Kwenye maisha yetu kuna vitu ambavyo tumekuwa tunavipa umuhimu mkubwa sana. Tumekuwa tunaona bila ya vitu hivi maisha yetu hayawezekani kabisa. na tumekuwa tunang’ang’ania vitu hivi mpaka wakati mwingine kutuletea matatizo kwenye maisha yetu.
Kwa kuona vitu fulani ni muhimu sana kwenye maisha yetu, tumekuwa ‘bize’ kupita kiasi, tukiamini kwamba kama tutaacha kuwa bize basi tutakosa kile ambacho ni muhimu sana na hivyo maisha yetu kuwa hovyo.
Leo nataka nikuambie kitu kimoja ambacho unaweza usipende kusikia, hakuna kitu chochote kwenye maisha yako, ambacho kina umuhimu mkubwa kama unavyotaka kuvipa wewe. Kwa kifupi ni kwamba aina ya umuhimu unaovipa baadhi ya vitu siyo sahihi. Unahitaji baadhi ya vitu kwa kiasi, lakini hakuna unachokihitaji kwa umuhimu sana. Huu umuhimu sana tumeutengeneza sisi wenyewe.
Ukweli mwingine ni kwamba ni vitu vichache sana ambavyo kweli ni muhimu kwenye maisha yetu. Yaani katika vitu vingi ambavyo tunaona ni muhimu, vichache sana ndiyo muhimu kwetu, vingine havina umuhimu kabisa. Yaani maisha yetu yanaweza kwenda vizuri hata kama hatuna vitu hivyo. Umuhimu tulioweka kwenye vitu hivyo ni hofu zetu wenyewe, zinazotusukuma kuona vitu ni muhimu wakati siyo.
Kama bado hujanielewa pata picha ya ugonjwa. Labda wewe mwenyewe au mtu wako wa karibu amewahi kupata ugonjwa. Je ni kipi kilikuwa muhimu wakati huu wa ugonjwa? Utakubaliana na mimi kwamba wakati kama wa ugonjwa, mambo yote ambayo mtu alikuwa anasumbuka nayo anayaweka pembeni na kushughulikia afya yake kwanza. Na katika kipindi hicho, hakuna chochote ambacho anapoteza au kinampita, kwa sababu vitu vingi siyo muhimu.
Ni vitu vipi muhimu?
Vitu vyote vinavyoanzia ndani yako ni muhimu, afya, tabia, nguvu na mengine yanayotokana na wewe ni muhimu sana. Lazima uyazingatie.
Vile vitu vya nje ambavyo vinasaidia vitu hivi vya ndani viweze kufanya kazi vizuri navyo pia ni muhimu. Vitu kama vyakula, mavazi, elimu, kuboresha afya ni muhimu.
Ni vitu vipi siyo muhimu?
Vitu vingine vyovyote ambavyo ukivikosa hutakufa na hutapungukiwa na vile vya ndani, basi siyo muhimu. Vipo vingi unaweza kujiorodheshea wewe mwenyewe kutokana na mazingira uliyopo.
Ufanye nini?
Vipe umuhimu vile vitu ambavyo ni muhimu kweli. Na kama siyo muhimu usikubali vipoteze muda wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK