Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba fedha inabadili watu, kwamba baadhi ya watu wamebadilika baada ya kupata fedha.
Lakini ukweli ni kwamba, fedha haiwezi kumbadili mtu. Fedha inamboresha mtu kwenye kile ambacho tayari anacho. Kama mtu ana roho nzuri basi akiwa na fedha anakuwa na roho nzuri zaidi. Na kama mtu ana roho mbaya, basi akiwa na fedha roho mbaya yake inaonekana vizuri zaidi.
Wapo wengine wengi ambao wamekuwa wakilalamikia fedha kuwatawala. Watu hawa wanapokuwa na fedha, hawawezi kutulia mpaka fedha hizo ziishe. Wakiwa hawana fedha wanakuwa na mipango mizuri sana, ila wakishakuwa na fedha mipango ile mizuri yote inafutika na kuja mipango mipya ya matumizi, ambapo fedha zikiisha ndiyo unagundua haikuwa muhimu kama ulivyofikiri awali.
Ujanja ambao unatakiwa kuwa nao kwenye fedha ni wewe kuitawala fedha, na siyo kuiruhusu fedha ikutawale wewe.
Unawezaje kuitawala fedha?
Anza kwa kujinyima matumizi ya fedha uliyonayo. Inakuwa hivi, tembea na fedha ambayo unaweza kuitumia lakini usiitumie kwa jambo lolote. Yaani unakuwa a fedha, na unahitaji fulani, lakini usitumie fedha hiyo.
Kwa mfano una fedha mfukoni mwako na una njaa, lakini unachagua kutokula. Hii inaijengea akili yako uvumilivu na kutokuendeshwa. Hii inakufanya uwe na utawala kwenye fedha, ufanye kitu kwa sababu umeamua kufanya na siyo kwa sababu fedha inakusukuma kufanya.
Kama fedha imekuwa inakupa changamoto kuitawala, hebu anza na zoezi hili, tembea na fedha na usiitumie kwa njia yoyote ile. Mwanzoni itakuwa vigumu lakini baadaye utazoea na utaweza kuzitawala fedha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK