Namshukuru Mungu kwa siku hii ya leo, nimeamka salama nikiwa na afya njema ambayo imenipa hamasa ya kuendelea kufanya kazi kama siku zote. Hata wasomaji wa Amka Mtanzania naamini mungu anaendelea kuwabariki na kupata kile mnachostahili kwa wakati. “Kwa umoja wetu tunasema asante msanifu wa sayari na maumbile yetu hakuna msanifu bora Zaidi yako” Mbali na kuandika mara kwa mara kuhusu uwekezaji wa ardhi na majengo, leo ningependa kuzungumza na watu wenye ndoto ya uwekezaji ingawa kipato chao ni kidogo, Nimeona watu wakilalamika kwamba uwekezaji huu wa ardhi na majengo haiwezekani kwa watu kama wao bali inawezekana kwa wengine tu walionacho zaidi. Inashangaza kuona Watu wengi wameweka juhudi kutafuta uwekezaji ambao ni rahisi kufanya na itakayowaletea mafanikio ya haraka. 

Ukweli ni kwamba hakuna aina ya uwekezaji ambao ni wa muda mfupi kufanya na kuwa tajiri kwa utimilifu. Uwekezaji wa ardhi na majengo una changamoto zake hata kama una kipato kikubwa kiasi gani, muhimu ni maarifa na hamasa ndiyo itakayokupa ushindi. Hivyo kigezo cha kuwa na kipato kidogo hakipaswi kuwa kikwazo cha kusonga mbele, bali hamasa ya uwekezaji unaotaka kufanya. Hivyo basi leo nimekuletea mambo muhimu ya kuzingatia ili ufike pale unapotarajia kufika pasipo kujali au kuhofia kushindwa kwa sababu ya kipato chako kuwa duni. 

Naamini leo hii utaianza safari yako ya mafanikio pasipo hofu ya kushindwa hata kama itachukua muda mrefu kiasi gani maadamu mwisho wa safari iwe ya furaha na yenye tija kwako na kwa jamii iliyokuzunguka.

1. NIDHAMU YA FEDHA
Ukweli ni kwamba watu wengi wamekuwa na malengo na matarajio makubwa sana juu ya maisha yao kiasi kwamba licha ya kupata mshahara na ujira mdogo tofauti na malengo yao bado wanafanya bidii mno katika shughuli nyingi wanazozifanya, wengine hulazimika kufanya shughuli zaidi ya moja kukuza uchumi wao ili angalau waweze kuendesha maisha yao na kukidhi mahitaji yao na wanaowategemea. Lakini idadi kubwa ya watu tuna matumizi makubwa Zaidi ya kipato chetu, wakati mwingine tunazidiwa na matumizi yasiyo na ulazima, tunalazimika ili twende sambamba na walimwengu wengine. Ndugu na rafiki yangu fahamu kwamba kila mtu anaishi kwa ndoto zake, unachopaswa wewe ni kuwa na nidhamu ya kile unachokipata na kupangilia matumizi. Nidhamu pekee ndiyo itakayo kufanya ufikie malengo yako kwa wakati, nidhamu pekee ndiyo itakayokufanya uweke akiba kwa ajili ya uwekezaji ndani ya muda muafaka. Mara zote huwaambia marafiki zangu kuwa usipojitahidi kuweka akiba sasa, upo uwezekano mkubwa wa kuangamizwa na umaskini siku zijazo. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele ndivyo gharama za maisha zinavyozidi kupanda kutokana na ushindani wa maisha kuongezeka huku fursa zikiwa ni chache. Muda sahihi wa kufanya maamuzi na kuanza kuweka akiba ni sasa, tathmini malengo yako na jiulize maswali muhimu, je unahitaji kiasi gani cha fedha na muda ili kufikia hitaji la uwekezaji wako. Huna sababu ya kuzeeka huku ukiwa na msongo wa mawazo, huna sababu yoyote ya kufa maskini ikiwa leo hii una nguvu na uwezo wa kufanya lolote upendalo. Timiza ndoto zako inawezekana.

SOMA; Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa”

2. MAARIFA YA UWEKEZAJI
Maarifa ni silaha namba moja ya mafanikio yako katika uwekezaji, maarifa ni ngao yako dhidi ya umaskini na karaha zote za maisha. Haijalishi una kiwango gani cha elimu, maarifa ya uwekezaji wa majengo ni muhimu sana. Ni lazima upate maarifa ya jambo husika kabla ya kuanza kulifanyia kazi, pasipo maarifa sahihi ya uwekezaji wako ni rahisi sana kukwama, maarifa ya uwekezaji wa ardhi na majengo ni muhimu sana ili uweze kutembea na kufikia malengo pasipo kukata tamaa, watu wengi wamekata tamaa kwa kutokuwa na uhakika wa kufanikiwa kwa jambo walifanyalo, matokeo ya kushindwa huumiza moyo na hata wakati mwingine mwili hudhoofu. Mara zote huwashauri marafiki zangu kuwa kabla ya kuanza safari zao za uwekezaji ni vema wapate mwalimu wa kuwafundisha na hata kuwaongoza. Rafiki yangu mpendwa jitahidi sana kila siku kuongeza ujuzi na maarifa kuhusu uwekezaji wako na biashara uifanyayo ili kuongeza ufanisi na kupunguza uwezekano mkubwa wa kushindwa. Kitu cha muhimu kukumbuka ni kwamba, katika maisha ya sasa ni vigumu sana kufanikiwa ukiwa mwenyewe pasipo kuwa na watu wanaokuzunguka kukujenga na kukuongoza kimawazo katika kufikia malengo yako.

SOMA; Epuka Migogoro Ya Ardhi Isiyo Na Ulazima Ili Uyafikie Mafanikio Yako Kwa Uhakika

3. TOA HUDUMA ZINAZOGUSA JAMII
Watu wote waliofanikiwa sana ni wale waliogusa maisha ya watu wengi. Dunia ya leo ukitaka kupata chochote unachotaka unahitaji kuwasaidia watu wengi kupata vile wanavyotaka. Nikiwa na maana kwamba kile unachokifanya lazima kiwe kinagusa maisha ya watu wengine. Unapaswa kujiuliza unawafikia watu kiasi gani kwa huduma unayotoa, je unapata marejeo ya huduma unayotoa, je uwekezaji unaofanya unakidhi na kufurahiwa na wote wanaofikiwa au kuipata huduma zako. Kama unachokifanya hakigusi maisha ya wengine ni wazi kuwa unapaswa ubadili mtazamo wako wa hicho unachokifanya. Kwa kugusa maisha ya watu wengine ndipo na wao wanapotoa fedha zao ili uendelee kuwagusa kupitia uwekezaji wako. Kama unachokifanya kinaleta furaha kwenye maisha ya wengine hawataacha kutoa fedha zao mfukoni kukupatia ili uwape huduma zaidi. Wakati mwingine maisha ni Zaidi ya fedha bali utu na haiba yako kwa wengine ni njia yako ya mafanikio. Ni ukweli usiopingika kwamba unahitaji watu wengi sana ili ufanikiwe. Chochote kile unachokifanya kwenye dunia hii ili ufikie mafanikio makubwa unahitaji watu wengi zaidi. Wewe uliyejenga nyumba ya makazi hakikisha wakazi wako wanafurahia mazingira yako, uliyejenga karakana hakikisha miundombinu inakidhi watumiaji wako. Na wewe mwenye ndoto ya kuwa na mgahawa wa kisasa, saluni ya kisasa, shule ya kisasa, gereji ya kisasa, maduka ya kisasa na makazi ya mifugo ya kisasa usife moyo bali anza safari yako kwa nguvu zote. Watu wengi wa sasa wapo tayari kugharamia mahali ambapo wanapata kilicho bora.

SOMA; Mambo Muhimu Unayopaswa Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Greenhouse.

4. HAMASA YA UWEKEZAJI
Hakuna mafanikio pasipo changamoto, hakuna ushindi pasipo mapambano na hakuna furaha pasipo amani. Kama utambuavyo kuwa tupo hapa tulipo kutokana na matokeo ya mawazo yetu. Fikra na Mawazo yetu ndiyo yanayoakisi namna tulivyo na tutakavyokuwa. Watu wote waliofanikiwa wana siri nzito nyuma yao, karibu wote watakwambia ni msukumo mkubwa walionao wa kupambana na umaskini na kufikia ndoto zao. Safari zao za mafanikio zilijaa changamoto na vihoja vya kusikitisha lakini hamasa ndio silaha yao kuu iliyowafanya wasigeuke nyuma na hata kufikia utimilifu wao. Kwa watu walio na kipato kidogo wanahitaji hamasa Zaidi ili wafikie ndoto zao katika uwekezaji wa ardhi na majengo. Hii ni kutokana na kuhitaji muda mwingi Zaidi tofauti na wale wenye kipato cha kati na kuendelea ili kufikia viwango vya kisanifu. Hatua ya kwanza ni kuwa na eneo, huwezi kujenga kwa wakati huo weka mazingira kwa ajili ya matumizi mengine ambayo ni ya muda mfupi huku ukijipanga, leo hii wapo watu wengi wanaotafuta maeneo ya wazi kwa ajili ya kufanyia shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.

Hamasa ina ushawishi mkubwa sana katika maisha yetu, hamasa ndiyo inayosababisha kufanyika kwa maamuzi yenye ujasiri wa ushindi. Rafiki yangu nakusihi sana jitahidi kujifunza na mara zote kuwa tayari kupokea mawazo mapya. Pale unapofikiria na kujiona kwamba unajua kila kitu, ndiyo unakuwa mwisho wako wa kukua na kufanikiwa. Ili kufanikiwa kwenye maisha ya uwekezaji ni muhimu uwe tayari kujifunza kila siku ili uhamasike zaidi.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com