhi kwa ama kugawiwa, kurithishwa, kupewa, kutwaa au kununua. Kutwaa hutumika pale ambapo mtu huingia katika eneo kama vile pori na kusafisha kisha kuliweka katika matumizi. Njia hii ni kongwe sana hapa nchini lakini ni ngumu kutumia njia hii nyakati hizi za sasa kwa kuwa karibu ardhi yote ipo chini ya umiliki, hivyo kutumia njia hii ni kuchochea migogoro ya ardhi. Urithi; Mtu yeyote anaweza kupata ardhi kwa njia ya urithi. Anaweza kurithi ardhi kutoka kwa ndugu, mke/mume au wazazi wake. Jinsia au tamaduni na mila haviwezi kuwa kigezo cha kumnyima mtu haki hiyo ya kurithi ardhi. Mgao wowote utakao mnyima haki hiyo kwa misingi ya jinsia au mila ni batili na unaweza kuwafikisha wahusika mahakamani.
Kugawiwa na Serikali; Mtu yeyote anaweza kupata ardhi kwa kugawiwa na Serikali. Anaweza kuomba ardhi na Kamishina akiridhika kwamba umetimiza masharti atakugawia ardhi hiyo. Katika ardhi ya kijiji, serikali ya kijiji ndiyo yenye mamlaka ya kugawa ardhi. Kununua; Hii pia ni njia mojawapo ambayo mtu yeyote anaweza kuitumia kupata ardhi Wakati mmiliki anapotaka kuuza ardhi yake iwe ya kijiji, hifadhi au binafsi, sheria inatoa ruhusa ya kununua kama unaweza. Upangishaji ni njia mojawapo ya kupata ardhi. Tofauti na njia nyingine za upatikanaji wa ardhi, upangishaji unakupatia haki pungufu na yule anayekupangisha.
Haki Miliki; Kwa muijibu wa sera na sheria za ardhi umiliki wa Ardhi unatambuliwa uko wa aina mbili:- Hakimiliki ya kiserikali (granted right of occupancy), na Hakimiliki ya kimila (customary right of occupancy). Aina hizi mbili za hati ya kumiliki ardhi Zina hadhi sawa kisheria. Ingawa hakimiliki ya kimila ilichukuliwa kama haki ya matumizi tu ya ardhi na haikubeba uzito kama ilivyo kwa hakimiliki ya kiserikali. Kwa hiyo, ilipotokea mgogoro kati ya wamiliki wawili, mmoja akiwa na hatimiliki ya kiserikali na mwingine akiwa na hakimiliki ya kimila, basi hakimiliki ya kimila ilionekana kuwa haina nguvu na hivyo kutotambuliwa. Kwa hivi sasa haki miliki ya kimila ina hadhi sawa sawa na hakimiliki kiserikali.
Hati miliki kimila ina hadhi ambayo kwa hali yoyote ni sawa na hati miliki inayotolewa kisheria: Yaweza kutolewa na Halmashauri ya kijiji kwa raia, familia ya raia kikundi cha raia wawili au zaidi, au chombo chenye hadhi ya shirika ambacho wabia wake wengi ni raia wa Tanzania.

SOMA; Ili Upate Mafanikio Ya Kudumu, Wekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.

3. MATUMIZI YA ARDHI
Ardhi ni rasilimali ambayo hupanda thamani kwa kadri siku zinavyoenda na kwa kadri mahitaji ya ardhi yanavyoongezeka. Hivyo ardhi inaweza kuendelezwa kutoka hali iliyokuwa nayo kwenda hali nyingine tofauti. Miongoni mwa matumizi endelevu ya ardhi ni pamoja na kujenga majengo ya kukaa au kupangisha, kuitumia kwa kilimo cha biashara na chakula au kuitumia ardhi kwa shughuli za ufugaji. Kama ardhi itaendelezwa kwa kujenga majengo basi majengo yale yanaweza kutumika kama makazi ya mwenye nayo au kutumika kama makazi au majengo kwa ajili ya kupangisha kibiashara.
Njia nyingine ya kuitumia ardhi kama sehemu ya kitega uchumi ni kuuzwa kwa wanunuzi mbalimbali. Ardhi inatumika kupata dhamana ya mkopo kwa kutumia ardhi kama kitu cha usalama (security) kwa mkopeshaji wa mkopo. Mmiliki wa ardhi huweza kuomba mkopo katika taasisi za fedha kama vile benki kwa kuweka hati ya miliki ya ardhi yake kama dhamana ya mkopo aliochukua. Tanzania ni nchi iliyo kwenye mikakati ya maendeleo endelevu. Maendeleo endelevu hutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo maliasili kama ardhi.Taasisi za fedha pia zinachangia katika maendeleo kwa njia ya kuwapatia wananchi mkopo wa fedha kwa riba. Kutokana na nia ya kuhakikisha uwepo wa maendeleo, Serikali ilionelea ni vyema kurekebisha baadhi ya vipengele katika Sheria za Ardhi, 1999 na Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura 334) kupitia kutungwa kwa Sheria ya Rehani. Sheria ya Rehani inatumika kuongoza taasisi za fedha katika kukopesha fedha kwa wananchi.
Ardhi ni rasilimali kubwa ambayo inaweza kupangishwa kulingana na mahitaji ya wakati huo na kumletea faida kubwa mmiliki wake. Mojawapo ya shughuli za upangishaji zilizozeleka ni upangishaji wa nyumba kwa ajili ya pango la makazi au biashara. Kwenye ardhi ya kijiji upangishaji uliozoeleka ni upangishaji kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Upangishaji wa aina hizi huweza kudumu kwa muda mfupi na muda mrefu. Upangishaji mwingine ambao una faida kubwa kwa hivi sasa ni upangishaji kwa wawekezaji kutoka makampuni makubwa ya kigeni na makampuni ya ndani ya nchi. Upangishaji huu wa ardhi una tija kubwa kwa wananchi hasa wanaomiliki ardhi mijini na vijijini. Ila tu, katika hatua hii ya upangishaji ni muhimu kwa wananchi kupata ushauri wa kisheria kabla ya kuingia mikataba. Pia Mmiliki wa ardhi anaweza kuwekeza ardhi yake kama mtaji mkubwa wa biashara kwa ama yeye mwenyewe au kuingia ubia na mwekezaji mkubwa na kujipatia faida kubwa kwa maendeleo yake binafsi au taifa.

SOMA; Faida Za Uwekezaji Wa Majengo Kwenye Maeneo Salama Na Yaliyopimwa Na Wataalam Wa Ardhi

4. ZINGATIA USHAURI
Miongoni mwa chanzo kikuu cha migogoro wakati wa ujenzi ni umiliki wa ardhi, ili kuepuka hili fuata taratibu zote wakati wa uhamishaji wa ardhi kutoka miliki moja kwenda miliki nyingine kutokana na sababu kadhaa zikiwamo kuuza, kurithi au kugawiwa. Pia Ardhi inaweza kutwaliwa na matumizi yake ya awali yakabadilishwa kwa ajili ya uendelezaji wa matumizi mengine kwa manufaa ya umma na mwenye ardhi anastahili kulipwa fidia pindi azimio la utwaaji wa ardhi litakapopitishwa.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com