Katika jambo lolote ambalo unafanya kwenye maisha yako, watajitokeza watu ambao watakupinga. Watakuambia haiwezekani au unakosea na maneno mengine ya aina hiyo ya kukatisha tamaa.

Pia utakataliwa mara nyingi kwenye kile unachofanya, utahitaji msaada wa wengine na wao watakataa. Au utahitaji kuwashawishi lakini hawatakubaliana na wewe.

Hii ni hali ya kusikitisha na kukatisha tamaa kama hutaielewa vizuri. Kama usipowaelewa vizuri wale wanaokupinga na kukukataa, na kama hutajielewa wewe mwenyewe vizuri, basi utajikuta unaacha kila unachoanza.

Leo nataka nikupe maarifa ya kuwaelewa vizuri wale wanaokupinga na kukukataa.

Mara nyingi watu wanapokupinga na kukukataa, ni kwa sababu zao binafsi. Ni kutokana na mitazamo yao, vipaumbele vyao na hali wanazopitia kwenye maisha yao. Ni mara chache sana watakupinga na kukukataa kwa sababu zako wewe. Msukumo mkubwa utatokana na sababu zao binafsi.

Kwa mfano mtu ambaye ana mtuzamo hasi wa kwamba mambo hayawezekani, atakupinga na kukataa kwa sababu haamini kama inawezekana. Pia watu wana vipaumbele tofauti na ulivyonavyo wewe, hivyo wanaweza kukupinga kwa sababu ya vipaumbele vyao wao wenyewe.

Ufanye nini?

Mtu anapokupinga na kukukataa, usikimbilie kupokea na kuumia, badala yake mwangalie kwanza mtu huyo, mdadisi kwa undani. Angalia ana mtizamo gani juu ya kile unachofanya na maisha kwa ujumla. Pia jua vipaumbele vyake kwenye maisha ni vipi. Na mwisho kabisa angalia hali gani anapitia kwenye maisha yake.

Kwa kuangalia hivyo, utaona namna ambavyo watu wanasukumwa kwa sababu zao binafsi, kukupinga au kukukataa wewe. Kwa kujua hili utaweza kufanya maamuzi sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK