Kuna wakati itakuwa mara ya mwisho kwako kufanya kile ambacho unapenda kufanya.
Itakuwa mara ya mwisho kwako kufanya kazi au biashara yako, mara ya mwisho kukaa na wale wa karibu yako, mara ya mwisho kumwambia mtu unampenda.
Itakuwa mara ya mwisho kwako kutoa mchango bora kwa maisha ya wengine. Upo wakati ambao utakuwa ni mara ya mwisho, hutapata tena nafasi nyingine ya kufanya hicho ambacho unataka kufanya.
Kwa bahati mbaya sana hatujui ni lini itakuwa mara ya mwisho, huenda ikawa sasa, huenda ikawa kesho. Hatujui. Na kwa kutokujua ni lini itakuwa mara ya mwisho, tumekuwa tunachukulia mambo poa sana. Tumekuwa tunafanya tukijua kesho ipo, hivyo hatutumii fursa ya leo vizuri.
Tuna nafasi ya kuweka ubora zaidi kwenye kazi yetu leo lakini hatufanyi hivyo kwa kisingizio kwamba kesho ipo. Tuna nafasi ya kumwambia mtu tunampenda leo, lakini hatufanyi hivyo tukiamini kesho ipo. Pia tuna nafasi ya kuomba msamaha wale tuliowakosea, au kuwasamehe wale waliotukosea leo, lakini tunasubiri tukiamini kesho ipo.
Swali ni je vipi kama hakuna kesho? Vipi kama leo ndiyo mara yako ya mwisho kupata nafasi kama uliyoipata leo?
Hatua za kuchukua.
Kwa jambo lolote muhimu unalotaka kufanya kwenye maisha yako, basi wakati sahihi kwako kulifanya ni sasa. Hakuna wakati mwingine utakaokuwa sahihi zaidi ya sasa. Tumia wakati huu ulionao vizuri, usijidanganye utafanya kesho, leo inaweza kuwa ndiyo nafasi ya mwisho kwako kufanya kile unachotaka kufanya.
Kwa jambo lolote lile ambalo unalifanya sasa, lifanye kwa ubora wa hali ya juu kabisa. Weka kila kilichopo ndani yako kwenye kile unachofanya sasa. Usijibanie, usiache kuweka kile ambacho unajua ni bora, usifanye juu juu ukisema kesho utaboresha zaidi. Fanya leo na fanya kwa ubora, huenda ndiyo mara yako ya mwisho kufanya. Hakuna ajuaye.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK