Kama jinsi ambavyo unahitaji zana ili kufanya kazi yoyote unayotaka kufanya, ndivyo pia unavyohitaji zana ili kutengeneza mafanikio yako. Hakuna kitu kinachotokea chenyewe, kila kitu kinatengenezwa. Na panapotengenezwa kitu, zana ni muhimu.
Zana za mafanikio zinaanza na wewe mwenyewe, zinaanzia kwenye akili yako na mfumo wa maisha yako. Zana zifuatazo ni muhimu sana kwako kama unataka kufanikiwa;
1. Kujiamini.
Huwezi kufanikiwa kama hujiamini, ni lazima ujiamini ndiyo na wengine nao waweze kukuamini. Ni lazima ujiamini kwamba unaweza kufanya makubwa, ndiyo uweze kufanya makubwa. Pia lazima uamini kwamba hakuna kinachoweza kukuzuia wewe kupata kile unachokitaka.
Watu hawapendi kuwafuata watu ambao hawajiamini, jiamini na wengi watapenda kuwa na wewe. Kumbuka mafanikio yako yanatokana na wale wanaoamua kwenda na wewe.
2. Nidhamu.
Nidhamu ni zana muhimu ya mafanikio. Kama huna nidhamu chochote unachofanya kitaanguka, hata kama utafanikiwa sasa, haitakuchukua muda utapoteza kila kitu. Nidhamu inakufanya uweze kujiwekea miiko ya vitu gani ufanye na vipi usifanye. Pia inakuwezesha kufanya hata pale ambapo hujisikii kufanya.
3. Maandalizi.
Chochote unachotaka kwenye maisha yako, maandalizi ni muhimu. Unahitaji kuwa na maandalizi ya kiakili kwa kile unachokwenda kufanya. Pia unahitaji maandalizi ya vifaa na mahitaji muhimu kwenye kile unachotaka kufanya. Usianze mambo kwa papara, utaishia njiani. Fanya maandalizi ya kutosha na utaweza kukabiliana na changamoto yoyote utakayokutana nayo.
Hizi ni baadhi ya zana muhimu kati ya zana nyingi za mafanikio. Nimekukumbusha leo ili usisahau, na kama ulishasahau basi kumbuka na chukua hatua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK