Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya. Tutumie muda wa leo vizuri rafiki.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUACHA SOKO LIAMUE.
Kumekuwa na tabia ya watu kuponda na kukosoa kile ambacho wengine wanafanya.
Hii imekuwa inatokea sana kwa wale ambao wanafanya kazi au biashara ya aina moja. Utaona mmoja akisema wale wanakosea, wale hawawezi kama sisi, au wale hawajui na maneno mengine ya aina hiyo.
Baadhi ya watu wabakuwa wanaona wao kwa mtazamo wao, wako sahihi kuliko wengine wanaofanya kama wao.
Lakini ukweli ni kwamba, watu wanatofautiana, siyo kila mtu anaweza kuwa au kufanya kama unavyofanya wewe.
Hivyo basi, badala ya kutumia nguvu kuonesha nani yupo sahihi na nani anakosea, ACHA SOKO LIAMUE. Soko, yaani wateja, walaji au watumiaji, watatumia kile ambacho kinaendana na matakwa yako. Na kama mtu anatoa ambacho hakiendani na matakwa yao, hawatakitaka, na hapo kazi au biashara ya mtu huyo itakufa.
Maamuzi ya soko ni kipimo bora iwapo kama mtu anafanya kazi au biashara yake kwa usahihi au la. Weka juhudi kwenye kufanya kile unachofanya kwa ubora, na utatengeneza soko kubwa kwako. Waache wengine wafanye kile walichoamua kufanya, na soko litaamua lenyewe. Dunia ya sasa hakuna anayelazimishwa kununua au kitumia kitu, watu wanafanya kwa mahitaji yao wenyewe.
Acha soko liamue lenyewe, hiki ndiyo kipimo bora kabisa kama mtu yupo sahihi au la.
Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amaani.
N;B KUNA NAFASI YA MWISHO KABISA KUSHIRIKI SEMINA YA MILIONI YA ZIADA, LEO KABLA YA SAA SITA MCHANA, PIGA 0717 396 253. KARIBU.