Kila mtu ana upekee wake, hata mapacha wa kufanana waliozaliwa pamoja, bado wanakuwa na maisha tofauti wakishakuwa watu wazima. Hii ni kwa sababu kuna vitu ambavyo vinawajenga watu kuwa na maisha ambayo wanakuwa navyo, na vitu hivi vinatofautiana kwa watu.
Uko hivyo ulivyo sasa, kwa sifa zote ambazo tayari unazo, kutokana na vitu vitatu ambavyo umekuwa navyo mara zote. Vitu hivi vitatu ndiyo vimekuengea wewe sifa uliyonayo sasa, iwe ni nzuri au mbaya.
Kama utapenda kubadilika, unahitaji kubadili kwanza vitu hivi vitatu. Uzuri ni kwamba vitu hivi havitegemei umri, elimu, kabila au hadhi ya mtu ya kimaisha. Mtu yeyote anayeweza kuweka sawa vitu hivi vitatu, atakuwa na maisha anayoyataka yeye.
Je ni vitu gani hivyo?
1. Hisia.
Hisia ambazo unazipata juu yako na juu ya wale wanaokuzunguka, zinachangia sana hapo ulipo. Kama unapata hisia chanya kama upendo, kujali na hata furaha, lazima uwe na maisha bora. Lakini kama unapata hisia hasi kama chuki, wivu na hasira, maisha yako lazima yatakuwa magumu wakati wote.
2. Fikra.
Upo hapo ulipo sasa, kutokana na fikra ambazo umeweka kwenye akili yako. Maisha yako, kazi au biashara yako na kila unachopitia, ni zao la fikra zako. Wazungu wanasema YOU BECOME WHAT YOU THINK. Yaani unakuwa vile unavyofikiri.
3. Matendo.
Uko hapo ulipo leo kutokana na matendo uliyofanya siku zilizopita. Hatua ulizochukua siku za nyuma ndiyo zimekufikisha hapo ulipo. Hatua unazochukua leo, ndizo zitakutengenezea maisha yako ya kesho. Kama ulichukua hatua ya kuweka juhudi kwenye kile ulichochagua kufanya, leo utakuwa kwenye nafasi nzuri. Ila kama uliamua kufanya kwa mazoea, leo utakuwa kwenye hali ngumu.
Ufanye nini?
Linda na dhibiti kabisa mambo haya matatu.
Dhibiti hisia zako, uwe na hisia chanya muda wote, dhibiti mawazo yako, usikubali fikra hasi zikuingie na chukua hatua sahihi kwa kila mahali unapokuwa.
Hisia, Fikra na Matendo, vitu hivi vitatu ndiyo vimekufikisha hapo ulipo sasa, na vitaweza kukufikisha mbali zaidi kama ukiweza kuvitumia vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK