Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana kwako rafiki yangu.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwako kwenda kufanya makubwa.
Tumia nafasi hii ya leo vizuri rafiki yangu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUJALI KWA WENGINE.
Mara nyingi tumekuwa tunashindwa kufanya mambo yetu kwa sababu tunaona wengine wanatufuatilia sana na kufuatilia yale tunayofanya.
Tunaona kama kila tunachofanya wanakifuatilia kwa karibu na kuhukumu au kukosoa.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna anayejali sana kuhusu wewe. Kila mtu anaazana kujali maisha yake na mambo yake. Kila mtu anaweka juhudi kubwa kwenye kufanya maisha yake yanakwenda sawa.
Hivyo ni muhimu kufanya maamuzi ya maisha yako, kwa namna ambayo ni bora kwako na siyo kwa sababu unataka watu wakuone kwa namna fulani.
Ndiyo watu wanaweza kukuuliza, ndiyo wanaweza kukukosoa na kukupinga, lakini baada ya hapo, hawafikirii tena kuhusu wewe na unachofanya. Badala yake wanafikiria maisha yao magumu yanayowakabili.

Fanya maamuzi sahihi kulingana na hali unayopitia, na siyo kuangalia wengine watasema nini.
Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info