Moja ya malengo niliyojiwekea katika kipindi chote cha uhai wangu ni kuhakikisha natumia uwezo wangu wote kuifanya Tanzania iwe moja ya nchi nzuri na salama kwa watanzania wote, napenda kuwa chachu ya mabadiliko endelevu ya nchi yangu Tanzania, njia mojawapo ni hii ya uandishi wa hizi Makala zinazowafikia maelfu ya watanzania popote walipo. Pia asanteni sana wasomaji wangu kwa maoni yenu mazuri na yenye tija kwa jamii yote ya Tanzania, nami nawaahidi kuwa nitaendelea kuwapa ushirikiano pasipokujali tofauti za aina yeyote ile. Hii inaonyesha mwonekano na ujasiri mkubwa sana walionao watanzania juu ya uwekezaji wa majengo tofauti na miaka kadhaa iliyopita. Uwekezaji wa majengo ni sekta mpya na inayokuwa kwa kasi sana hapa Tanzania tofauti na wakati mwingine wowote, mara nyingi jambo jipya huwa na changamoto zake ambazo ni tofauti na tulizozizoea, usikubali kirahisi hali yeyote isababishe usifikie malengo yako, njia sahihi ni kutafuta njia bora ya kuondoa changamoto zinazokukabili na siyo kukata tamaa. Makazi bora na salama ni haki ya kila Mtanzania, tuhamasishane kuweza kufikia viwango bora vya makazi ya kibinadamu. Maswali mengi Zaidi niliyoulizwa yanahusu ujenzi wa gharama nafuu. Wakati mwingine nasema ujenzi wa gharama nafuu ni kilio kikuu kwa watanzania walio wengi pasipo kujali tofauti ya vipato vyao. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili uweze kutimiza ndoto yako ya kuwa na makazi bora kulingana na kipato chako.

1. UBUNIFU WA MAJENGO
Ubunifu wa majengo ni hali ya kuumba taswira iliyo kwenye kufikiri na kuiweka katika hali Fulani ya mwonekano wa umbo halisi. Ubunifu huwa ni jambo la awali kwenye ujenzi. Ubunifu huu huwasilishwa kwa njia ya michoro ya kisanifu na hatimaye kutumika kuumba umbo halisia. Mara nyingi katika hatua hii ni vema ukajitathmini kama hicho unachofikiria kukijenga una uwezo nacho au la. Je ni mpango wa muda mrefu au muda mfupi? Unahitaji muda gani kufikia gharama halisi ya nyumba ya ndoto yako? Jipange na uwe mwenye nidhamu katika safari hii ya kufikia malengo haya. Ubunifu na mwonekano halisi wa nyumba yako hutafsiri gharama halisi ya nyumba yako. Zipo njia mbalimbali zinazotumika kupunguza gharama kwenye ujenzi wakati huohuo unafikia lengo kuu la mwonekano wa nyumba uitakayo. Mfano; njia ya kupunguza idadi ya kuta za ndani hasa zile zisizo na ulazima, kuwepo au kutokuwepo wa kuta hizo hakuathiri mgawanyo au mpangilio wa nyumba. Zungumza na msanifu majengo kuhusu mahitaji na malengo ya ndoto yako ya kuwa na nyumba uitakayo. Naamini atakushauri vizuri na atatumia taaluma yake kukusaidia kufikia kile unachofikiria kwa miaka mingi. Ubunifu ni muhimu sana, jenga nyumba bora na ya kisasa zaidi, ni bora ukajenga nyumba ndogo yenye mwonekano mzuri, kuliko nyumba kubwa na ukashindwa kuimaliza, huko ni kukosa mipango bora na yenye uhakika.

SOMA;  Hatari Tatu Zinazoukabili Uwekezaji Wako Wa Majengo Na Namna Ya Kuepukana Nazo.

2. USIMAMIZI WA UJENZI
Hii ni hatua muhimu sana ambayo haipaswi kupuuzwa, ni hatua ambayo ubunifu uliowasilishwa kwenye michoro kutafsiriwa na kuwa katika umbo lenye mwonekano halisi. Ni vema ukaambatana na mjuzi wa ujenzi katika kusimamia ujenzi wako ili akushauri kwenye hatua mbalimbali, ujenzi wa kisasa ni tofauti sana na ujenzi tuliozoea nyakati zilizopita, nyumba za kisasa zina mifumo mingi ili kukidhi mazingira halisi ya leo na kesho. Sayansi na teknolojia ya sasa inatulazimisha tutumie ujuzi wa kitaaluma kwenye ujenzi hata ule ambao ni mdogo Zaidi, hii ni kutokana na nyumba za kisasa kuhitaji mifumo mingi inayohitaji taaluma tofauti tofauti ili kukidhi mahitaji ya lazima kwa matumizi ya jengo. Ni muhimu sana kupangilia aina za kazi kiutendaji, ni mhimu sana kuwafahamu mafundi wako kiutendaji, pia ni muhimu sana kufahamu tabia za watu wote wanaohusika kwenye ujenzi wako. Usiwapuuze wazembe na wote wenye mtazamo hasi juu ya kile unachofikiria katika usahihi wake na kamwe usimwamini yeyote kwa maneno pasipo kujiridhisha, weka msimamizi bora, mwaminifu na mjuzi wa mambo ya ujenzi ili akusaidie kutembea katika dira uliyoichagua, namaanisha gharama, ubora na muda utakaoutumia kujenga nyumba hiyo. Weka mifumo itakayoweka wazi ununuzi wa vifaa vya ujenzi, matumizi yake na ulinganifu wake, mifumo hiyo itakusaidia kufanya uhakiki wa kila kilichotumika na uhalisia wa gharama zake. Kutofanya hivyo ni kujiweka kwenye hatari ya kutofikia lengo lako kwa uhakika, ni kujiweka katika hatari usioijua.

SOMA; Faida Za Uwekezaji Wa Majengo Kwenye Maeneo Salama Na Yaliyopimwa Na Wataalam Wa Ardhi

3. SERA NA UTAWALA KISIASA
Mara nyingi nimelisema hili na leo nalisema tena, ni muhimu sana kuwashauri viongozi wetu wa kisiasa kuwa vifaa vya ujenzi vipewe kipaumbele hasa kuhusu gharama kubwa ambazo watanzania wengi bado hawawezi kukidhi na kuwa na makazi bora ingawa ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kuwa na makazi bora na salama. Uchumi wowote ule, uwe wa mtu binafsi au wa nchi kwa ujumla huathiriwa na sera za wakati huo na vipaumbele vya utawala kisiasa. Makazi ni moja ya mahitaji ya lazima ya binadamu yeyote, kutokuwa na makazi bora na salama ni kuhatarisha uhai, kwa umoja wetu tuhamasishane tudai sera endelevu na rafiki zitakazotusaidia kupunguza makali ya gharama za ujenzi. Saruji, nondo, rangi, kokoto, mchanga, mabati ni moja ya malighafi katika ujenzi ambazo huzalishwa hapa hapa Tanzania, hivyo ni rahisi tukaweka mikakati ya kuwa na bei rafiki kwa watanzania wa vipato vyote na hatimaye kila mmoja wetu apate ahueni ya maisha. Wachumi na watu wa mipango ya maendeleo ya jamii naomba mtusaidie hili jambo.

SOMA; Ili Upate Mafanikio Ya Kudumu, Wekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.

4. ZINGATIA USHAURI
Unapaswa kutambua kuwa ujenzi ni uwekezaji ambao haupaswi kulinganishwa na uwekezaji wowote uliokwishatokea, hivyo hupaswi kupuuza hatua yeyote uliyokwishaifanya na ambayo unatarajia kuifanya. Kwenye ujenzi hakuna jambo dogo linalopaswa kupuuzwa, unapaswa kujipongeza kwa kila hatua uliyofikia, endelea na ifanye nyumba yako kuwa mahali bora na salama kwa kila atakayefika hapo. Mambo hayo matatu ni miongoni mwa sababu zinazoathiri jitihada zetu za kuwa na makazi bora kwa gharama nafuu. Kutokuwa na ubunifu na usimamizi bora kabla na wakati ya ujenzi kutakuongezea gharama mara dufu Zaidi. Utawekewa malighafi zisizofaa na utaambiwa vitu ambavyo havipo wala havipaswi kuwepo kwenye mfumo wa ujenzi wako, huko ni kutengeneza nyumba nyingine usiyoijua. Ni hatari na hasara katika uchumi wako. Ni vema ukafanya ujenzi wako kwa uhakika na furaha kwa kutembea na mtu atakayelinda dira yako hata kukamilika kwake.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com