Moja ya vitu vinavyopelekea watu kuwa na hofu na kushindwa kuchukua hatua, ni kukosa maarifa sahihi.
Angalia watu wengi ambao wamekuwa wanapanga kuanza biashara lakini wanakuwa na hofu. Mara nyingi inatokana na wao kukosa maarifa sahihi ya kuanzisha biashara zao. Watafikiria namna biashara inavyohitaji kuendeshwa, na kuona hawawezi kila kitu.
Lakini ukiwapa watu hawa maarifa sahihi, kwamba biashara siyo kitu kigumu kama wanavyofikiri, badala yake biashara ni kuongeza thamani kwa wengine, wanaanza kuona namna ya kufanya hivyo kwa urahisi zaidi.
Angalia watu wote ambao wamekuwa wanapanga kufanya mambo lakini wanakuwa na hofu, labda wanataka kuongea mbele ya watu wengine lakini hofu inawafanya wasiweze kutimiza hili. Hofu hii inatokana na kukosa maarifa sahihi ya kuongea mbele ya watu.
Ukiwapa watu hawa maarifa sahihi, kwamba kuongea mbele ya watu siyo kitu kikubwa kama wanavyofikiri, badala yake ni kuchagua mtu mmoja kwenye kundi hilo la watu na kuongea naye tu. Kwa kufanya hivi wanaona hofu ya kuongea mbele ya wengine ikitoweka.
Chochote ambacho unahofia sasa, ni kwa sababu bado hujapata maarifa sahihi ya kukifanya. Kama hujawahi kuendesha gari, siku ya kwanza utakayoendesha utakuwa na hofu kubwa, utaona kama unagonga au kugongwa. Lakini kadiri unavyoendelea kuendesha, unazoea na hofu inaondoka kabisa.
Hatua za kuchukua;
- Orodhesha mambo yote ambayo unahofia kufanya kwa sasa, yote kabisa, usiache hata moja.
- Mbele ya kila jambo andika ni maarifa gani ambayo huna kuhusu jambo hilo, ambayo ndiyo yanakuletea hofu uliyonayo.
- Anza kutafuta maarifa hayo, kupitia kujifunza na hata kufanya. Anza kufanya kwa hatua ndogo kabisa, endelea kuongeza mpaka utakapoondoa kabisa hofu inayokuzunguka kwenye eneo hilo.
Anza kufanyia kazi hofu ulizonazo sasa, hakuna kikubwa bali ni maarifa na uzoefu ambao mpaka sasa huna. Anza kupata maarifa na uzoefu, na hofu zitakimbia zenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK