Karibu kila siku huwa napata taarifa kutoka kwa watu juu ya fursa nzuri ya kutengeneza kipato kikubwa bila ya kutumia nguvu kubwa. Watu hawa wanaoleta fursa hizi wanakuwa wameshawishika sana juu ya fursa hizo walizopewa.
Lakini kawaida yangu ni kuchunguza kitu kwa undani kabla sijakubaliana nacho au kukifanya. Mara nyingi ninapozifanya uchunguzi wangu naona namna ambavyo fursa hizo zina mambo yaliyofichwa ndani yake.
Unakuta labda fursa hiyo siyo ya ukweli, na hivyo kuja kupelekea matatizo baadaye, pale watu wanaposhindwa kupata kile ambacho walitegemea kupata.
Au mara nyingi unakuta fursa hiyo ni ya kweli, ila watu hawajapewa uhalisia. Watu wanakuwa wameambiwa ule upande mzuri wa fursa pekee, kwamba unaweza kutengeneza kipato kikubwa, lakini hawaambiwi upande wa pili wa fursa hiyo ambapo ni changamoto na kazi ambayo mtu anapaswa kufanya.
Nimekuwa nikijaribu kuwaelewesha watu juu ya mambo haya, lakini huwa hawaelewi, hasa pale wanapokuwa wameshajazwa hamasa juu ya fursa hiyo. Chochote unachojaribu kuwaambia wanakuona wewe hujui au utapitwa na fursa hiyo.
Leo nataka nikushirikishe wewe maarifa sahihi kabla hujajazwa hamasa ya fursa za aina hii na ukapoteza uwezo wako wa kufikiri sawasawa. Msingi wa kupata fedha basi ni ule ule, haujabadilika na wala hautakuja kubadilika.
Pesa ni matunda ya kazi, huwezi kupata pesa kama hujafanya kazi, na ukipata bila ya kazi basi kuna tatizo unatengeneza na baadaye utarudisha au kupoteza fedha zote ambazo umezipata bila ya kazi.
Ili upate fedha halali na ufanikiwe, ni lazima ufanye kazi, lazima utoe thamani kwa wengine. Hakuna njia ya mkato kwenye hili.
Akitokea mtu na kukuambia kwamba kuna fursa ya kupata fedha nyingi bila ya kufanya kazi basi kimbia haraka sana, usiendelee kumsikiliza, maana ukiendelea utajikuta umeshashawishika na kupoteza muda wako.
Watatokea watu na kukudanganya kwamba teknolojia imebadilika, sasa unaweza kupata fedha kwa urahisi bila kufanya kazi, ni uongo, teknolojia haiwezi kubadili msingi wa fedha, hata ije teknolojia kubwa kiasi gani, lazima utoe thamani ndiyo upate fedha, na thamani inahitaji kazi. Hakuna tofauti na hapo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK